NA JOHN NGUNGE
29th June 2013
Wabunge waipongeza bajeti.jpg)
Hata hivyo, imepandisha kidogo tozo kwa mafuta ya taa ili kuondoa uchakachuaji.
Akiwasilisha majumuisho ya hoja mbalimbali za wabunge kuhusu Muswada wa Sheria ya Fedha bungeni jana, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, hata hivyo, alisema serikali imeongeza ushuru wa barabara.
Alisema ushuru wa barabara umeongezwa kutoka Sh. 200 hadi Sh. 223 kwa lita moja ya mafuta ya petroli na Sh. 200 hadi Sh. 263 kwa lita moja ya mafuta ya dizeli, fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara.
Akifafanua kuhusu tozo za mafuta kama zilivyopendekezwa kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha, Dk. Mgimwa alisema serikali ilipendekeza tozo ya Sh. 400 kwa lita moja ya petroli badala ya Sh. 339 ya sasa.
Kwa upande wa mafuta ya dizeli alisema pendekezo la awali lilikuwa ni tozo ya Sh. 217 kwa lita moja badala ya Sh. 215 ya sasa.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa mafuta ya taa wamelazimika kuongeza kidogo tozo kutoka Sh. 400.30 ya sasa hadi Sh. 425 kwa lita moja.
Alisema awali serikali ilipendekeza tozo liwe Sh. 516 kwa lita moja.
Alielezea kuwa hali hiyo imefanywa kwa lengo la kuzuia uchakachuaji.
Alisema kutokana na tozo hizo, lengo la serikali ni kukusanya Sh. bilioni 298.0993 ambapo tozo ya Sh. 50 itatumika kwa ajili ya kutoa huduma ya umeme vijijini (REA) na Sh. 53 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara.
Kuhusu ushuru wa huduma za simu, Dk. Mgimwa alisema haitahusisha huduma ya kusafirisha fedha kama za M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na nyinginezo kutokana na wabunge kuwasilisha hoja za kukataa huduma hiyo kutozwa ushuru.
Dk. Mgimwa alisema huduma za simu zitakazotozwa ushuru ni za kupiga simu, kutuma picha, milio ya sauti ya simu na nyinginezo lakini sio za kusafirisha fedha.
Katika Bajeti ya Serikali na kwenye mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Fedha, serikali ilitaka kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa katika huduma zote zinazotolewa na simu za aina zote badala ya muda wa maongezi pekee, kutoka asilimia 12 ya sasa hadi kiwango cha asilimia 14.5.
Waziri Dk. Mgimwa alisema kiasi cha asilimia 2.5 cha ushuru huo ni kwa ajili ya kuchangia katika Mfuko wa Elimu ili kugharimia elimu hapa nchini.
Akizungumzia pendekezo la kuongeza ushuru kwa magari yasiyo ya kazi yanayoingizwa nchini yenye umri zaidi ya miaka 10, alisema, halijabadilishwa na kwa maana hiyo litaendelea kuwepo kama lililovyoongezwa.
Serikali imeongeza ushuru huo kutoka asilimia 20 hadi asilimia 25.
Kwa upande wa magari ya kazi yanayaoingizwa nchini yakiwa na umri wa miaka 10, alisema pendekezo la kuongeza ushuru wa asilimia tano halijafanyiwa mabadiliko na litaendelea kuwa kama lilivyo.
Alisema kwa lengo la kupandisha ushuru huo ni kuzuia uharibifu wa mazingira na ajali zinazotokana na uchakavu wa magari hayo.
Hata hivyo, alisema masharti ya uingizaji wa magari mapya yanaendelea kubaki kama yalivyo.
Muswada huo wa Sheria ya Fedha unatarajiwa kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete leo ili uweze kuwa sheria itakayoanza kutumia rasmi Julai Mosi, mwaka huu.
Baadhi ya wabunge wakizungumzia bajeti hiyo, walisema wanaiomba serikali kwa upande wake itekeleze bajeti hiyo kwa kupeleka fedha maeneo husika ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), aliipongeza bejeti hiyo kuwa itasaidia kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Mbunge wa Viti Maalum, Injinia Stella Manyanya (CCM), alipongeza mfumo huu mpya wa kujadili ambao unaanza kwanza kwa kila wizara na baadaye Bajeti ya Serikali.
Alisema utaratibu utasaidia kufikisha fedha za maendeleo kwa wananchi kwa muda muafaka.
CHANZO: ALASIRI
No comments :
Post a Comment