Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, August 14, 2013

Ponda azungumza

NA WAANDISHI WETU

14th August 2013


  Asema alipigwa risasi
Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa amelazwa wodini MOI.
Wakati shinikizo zikizidi kuelekezwa kwa Jeshi la Polisi ili liseme ukweli wa kilichomjeruhi Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, majeruhi huyo ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) amezungumza kwa mara ya kwanza tangu afikwe na mkasa huo Jumapili iliyopita mjini Morogoro. 

Akizungumza na waandishi wa habari kwa kifupi sana akiwa wodini alikolazwa jana

jioni kutokana na polisi kuzuia waandishi kumhoji, Ponda alisema kilichomjeruhi ni risasi.

Ponda alisema kutokana na ongezeko la matukio ya kupigwa, kujeruhiwa na hata kuuawa kwa raia wakiwa mikononi mwa polisi jumuiya za kimataifa sasa zinapaswa kuishinikiza na kuihoji serikali kama kweli inafuata utawala wa sheria.

Ponda alisema kuwa matukio hayo yamekuwa ni mengi hali inayoonyesha kuwa serikali haifuati sheria.
“Kuna haja ya jumuiya za kimataifa kuiangalia Tanzania kwa jicho tofauti kwani kwa sasa siyo tena kisiwa cha amani kama inavyoonekana huko nje,” alisema Ponda huku akiwa amejilaza kitandani.

Ponda alisema: “Nimepigwa risasi na polisi bila ya sababu wakati mkutano ule ulifuata taratibu zote zilizotakiwa ikiwa ni pamoja na kupata vibali vyote.”

Alipoulizwa sababu za polisi kufikia hatua ya kumpiga risasi, alisema anafikiri kuwa siku zote amekuwa akipingana na serikali kuhusu mambo mbalimbali ambayo ameyaona hayako sawa, wakati wao wanaona njia ya kumnyamazisha ni kumuua.

Nje ya wodi alikolazwa Ponda kulikuwa na askari wanne, kati yao wawili walikuwa wamevaa sare za Jeshi la Polisi wakiwa na bunduki aina ya SMG na wawili wakiwa katika mavazi ya kiraia.

Baada ya waandishi kuruhusiwa kuingia wodini kumwona Ponda, askari mmoja aliyekuwa amevaa kiraia aliingia na kuwataka waandishi kumsalimia tu bila kupiga picha wala kumhoji chochote.

Hata hivyo, baada ya ushauri wa mmoja wa masheikh waliokuwa wodini hapo kumjulia hali Ponda, askari huyo alikubali waandishi kuzungumza na Ponda kwa dakika mbili tu lakini akazuia kupiga picha.

Huku Ponda akifunguka kwa mara ya kwanza, shinikizo mbalimbali zimeelekezwa kwa Jeshi la Polisi miongoni mwake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kime lishutumu kuhusika moja kwa moja kumpiga risasi kiongozi huyo Agosti 11, mwaka huu mkoani Morogoro.

Chama hicho pia kimesema hakina imani na timu iliyoundwa na Jeshi la Polisi inayoongozwa na  Kamishna wa Polisi, Isaya Mungulu kuchunguza tukio hilo.

Hayo yalisema jana jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Abdalah Safari, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo.

Alisema Mungulu alitumwa maeneo mbalimbali likiwamo la tukio la mlipuko wa bomu Arusha kufanya uchunguzi ambalo hadi sasa hakuna taarifa yoyote, wala watuhumiwa hawajakamatwa wala kufikishwa mbele ya sheria.

Alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alinukuliwa na vyombo vya habari vya nje na kulitaja gazeti la The Mirror la Uingereza akithibitisha kuwa Jeshi hilo linahusika kumpiga risasi Ponda katika harakati za kutaka kumkamata.

Profesa Safari alisema Chadema wanashangazwa na Jeshi la Polisi kujikanganya kwa kujaribu kuficha ukweli wa tuhuma hizo wakati ukweli juu ya tukio hilo unajulikana.

Alisema katika hatua ya sasa Chadema kinaendelea kusimamia kwa dhati msimamo kuwa vitendo vya jeshi la Polisi kutumika na serikali kushambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua watu kuwa ni mwendelezo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuamua kutumia nguvu na kutegemea dola kutawala nchi.

Aliongeza kuwa ukweli wa hali hiyo ni pale Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipotoa kauli ya kuchochea uvunjifu wa amani kwa kuagiza Polisi wapige raia wasiokuwa na hatia.

“Mambo yote yanayoendelea ndani ya nchi kwa sasa Jeshi la Polisi limekuwa katika tuhuma ni mwendelezo wa maagizo ya kauli ya Waziri Mkuu,” alisema Profesa Safari.

Aidha Chadema wamelaani tabia ya kupandishwa vyeo kwa askari  Polisi kila wanapofanya matukio ya kinyama ikiwamo mauaji ya raia.

Profesa Safari alitolea mfano kwa aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Michael Kamuhanda, kuwa Naibu Kamishna wa Polisi baada ya tukio la kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Chanel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.

Mwingine ni aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Thobias Andengenye na kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polisi.

“Polisi walifanya na kusimamia mauaji huko Zanzibar mwaka 2001, walihusika na kusimamia mauaji ya watu waliozikwa hai kwenye machimbo ya Bulyanhulu akiwamo Robert Manumba ambaye leo ni DCI, Polisi walishiriki kuua Imrani Kombe, bila maelezo yoyote kinyume cha sheria,” alidai Profesa Safari.

Kadhalika Chadema kilitoa wito kwa Rais Kikwete kuunda tume huru ya kimahakama/kijaji kwa ajili ya kuchunguza vifo, mauaji na mateso yanayofanywa na vyombo vya dola kwa raia wasiokuwa na hatia.

“Matukio kama ya kuuawa kwa Mwangosi, mauaji ya watu watatu Januari 5, 2011 Arusha, Mwembechai, Bulyanhulu, Usa River, Arumeru, Morogoro, Ndago Singida, Igunga, Tabora, kutekwa kwa Absalom Kibanda na Dk. Stephen Ulimboka,” alisema Profesa Safari.

CUF YAMSHUKIA KOVA

Naye Naibu Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya, amesema kuwa wanapinga kauli aliyoitoa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kwamba Ponda yuko chini ya ulinzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Kambaya alisema ni dhahiri kwamba Kova amepandisha hasira za waumini wa dini ya Kiislamu.

Alisema kiongozi mwenye busara hawezi kutoa kauli kama ile kwa umma kwani anachochea vurugu.

“Taarifa ya Kova kwamba Ponda amekamatwa huku akijua ana majeraha na anavuruga amani ya nchi. Kwanza anavyosema kuhusu tukio la Morogoro kwamba amekiuka kifungo cha nje haina mashiko kwa sababu haliko kwenye ngazi yake,” alisema Kambaya.

Alisema Jeshi la Polisi mkoani Morogoro lilishaunda timu kwa ajili ya kuchunguza tukio la Ponda, hivyo haikustahili Kova kutoa kauli ya kukurupuka.

“Kauli ya Kova inatengeneza mazingira magumu kwa ajili ya nchi yetu, inashangaza hata timu iliyoundwa haijatoa maelekezo yeye ameshaanza kutoa tamko,” alisema na kuongeza:
“Kova hakupaswa kutoa tamko kwenye situation (hali) kama hii.”

Alisema ni jambo linaloshangaza kwa kitendo cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kudai kuwa jeraha alilopata Ponda hawajui limesababishwa na kitu gani.

“Kama Hospitali ya Taifa inashindwa kutambua jeraha limesababishwa na nini, wakati inaonyesha wazi kwamba risasi imetoka kwa nyuma,” alisema Kambaya.

MORO WAUMINI WAMGOMEA IGP

Waumini wa Kiislamu mkoani Morogoro wanaodaiwa kushuhudia tukio hilo wamekataa kutoa ushahidi katika timu iliyoundwa kuchunguza tukio hilo.

Hatua hiyo inatokana na timu hiyo chini ya  Mungulu  kuwasili mjini Morogoro katika makao makuu ya Jeshi la Polisi na kutaka viongozi na waumini waliokuwapo katika tukio hilo kuwasilisha ushahidi wao.

Kamati hiyo ilikuwa katika chumba maalum kwa ajili ya kusikiliza viongozi na waumini hao ambao walijitokeza kuanzia saa 5:30 asubuhi kwa maandamano.

Waumini hao wanaokadiriwa kufikia 200 waliongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kislamu Mkoa wa Morogoro, Sheikh Ayubu Mwinge Salumu.

Wakati viongozi hao wakiwa ndani kusikiliza viongozi wa timu hiyo kwa takribani saa mbili na ilipofika saa 7:00 mchana, wafuasi wao waliokuwa nje waliamua kufanya sala karibu na majengo ya Jeshi hilo huku wakisubiri viongozi wao kuwapa taarifa kuhusu utoaji wa ushahidi wa tukio  hilo.

Ilipofika saa 7:45, Sheikh Salumu akifuatana na viongozi wengine walitoka nje ya ofisi hiyo na kuwaamuru waumini hao kuondoka haraka katika eneo hilo na kuelekea katika msikiti mkuu wa Morogoro kwa ajili ya kutoa taarifa rasmi.

Sheikh Salumu alisema wameamua kukataa kutoa ushahidi kwa timu hiyo kwa kuwa hawana imani nayo kwa kuwa siyo huru kama walivyotarajia.

Alisema kuwa wao ndio waliomba kuundwa kwa timu hiyo na kutaka iwe huru, lakini wameshangazwa timu hiyo kuundwa na Jeshi hilo la Polisi ambalo ndilo linatuhumiwa katika kadhia hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema wana ushahidi wa kutosha kuhusiana na tukio hilo lilotokea Agosti 10, mwaka huu baada ya Sheikh Ponda kumaliza kuhutubia kongamano la wahadhiri wa Kiislam lilofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, lakini kwa jinsi timu hiyo jinsi ilivyoundwa hawako tayari kuutoa.

Alisema kuwa timu hiyo imekubali maombi yao na kuyapeleka makao makuu ya jeshi hilo.

Alisema kuwa hivi sasa wanawasiliana na uongozi wa taifa wa Jumuiya na Taasisi za Kislamu Taifa ili kujua ni viongozi gani wataongezewa katika kutoa ushahidi katika timu itakayokuwa huru kuchunguza tukio hilo.

Mungulu alipotafutwa na waandishi wa habari kuzungumzia hatua hiyo, baadhi ya wajumbe na wasaidizi wake waliwazuia kwa maelezo kuwa hawezi kuzungumza na waandishi.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Faustini Shilogile, alisema hawezi kuzungumzia chochote kwa kuwa kuna timu imeundwa kwa ajili ya kuchunguza na kwamba yeye ameicha ili itafute ukweli wa jambo hilo.

 MOROGORO POLISI LAWAMANI
Naye Naibu Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam mkoa wa Morogoro, Sheikh Chaulembo Ally, alisema kuwa polisi ndio wamekuwa chanzo cha matukio ya Waislam kufanyiwa vurugu katika makongamano yao.

FAMILIA YAKATAA POLISI
Awali Msemaji wa familia ya Sheikh Ponda, Isihaka Rashid, aliwaambia waandishi wa habari hospitalini hapo kuwa wanataka tume huru kuchunguza tukio la kujeruhiwa kwa ndugu yao na hawana imani na timu iliyoundwa na polisi kwa kuwa wao ni watuhumiwa namba moja.

Isihaka alitoka kauli hiyo huku polisi wakiendelea kuweka ulinzi Moi alikolazwa Sheikh Ponda. Isihaka alimnukuu Ponda akisema kuwa alijua haya yaliyomfika yangetokea kwa kuwa amekuwa akipigania maslahi ya Waislamu nchini.

Alisema kama serikali inataka kutatua tatizo ni vyema wakae chini wakazungumza juu ya malalamiko ya Waislamu ambayo wanaamini hayako sawa.

Imeandikwa na Jimmy Mfuru, Gwamaka Alipipi, Samsom Fridolini, Dar na Ashton Balaigwa, Morogoro.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment