NA GEORGE RAMADHAN
14th August 2013
Mwakyembe akiwa jijini Mwanza jana aliapa kwamba katika kipindi cha wiki mbili kuanzia jana atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vya ndege hapa nchini.
Akihutubia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana yaliyoandaliwa na taasisi ya Jitambue Foundation, yaliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza, alisema kuwa yuko tayari kufa katika vita hivyo.
Kauli hiyo ilifuatia kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Japhet kuhoji sababu za serikali kushindwa kuwachukulia hatua vigogo wanaodaiwa kuwatumia vijana kusafirisha dawa za kulevya na kuwaharibia maisha.
“Nakumbuka mwaka 2006 Rais Jakaya Kikwete aliomba apelekewe majina ya vigogo wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, na yeye mwenyewe alikiri kwamba, ameshapokea majina hayo, lakini hadi sasa hatujasikia kigogo yeyote aliyekamatwa wakati vijana wanazidi kuangamia na dawa za kulevya?” alihoji Japhet.
Akihutubia wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, Waziri Mwakyembe alisema ameshaagiza vyombo vinavyofanya kazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kumpelekea taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wasafrishaji wa dawa za kulevya.
“Dawa za kulevya zinasafirishwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambao umebeba jina lenye utukufu hapa nchini. Hatuwezi kukubali nchi yetu iendelee kudhalilishwa namna hii,” alisema Dk. Mwakyembe na kuongeza:
“Haiwezekani makontena tisa ya dawa za kulevya yamekamatwa halafu leo tunaambiwa ni mtu mmoja amesimamishwa kazi. Hapa kuna mtandao na lazima nitaukamata. Nipeni wiki mbili.”
Alisema atahakikisha anawabana watumishi wa JNIA ili waeleze jinsi dawa za kulevya zinavyopitishwa katika uwanja huo na wawataje wahusika kwa kuwa watakuwa wanawafahamu.
“Ni jambo, ambalo haliingiia akilini kwamba, tuna vyombo vyote vya kudhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya, lakini ukiuliza kwa nini dawa zinapitishwa wanatoa sababu, ambazo hazieleweki.
Nimewapa wiki mbili waniletee taarifa. Kama walikuwa wanafanya hivyo ni huko nyuma siyo leo,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema mbinu zilizotumika kukomesha wizi wa makontena katika bandari ya Dar es Salaam ndizo atakazotumia kukamata mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vya ndege hapa nchini.
Alitoa mfano akisema katika bandari ya Dar es Salaam kulikuwa na upotevu wa mali uliokithiri na kwamba, takriban makontena 30 yalikuwa yamepotea katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu.
Hata hivyo, alisema baada ya kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti wizi bandarini ikiwa ni pamoja na kutishia kukata mishahara ya wafanyakazi kufidia upotevu wowote utakaojitokeza, hivi sasa hali imekuwa shwari.
Alisema licha ya kuwapo kwa vitisho vya kuuawa, lakini hatasita kuchukua hatua kudhibiti uhalifu au uzembe unaofanywa chini ya wizara yake.
“Watu wanafanya uhalifu halafu eti wanatishia nikichukua hatua nitauawa. Kwanza mimi nilishakufa. Ni Mungu tu amenirudishia uhai.
Kwa hiyo, natuma salamu kwa wale wote wanaoingiza au kusafirisha dawa za kulevya kwamba, hawako salama. Siyo Dar es Salaam pekee, hata KIA (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro) na hapa Mwanza,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema anafanya hivyo kutimiza wajibu wake wa kisheria wa kuwatumikia Watanzania akiwa kama waziri aliyepewa dhamana na rais.
“Rais ametuteua mawaziri na kutupatia mamlaka ya kusimamia utendaji chini ya wizara zetu.
Kama kuna waziri anadai hawezi kuchukua hatua kwa sababu hana mamlaka, huyo atakuwa hajui kazi yake,” alisema Dk. Mwakyembe.
Mwakyembe anatoa kauli hiyo zikiwa zimepita wiki tatu tangu apate kigugumizi cha kuwachukulia hatua maofisa wa JNIA walioruhusu shehena kubwa ya dawa za kulevya kupita hadi Afrika Kusini.
walipokamatwa na kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8 nchini Afrika Kusini wakati zikisafirishwa kutoka Tanzania.
Taarifa za kukamatwa kwa wasichana hao nchini Afrika Kusini zilipatikana Julai 5, mwaka huu.
Walikamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya nchi hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, uliopo eneo la Kempton Park, Johannesburg.
Taarifa hiyo ilionyesha wasichana hao walisafirisha dawa hizo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.
Waliokamatwa, ni Agnes Jerald (25), Melisa Edward (24), ambao wameshtakiwa Afrika Kusini.
Awali, Julai 23, mwaka huu, NIPASHE ilizungumza na Dk. Mwakyembe kwa njia ya simu kutoka Kagera, lakini akajibu kwamba, hana taarifa za kina kuhusu sakata hilo.
Hata hivyo, alisema yeye hahusiki nalo kwa kuwa suala la uhalifu linaihusu Polisi na kumwelekeza mwandishi awasiliane na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi au Jeshi la Polisi.
Alipoelezwa kwamba, suala hilo linamhusu kwa kuwa ni vigumu kwa kilo 150 za ‘unga’ kupita uwanja wa ndege bila kujulikana na viwanja hivyo viko chini ya wizara yake, alisema hawezi kuzungumza chochote na kwamba, suala hilo aulizwe Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Suleiman Suleiman.
Hata alipoambiwa watendaji walio chini yake wamekuwa wakipiga danadana bila hata kuchukua hatua ya kuwawajibisha wanaoichafua nchi, alisema: “Hebu kata simu kuna simu inaingia hapa, unajua niko kwenye ziara ya bwana mkubwa huku Bukoba (ziara ya Rais mkoani Kagera).”
Kigugumizi cha Mwakyembe, kiliibua maswali mengi, ambayo yaliashiria kwamba, biashara haramu ya dawa za kulevya itakuwa inahusisha mtandao wa watu wenye nguvu nchini.
Wasiwasi huo ulitokana na ukweli kwamba, makali yake kwa vuwanja vya ndege ni tofauti kabisa na yale aliyoonyesha dhidi Mamlaka ya Bandari (TPA), kwa kuwatimua kazi wakurugenzi wakuu pamoja na kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi kutokana na utendaji usio na tija na hasa baada ya kutokea kwa wizi wa shaba bandarini.
Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.
Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
Pia Watanzania wengine wawili walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hong Kong.
Matukio hayo yanatokea wakati wakuu wa uwanja wa ndege wa JNIA zinakopitishwa wakiwa hawana cha kusema juu ya uharamia huo unaotokea kwenye kitovu cha mawasiliano cha nchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment