AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, May 15, 2013

Muhongo: Tanesco imeshindwa

NA RICHARD MAKORE

15th May 2013


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia ) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu masuala ya umeme nchini. Wengine ni Balozi wa Sweden nchini, Lennarth Hjelmaker (kushoto) na Waziri wa Biashara wa Sweden, Gunnae Oom.
Serikali imetangaza kwamba itaanza kuliboresha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kwa lengo la kuleta ufanisi katika sekta ya umeme kwa kuwa kwa miaka 49 tangu lianzishwe limeshindwa kupata ufumbuzi wa matatizo ya umeme.

Katika kuliboresha shirika hilo kazi ya kuunganisha umeme itatekelezwa na Tanesco wakati uzalishaji na usambazaji utafanywa na kampuni za uwekezaji za ndani na za nje.

Kauli hiyo ya serikali ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye kikao kati yake na Waziri wa Biashara wa Sweden, Gunnar Oom.

Hata hivyo, Profesa Muhongo hakufafanua zaidi lini muundo mpya wa shirika hilo utakapoanza kufanyakazi.

“Kazi ya kuunganisha umeme itabaki kwa serikali, lakini uzalishaji na usambazaji wa nishati hiyo watapewa wawekezaji wenye uwezo wa kufanya kazi ili kuhakikisha wananchi wengi wanafikiwa na huduma hiyo,” alisema.

“Tanesco imeelemewa na mzigo na hapo ilipo haiwezi kumaliza tatizo la umeme nchini, hivyo tunatafuta wawekezaji watakaowezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa bei ndogo na unaotabirika,” aliongeza Profesa Muhongo.
Alisema zama za kutegemea wafadhili kufadhili miradi mikubwa ikiwamo ya umeme zimepitwa na wakati, badala yake serikali hivi sasa inajikita kutafuta wawekezaji wenye uwezo wa kutatua tatizo la umeme lililodumu nchini kwa kipindi kirefu.

Alifafanua kuwa licha ya Tanesco kuanzishwa mwaka 1964, bado ni asilimia 21 ya Watanzania wanaopata umeme na kati ya hao, asilimia saba wakiwa wapo maeneo ya vijijini. Profesa Muhongo alisema serikali imedhamiria ifikapo mwaka 2015, uzalishaji wa umeme uwe umefikia megawati 3,000 na asilimia 30 ya Watanzania wawe wanapata umeme wa uhakika.

“Siyo sahihi Watanzania kuendelea kutegemea maji kama chanzo kikuu cha kuzalisha umeme bali umeme uzalishwe kwa kutumia upepo, jua, makaa ya mawe, gesi asilia na maporomoko ya maji,” alisema.

Profesa Muhongo alisema kazi iliyomuweka ofisini ni kutafuta ufumbuzi wa tatizo la umeme na siyo kuangalia mafaili ya kutaka kujua nani aliiba ama kuanza kujadili watu.

Alisema miundombinu ya kusafirisha umeme unaozalishwa imechoka na kwamba asilimia 23.4 unapotea njiani kabla ya kumfikia mtumiaji na kuongeza kuwa wanawahamasisha wawekezaji kuwekeza kwenye miradi ya kuzuia upoteaji huo.

“Serikali pekee haiwezi kumaliza tatizo hili la umeme kwa kuwa suala hili siyo kama kujenga shule, ni miradi inayohitaji fedha nyingi na serikali haiwezi kumudu,” alisema Profesa Muhongo.

Kuhusu bajeti ya wizara yake inayotarajiwa kusomwa bungeni Mei 22, mwaka huu, Profesa Muhongo alisema itakuwa ya kipekee na ya kisasa ambayo itakuwa na majibu yote kuhusu matatizo ya umeme nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara wa Sweden aliyekutana na Profesa Muhongo, alisema maendeleo ya nchi yanahitaji mabadiliko kutoka utegemezi wa mikopo ya wafadhili katika biashara na uwekezaji.

Alisema kutegemea mikopo ya wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya nchi siyo njia sahihi hususani kwa nchi zinazoendelea.

Aliongeza kuwa kampuni zao zipo tayari kuwekeza nchini kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Sweden uliodumu kwa zaidi ya miaka 50.

Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri Muhongo kuweka hadharani kwamba njia pekee ya kuinasua Tanesco hapo ilipo tangu ashike madaraka hayo mwaka jana, lakini akirejea kwenye mkakati wa kuigawanya Tanesco ambao ulikuwa wa serikali ya awamu ya tatu, lakini awamu ya nne ikaona haufai. Ingawa mgawanyo huo sasa unapigiwa chapuo, serikali imekuwa inakwepa kueleza ukweli kwamba miongoni mwa mambo yanayoiua Tanesco ni serikali yenyewe kutokulipa madeni yake ya matumizi ya umeme, lakini pia mikataba mibaya ya kuuziana umeme kutoka kampuni binafsi za kuzalisha nishati hiyo.

Wakati wa bajeti ya wizara hiyo mwaka jana, nguvu kubwa ilielekezwa kuwatuhumu baadhi ya maofisa waandamizi wa Tanesco kama chanzo cha kuzorota kwake, lakini pia wakiwatuhumu baadhi ya wabunge kuwa walikula rushwa ili kukwamisha shughuli za wizara.

Kwa miaka mitatu sasa wizara ya Nishati na Madini imekuwa na wakati mgumu bungeni kutokana na upatikanaji nishati hiyo kutokufikia matarajio ya wananchi wengi.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment