NA MHARIRI
9th August 2013
Tunachukua fursa hii kuwapongeza Waislamu wote kwa kumaliza salama mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na leo kusherehekea sikuu ya Iddi el Fitri.
Kwa hapa nchini sherehe za Iddi mwaka huu kitaifa zitafanyika mkoani Tabora ambako Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, atakuwa mgeni rasmi.
Maadhimisho ya sherehe hizo kitaifa yatafanyika katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani humo na pia katika mikoa mingine yote nchini.
Wakati mwezi mtukufu wa Ramadhani ukiwa umefikia tamati, tunapenda kuwasihi Waislamu kuyaendeleza mema yote ya mwezi huo na kujiepusha na uovu na mambo mengine yanayomchukiza Mwenyezi Mungu.
Wakati wa Mwezi wa Ramadhani, tulishuhudia Waislamu katika umoja wao wakihimizana kutenda mambo mema, kusaidia jamii hasa yatima, wajane, watu wasio na uwezo, wagonjwa,
kuwa na uvumilivu, subira, kuhimizana mema na kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu katika swala na kwa kufuata mafundisho yake.
Katika kipindi hicho, viongozi wa dini wamehimiza upendo, umoja, mshikamano, kuepuka chuki na mambo mengine mabaya na kuufanya mwezi huo kuwa wenye amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Waislamu na wasio Waislamu.
Ni matumaini yetu kuwa Mwezi wa Ramadhani hautaondoka na mema yake, bali Waislamu na wasio Waislamu watayaendeleza mema yote waliyokuwa wakiyazingatia katika mwezi huo.
Pia ni matumaini yetu kuwa Waislamu watashirikiana na wenzao wasio Waislamu kusherehekea sikukuu ya Iddi kwa amani na utulivu.
Tunawasihi wananchi kujiepusha na mambo yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama wao au wa watu wengine wakati wa kusherehekea sikukuu hii.
Hatutarajii kuona watu wakisherehekea sikukuu hii kwa kujiingiza katika ulevi na mambo mengine maovu yanayoweza kuharibu maana nzima ya sikukuu hii ya kidini.
Aidha, tunatoa tahadhari kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao wakati wa sikukuu hizi ili kuwalinda dhidi ya mambo yoyote mabaya yanayoweza kuwatokea.
Tunasema hivi kutokana na uzoefu kuonyesha kuwa, wakati wa sikukuu za kidini baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwaachia watoto kwenda kutembea katika maeneo mengine ikiwamo katika kundi za starehe na fukwe za bahari bila ya uangalizi ambako mara nyingine hukumbana na masahibu mbalimbali na hata wakati mwingine kupoteza maisha.
Madereva nao tunawaasa kuendesha magari yao kwa tahadhari na kuepeuka kuendesha huku wakiwa wamelewa ili kuepusha ajali zinazoweza kujeruhi au hata kupoteza maisha ya watu watakaokuwa barabarani wakisafiri au katika matukio mbalimbali ya kusherehekea sikukuu.
Pia tunatoa wito kwa Polisi kuimairisha ulinzi kwenye nyumba za ibada ili waumini waswali swala ya Iddi kwa amani na kurejea majumbani.
Tunawatakia Waislamu na Watanzania wote Iddi Mubaraka.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment