Wabunge waipinga NSSF
13th May 2013
.jpg)
Wabunge jana walikuja juu na kuishambulia mifuko ya hifadhi ya jamii wakisema kuwa haiwanufaishi wanachama wake.
Moja ya mambo ambayo wabunge hao walilalamikia katika semina hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA), ni kuwa wanachama hawanufaiki ni bei kubwa za nyumba zinazouzwa na mifuko hiyo.
Malalamiko hayo waliyatoa jana wakati wa semina ya wabunge kuhusiana na mifuko hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Kiwanga, alisema Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umekuwa ukitoa huduma za matibabu kwa wanachama wao katika hospitali zisizo na ubora unaotakiwa.
Alitoa mfano wa hospitali ambazo zinatoa huduma ya matibabu kwa wanachama ni Hospitali ya Tumaini huku wafanyakazi wa mfuko huo wakitibiwa katika hospitali nzuri ya Regency.
Moja ya mambo ambayo wabunge hao walilalamikia katika semina hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA), ni kuwa wanachama hawanufaiki ni bei kubwa za nyumba zinazouzwa na mifuko hiyo.
Malalamiko hayo waliyatoa jana wakati wa semina ya wabunge kuhusiana na mifuko hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Kiwanga, alisema Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umekuwa ukitoa huduma za matibabu kwa wanachama wao katika hospitali zisizo na ubora unaotakiwa.
Alitoa mfano wa hospitali ambazo zinatoa huduma ya matibabu kwa wanachama ni Hospitali ya Tumaini huku wafanyakazi wa mfuko huo wakitibiwa katika hospitali nzuri ya Regency.
“Mimi nashangaa wanachama wa NSSF wanaenda kutibiwa katika hospitali ya Tumaini pale kuna nini? Wakati wao (watumishi wao) wanaenda kutibiwa katika hospitali ya Regency,” alisema.
Kiwanga alisema pia wakati mwanachama anajiunga na NSSF haambiwi kuwa mikopo itakuwa ikitolewa katika vyama vya kuweka na kukopa (Saccos). lakini wakishajiunga wamekuwa wakielezwa iwapo wanataka mikopo hiyo wanatakiwa kujiunga katika vyama hivyo
Aidha, alihoji suala la kutoa mafao kwa wanachama baada ya miaka 60 kwamba linaziweka familia katika wakati mgumu.
“Mimi ni mwanachama wa Mfuko wa NSSF, sina uhakika kama nitarejea tena bungeni baada ya miaka mitano, nitawezaje kuchangia tena katika mfuko huu wakati mnasema muda wa kunufaika na pensheni hadi miaka 60,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Christowaja Mtinda, alisema NSSF imekuwa ikiwaibia wanachama kwa sababu hakuna nyumba inayojengwa na shirika hilo ambayo mwanachama anaweza kuinunua.
Alitoa mfano wa nyumba ambazo zinauzwa kwa Sh. milioni 103, halafu makato kwa mwezi ni Sh. milioni 1.6.
Alihoji ni mwanachama gani ambaye anaweza kulipa kiasi chote hicho cha fedha kama sio wizi huo?
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy, alisema mifuko ya jamii inawaibia wanachama, haiwezi kuuza nyumba kwa Sh. milioni 70 wakati yeye mwenyewe amejenga nyumba nyingi kwa Sh. milioni 30.
Alisema kuwa nyumba zenyewe ni za hovyo na kuwa nyumba ya vyumba viwili inauzwa kwa Sh milioni 70 wakati anaweza kujenga nyumba ya vyumba vitatu ama vine kwa Sh. milioni 30.
Keissy alisema pia mifuko hiyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wafanyabiashara wakubwa na wakati mwingine wanashindwa kulipa.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, alisema mifuko hiyo imekuwa ikiwekeza katika kujenga majumba makubwa, lakini haijihusishi katika miradi itakayoinua uchumi wa nchi.
Alisema katika nchi nyingine duniani mifuko imekuwa ikiwekeza katika miradi ya kuinua uchumi kama vile ujenzi wa miundombinu, miradi ya umeme na maji, lakini hapa nchini wamekuwa wakijenga majengo tu.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah, alihoji kazi iliyofanya Tume ya Huduma za Bunge katika kushughulikia mafao ya wabunge.
“Kwanini Tume ya Bunge haisikilizi na kufanyia kazi masuala ya wabunge na kwanini haifanyii kazi malalamiko ya wabunge?” alihoji.
Mbunge wa Kondoa Kusini (CCM), Juma Nkamia, alisema umri wa Mtanzania wa kuishi ni miaka 45, lakini mifuko inaruhusu mtu kuchukua mafao yake baada ya miaka 60.
Alisema hatua hiyo inafanya watoto na wategemezi kuishi maisha ya taabu mwanachama anapofariki kabla ya kufikia umri huo.
Alihoji kama mifuko hiyo ina mpango na Mungu wa kumpangia maisha ya kuishi mwanadamu.
Mbunge wa Ileje (CCM), Aliko Kibona, alisema SSRA, uko kwa ajili ya kusimamia stahili za wanachama wote na inakuaje wameshindwa kutoa jibu linaloeleweka kuhusiana na fao la kujitoa.
MAJIBU YA SSRA
Mkurugenzi Mkuu wa SSRA , Irene Isaka, alisema mgongano wa fao la kujitoa bado unashughulikiwa.
Kuhusu gharama kubwa za nyumba, Isaka alisema kuwa mifuko hiyo imekuwa ikiitisha kandarasi na kufanya manunuzi pamoja na taratibu nyingine ambazo zinafanya bei ya nyumba kuwa kubwa.
“Sisi kama SSRA tunatarajia baada ya kuweka pamoja mafao, tutaweka miongozo ya nyumba na mtu atakopeshwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama kujenga katika kiwanja au kununua kiwanja chenye maji na umeme,” alisema.
Kuhusu kukopesha mtu mmoja, alisema mifuko hiyo imeanzisha utaratibu huo wa vikundi ili iwe rahisi kufuatilia marejesho ya mikopo hiyo.
NSSF YAJIBU
Akizungumza na NIPASHE jana baada ya semina ya wabunge, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Oigo James, alisema hospitali za matibabu kwa wanachama wao ni nyingi na siyo mbili kama inavyodaiwa.
Alisema kwa Jiji la Dar es Salaam pekee kuna hospitali 40 ambazo mwanachama anaweza kupata matibabu zikiwamo Regency na Tumaini.
Alisema suala la matibabu limeibuliwa kutokana na Hospitali ya Tumaini kuwa kwenye kipindi cha mpito kilichosababisha matibabu kuyumba.
“Mwanachama anaruhusiwa kutibiwa hospitali yoyote kwa matakwa yake, wapo waliojiandikisha kutibiwa Tumaini ilivyoyumba ndipo malalamiko yakajitokeza na kuna wakati ilivunja mkataba na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na wanachama wetu walivyokwenda kujitambulisha wana bima wakaambiwa hakuna mkataba, tuliwaelewesha wafanyakazi na sasa huduma zipo,” alisema.
Kuhusu nyumba, Oigo ambaye pia ni Meneja wa Mafao wa NSSF, alisema kuna utaratibu wa kununua moja kwa moja na kuingia mkataba na benki ya Commercial Bank of Africa (CBA), ambayo imebainika ina riba kubwa.
Alisema riba hiyo imesababisha bei ya nyumba kuonekana kubwa na kuzua malalamiko na kwamba wapo kwenye mazungumzo na benki ili kuangalia uwezekano wa kupunguza riba hiyo na kuwawezesha wanachama wa kipato cha kawaida kununua nyumba hizo.
Alisema suala la Saccos linatokana na baadhi ya wanachama ambao hawana sifa zinazotakiwa kwenye vyama vyao kutaka kukopa mikopo mikubwa.
Alisema Saccos nyingine zinataka kukopa kiwango kikubwa kuliko uwezo wake kwenye usajili na zimezuka Saccos za mfukoni ambazo hazikidhi vigezo vya kupewa mikopo.
Imeandikwa na Sharon Sauwa na Jacqueline Massano, Dodoma na Salome Kitomari, Dar.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment