NA MWANDISHI WETU
18th May 2013
Wakazi wajifungia ndani kwa hofu
Shughuli za maendeleo zasimama.jpg)
Hatua hiyo ilitokana na fununu za kutokea ghasia, vurumai na mashambulizi yanayotokana na wananchi kupinga usafirishwaji wa gesi hiyo.
Shughuli za biashara na nyingine za kijamii zilisimama na kuhusisha taasisi kama ofisi za umma na binafsi, shule, hospitali na masoko.
Dalili za kuibuka hofu hiyo zilianza kujitokeza Jumanne wiki hii, baada ya baadhi ya vipeperushi kutawanywa katika mitaani mbalimbali ya manispaa ya Mtwara Mikindani.
Vipeperushi hivyo viliwahamasisha wananchi kuacha kufanya kazi siku ya Ijumaa, wakijua kwamba bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini itaposomwa bungeni, ili wajue hatma ya gesi iliyopo mkoani Mtwara. Lakini kulingana na ratiba, hotuba hiyo imepangwa kuwasilishwa wiki ijayo Mei 22.
Hata hivyo, bajeti iliyosomwa ilikuwa ya wizara ya uchukuzi inayoongozwa na Waziri wake, Dk Harrison Mwakyembe.
Baadhi ya shule za msingi zikiwamo Raha Leo na Maendeleo, wanafunzi hawakuonekana madarasani.
Hata hivyo, ilisemekana kwamba wanafunzi 160 kati ya 782 wa Raha Leo, walihudhuria asubuhi kisha kurejea nyumbani.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Vincent Hokororo, alithibitisha kutokuwapo kwa wanafunzi shuleni hapo jana.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maendeleo, Fabiola Haule, wanafunzi 184 kati ya 571 waliwasili asubuhi, hali ambayo haijawahi kutokea.
USAFIRI
Usafiri kwenye stendi kuu ya mabasi haukuwepo kuanzia asubuhi. Daladala na bodaboda zilisimama kutoa huduma kutwa nzima huku magari yanayosafirisha abiria mjini hapa yakiegeshwa.
Safari za mabasi yanayopeleka abiria wanaosafiri kutoka kituo kikuu cha mabasi Mtwara kwenda wilaya za Tandahimbi , Newala , Masasi na Nanyumbu hayakufanyakazi, licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, kusisitiza kuwa mabasi hayo yalisafiri.
Hata hivyo, mabasi ya masafa marefu kati ya Dar es Salaam na Mtwara na mikoa mingine yalisafirisha abiria alfajiri.
HOSPITALI YA RUFAA LIGULA
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dk Sadud Kabuma , alisema hospitali haikuwa na wagonjwa wengi kama ilivyo kawaida, isipokuwa wachache waliohitaji matibabu ya dharura.
Kwenye maeneo ya masoko, hapakufanyika biashara huku eneo lililoathirika zaidi likiwa ni soko kuu la mjini humo.
Meneja wa Soko Kuu la Mtwara, Hamza Liteta, alisema wamekosa ushuru wa bidhaa unaotozwa.
Pia alisema wauzaji na wachuuzi walipata hasara kutokana na wa kuwa hawakufanya biashara kutwa nzima.
MADUKA
Maduka mengi yalifungwa tangu asubuhi, wakati wafanyabiashara wakihofia uharibifu wa biadhaa wanazouza.
BENKI ZAKOSA WATEJA
Hapakuwa na msongamano wa wateja kwenye benki nyingi za mjini hapa, ikielezwa kutokana na hofu hasa ya kuporwa fedha.
Meneja wa NBC Tawi la Mtwara , Nestory Mwakiokile, alisema utoaji huduma jana hakufanyika kama ilivyozoeleka na kwamba wateja hawakuonekana, wakihofia kuporwa ama kughasiwa.
POLISI WAUZINGIRA MJI
Polisi waliokuwa kwenye magari ya doria `walizagaa’ kwenye maeneo kadhaa ya mji wengine wakishika doria kwa kuweka kambi ndogo katika sehemu zinazohofiwa kuwa watu wengi.
Katika doria hizo polisi walikuwa na silaha pamoja na maji ya kuwasha, mabomu ya machozi na virungu.
Walikuwa wametanda sehemu za Bima, Soko Kuu, Magomeni na mitaa ya Majengo.
NYUMBA ZA VIGOGO ZALINDWA
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, alisema polisi iliimarisha ulinzi kwenye nyumba za ibada-misikiti na makanisa na nyumba za viongozi.
Sinzumwa alisema ulinzi mkali umewekwa kwenye nyumba za Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mchuchika, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa , Hawa Ghasia na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara Mohamed Sinai.
KAULI YA POLISI
Sinzumwa, alisisitza kuwa hali ni shwari na kwamba hadi jana hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa kuhusiana na kusambaza vipeperushi vilivyochochea taharuki hiyo.
Alisema usafiri ukiwamo wa bodaboda umerejea wakati wananchi wanatembea mitaani isipokuwa, maduka yaliendelea kufungwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment