Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, August 23, 2013

Rwanda, Uganda wametukumbusha wajibu

NA MHARIRI

23rd August 2013


Katuni
Tanzania imetahadharishwa kwamba huenda uchumi wake ukayumba kutokana na maamuzi ambayo yanadaiwa kufanywa na serikali za Rwanda na Uganda kwamba kuanzia Septemba mosi mwaka huu, hazitatumia Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao kutokana na urasimu mwingi unaosababisha mizigo kuchelewa kutoka.

Taarifa hiyo ambayo iliwekwa hadharani juzi na Msemaji wa Chama cha Wasafirishaji wa Mizigo nchini (Tatoa), Elias Lukumay, wakati akizungumza na Kamati ya Bunge ya Bajeti, jana ilipewa uzito mkubwa katika vyombo vya habari nchini kutokana na unyeti wake.

Kulingana na taarifa hiyo nchi hizo  zimekubaliana kutumia Bandari ya Mombasa kusafirisha mizigo yao kutokana na bandari hiyo kuwa na mfumo wa kulipia makontena mara moja na mizigo kufika sehemu husika kwa wakati mwafaka.

Kutokana na unyeti wa bandari katika uchumi wa taifa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge, alisema kamati yake imeamua kulipeleka suala hilo katika vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza wiki ijayo ili lijadiliwe juu ya urasimu unaofanya Bandari ya Dar es Salaam ikimbiwe na wateja.

Ingawa hadi sasa ni vigumu kusema kwa yakini kwamba taarifa hizo ni sahihi kwa asilimia 100 kwa kuwa bado hakuna msemaji yeyote wa serikali hizo mbili kwa maana ya Uganda na Rwanda aliyejitokeza hadharani kueleza hayo, habari hizi ni za kushtua na zinahitaji ufuatiliaji wa haraka sana ili kuepusha taifa hili na madhara ya kukimbiwa na wateja wa nchi hizo mbili jirani na wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wakati kamati ya Bunge ya Bajeti ikijipanga kupeleka suala hilo bungeni, tunafikiri kuna sababu za msingi kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wizara ya Uchukuzi kukaa kitako na kutafakari hatua za haraka za kuchukua juu ya kusudio hilo. 

Katika hali hii sisi tunasema kwamba inawezekana kabisa ufanisi duni katika bandari ya Dar es Salaam ni moja ya mambo yanayoweza kukimbiza wateja; wawe ni serikali au hata mfanyabiashara mmoja mmoja.

 Ni vyema tukakumbushana hapa kuwa bandari ni sawa na mgodi mkubwa wa madini, unatazamwa kama chanzo kikubwa cha mapato ya kuendesha serikali na shughuli zake. Ni kwa kutambua ukweli huo, mataifa mengine duniani yanaweza kujiendesha tu kwa kutumia bandari. Hawana rasilimali nyingine ya maana na mambo yanakwenda vizuri tu.

Kwa maana hiyo, uamuzi wa Rwanda na Uganda kama kweli upo, basi uchukuliwe kama changamoto na fursa ya kujitazama kwa kujitafakari nini cha kufanya ili kwanza kuboresha huduma katika bandari hii. Maamuzi kama hayo siyo tu yatavutia wateja wengi zaidi bali pia yataongeza mapato yake na kusaidia kukwamua uchumi wa taifa hili.

Ufanisi bandarini ukiongezeka ndivyo utaiweka Tanzania kwenye nafasi nzuri katika ushindani wa huduma katika sekta ya usafishaji wa majini na hata nchi kavu.

Ni kwa msingi huu tunasema kuwa kwa vyovyote vile hadhari ya Tatoa siyo ya kupuuza hata kidogo.

Watanzania wanajua kuwa kumekuwa na juhudi nyingi za kurekebisha mifumo na watendaji wa TPA kwa kitambo sasa. Mwaka jana na mwaka huu ulipita mtikisiko mkubwa sana katika mamlaka hiyo kwa kuwandoa wakurugenzi kadhaa. Mabadiliko hayo yalitarajiwa kuleta ufanisi zaidi na kuziweka bandari za taifa hili kwenye nafasi nzuri zaidi ya ushindani wa huduma za usafirishaji.

Mara kadhaa Wizara ya Uchukuzi yenye dhamana na bandari imekuwa ikieleza mikakati ya kurekebisha bandari nchini, ikianzia na ya Dar es Salaam ambayo ni kubwa kuliko zote, Tanga na Mtwara. Ni vigumu kwa sasa kusema kwa uhakika ni kwa kiwango gani mipango ya mageuzi katika uendeshaji wa bandari hizi imefanikiwa kwa kuwa mingine inahitaji muda hasa ujenzi na upanuzi wa miundombinu.

Inawezekana kabisa kwamba wenzetu nchi jirani wamejizatiti muda mrefu zaidi kuboresha huduma zao hivyo kuwapa Rwanda na Uganda jeuri ya kuipiga teke Dar es Salaam na kukimbilia Mombasa. Hili linawezekana kabisa.

Hata hivyo, pamoja na kasoro nyingi na udhaifu wowote unaoweza kuorodheshwa kuhusu huduma ya bandari ya Dar es Salaam na hali ya ubora wa barabara zetu na reli kutoka bandarini hadi Rwanda na Uganda, pia suala la ‘kushikishana adabu’ lisipuuzwe.

Ni kweli tuna matatizo, ni kweli kuna urasimu wa uendeshaji mambo nchini, ni kweli tuna vizuizi vingi barabarani tangu mzigo unapotoka bandarini hadi unavuka mpaka kwenda Rwanda au Uganda, lakini pia ni kweli hali ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na majirani zake hasa Rwanda siyo mazuri sana. Inawezekana tumeanza kuviziana.

Tunasema haya yote yanawezekana na ni wajibu wa serikali kutafakari hali hii ili kujipanga vizuri kukabiliana na changamoto hizi mpya zinazoibuliwa na majirani zetu.

Kitu kimoja ambacho hata hivyo ni lazima kukizingatia ni kwamba sisi ni taifa huru, tuna haki ya kuamua jinsi ya kuendesha mambo yetu bila kushurutishwa kwa mbinu  zinazojengwa kwenye picha ya vikwazo vya kiuchumi.

Tujipange tujenge taifa letu liwe imara kiuchumi; tuwe na umoja wa kweli wa kitaifa, tujielekeze kufanya kazi kwa bidii zaidi, kwa kuwa matendo hutoa ujumbe mzito zaidi ya maneno.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment