NA MHARIRI
30th June 2013
Kiongozi huyu anaitembelea Tanzania wiki inayoanza kesho, ikiwa ni miaka mitano baada ya mtangulizi wake, Rais mstaafu George Bush kuzuru taifa hili na kuwapatia Watanzania msaada wa karibu Dola milioni 700.
Marekani ni rafiki mkubwa wa Tanzania na taifa hili kubwa limekuwa mstari wa mbele katika kusaidia juhudi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kuanzia malaria, VVU na Ukimwi nishati na mawasiliano.
Kwa mfano sekta ya afya, Watanzania wengi wamenufaika na dawa za kufubaza makali ya VVU wakiwamo wajawazito na watoto zilizotolewa kupitia Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR). Mbali na kupata dawa hizo wagonjwa wa kifua kikuu wametibiwa pia.
Shirika la Changamoto za Milenia (MCA) la Marekani nalo ni jina lenye nafasi kubwa ndani ya mioyo ya Watanzania ambapo limefanikisha miradi mingi ikiwamo ujenzi wa barabara mkoani Tanga, Ruvuma, miradi ya kuboresha upatikanaji wa umeme na nishati umejengwa Dodoma na Jijini Dar es Salaam.
Mambo ni mengi na Tanzania ina kila sababu ya kufungua moyo na kumkaribisha Rais Obama pamoja na familia ya ujumbe wake kwa kuipa heshima ya kipekee kuitembelea.
Hii ni fursa adimu ambayo mataifa mengi yanaitamani hivyo tumpokee kwa mikono miwili na kumpa ukarimu na heshima zote. Sisi tunasema karibu sana Rais Obama na asante sana kwa kuizuru Tanzania .
Ujio wa Rais Obama unaipa Tanzania mng’aro kimataifa kwani macho yote duniani hivi sasa yameelekezwa Afrika na hasa Tanzania ambako anatarajia kufanya ziara ya kiserikali kwa takribani siku mbili wiki inayoanza kesho.
Kuja kwake Tanzania hajakosea hata kidogo. Anajua kwanza hiki ni kisiwa cha amani, na pili kidiplomasia ni rafiki wa muda mrefu katika njanja mbalimbali za maendeleo. Na ndiyo maana kuja kwake kutakuwa kwa manufaa makubwa kiuchumi na kijamii.
Kwa ujumla, ushawishi wa Marekani kwenye siasa za kimataifa unaihakikishia nchi yetu kuwa inakubalika popote duniani na wawekezaji wakubwa wanaweza kuja na kuwekeza nchini.
Ziara ya Rais Obama kama chachu ya kushirikiana na Washington kujiendeleza kiuchumi hasa kwenye sekta ya miundombinu hasa reli na viwanja vya ndege na uimarishaji wa barabara hasa kwenye mikoa maarufu kwa kilimo na uzalishaji.
Bila kusahau sekta ya afya ambayo inahitaji kuwa na hospitali kubwa ya kisasa na yenye huduma za kukidhi mahitaji ya sasa ili kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa ng’ambo. Tunaamini Serikali itatilia mkazo umuhimu wa kushirikiana na taasisi za Marekani kama Abbott na Chuo Kikuu cha John Hopkins kufanikisha jitihada hizo.
Ni dhahiri pasipo shaka kwamba kuwa na ubia na Marekani kwenye sekta ya afya kutawezesha kuzalisha matabibu bingwa, wataalamu wa mashine za tiba, maabara na mafundi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano itakayosaidia kuendeleza tiba mtandao na kupunguza gharama kwa lengo la kufikia Watanzania wengi.
Na kusema ukweli, kinachotakiwa ni kwamba ushirika katika afya ulenge pia eneo la utafiti kupunguza magonjwa na kuiwezesha nchi kuzalisha dawa na kukinga maradhi badala ya kuendelea kuyatibu.
Sekta ya Elimu ni eneo lingine ambalo linahitaji ushirikiano na Washington. Ziara ya Rais Obama ifungue njia ya umoja wa kuendeleza elimu kwa kuwa na Chuo Kikuu Mama kitakachowezesha kufunza na kuendeleza wataalamu mabingwa kwenye uchumi, uongozi , biashara, teknolojia kama ilivyo Chuo Kikuu cha Harvard nchini humo.
Uwekezaji wa kiuchumi ni fursa ambazo hazikwepeki . Tanzania ni tajiri wa rasilimali na ina mengi ya kuvutia wawekezaji kutoka Marekani. Ziara ya Rais Obama na ujumbe wake uinue fursa za kiuchumi nchini zitakazowezesha rasilimali kuchakatwa na kuzalisha bidhaa mbalimbali za kuuzwa nje badala ya kuuza malighafi.
Kwa hiyo, tunamkaribisha Rais Obama na ujumbe wake lakini tukiwasihi wawakilishi wetu kwenye mikutano na majukwaa ya ushirikiano wa Marekani na Tanzania kuweka maslahi ya nchi mbele na kuwapatia Watanzania kile wanachotarajia ambacho ni kuwa na ushirikiano chanya utakaoboresha hali ya maisha ya raia wa taifa hili.
Karibu sana Barack Obama. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Marekani.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment