Marekebisho ya Sheria ya Katiba Mpya Maoni ya
Baraza la Katiba,
Zanzibar (BAKAZA),
Baraza la Katiba, Zanzibar (BAKAZA) Press Release
Marekebisho ya Sheria ya Katiba Mpya Maoni ya Baraza la Katiba,
Zanzibar (BAKAZA),
28 Septemba, 2013
Baraza la Katiba, Zanzibar (BAKAZA), ambalo ni jumuisho la asasi
saba za kiraia*limesikitishwa sana na matukio katika Bunge la Tanzania siku ya
Alhamis tarehe 5 Septemba2013, ambayo siyo tu yamevunja heshima ya chombo hiki
cha uwakilishi wa Watanzania,bali yametishia kuvuruga kabisa mchakato mzima wa
kuandaa Katiba Mpya inayotarajiwa naWazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Bunge la nchi ni kama kioo cha nchi yenyewe, na sura ilioonekana siku
ya tarehe 5Septemba 2013 katika kikao cha Bunge kilichotaka kuupitisha Mswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2013 kwa
mabavu ya uwingi waWabunge wa upande mmoja, na amri ya Naibu Spika kuamrisha
Mkuu wa Kambi yaUpinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe, kutolewa Bungeni kwa
nguvu, ni aibu si kwaBunge tu bali kwa Watanzania wote.
1. Ushirikishwaji wa Wazanzibari
Kazi kubwa lililopewa Bunge la
Tanzania wakati huu ni kusimamia mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya
kidemokrasia ambayo, kwa mara ya kwanza, ilitakiwa kuwashirikishawananchi wote,
wa Zanzibar na wa Tanganyika.
Katika kazi hii, Bunge limeonekana limeshindwa kabisa kumudu kazi
yake kwa njia ya uwazi na ya kidemokrasia.
Ulipopelekwa Bungeni mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mara
ya kwanza Machi,2011, Bunge liliamuwa kuipeleka rasimu hiyo kwa wananchi. Kama
tunavyokumbuka, Mhe.Samuel Sitta alipelekwa Zanzibar kwa makusudi ya kuiuza
rasimu hiyo, lakini ilioibuka nisio tu wananchi hawakushirikishwa katika
uundwaji wa rasimu hiyo, bali hata SMZilihadaiwa.
Tuligundua kwamba rasimu ya sheria ilipelekewa kwa SMZ, na kwa nia
safi,SMZ iliijadili na kutoa mapendekezo kumi na nne. Kamati ya Bunge ya Katiba
sio tuikachukua mawili tu na ikatupa mengine katika debe la taka, bali
ikaendelea kuzidisha mambo mengine mengi bila kushauriana na SMZ.
Hii ilikuwa ni dharau kubwa kwaZanzibar na Serikali yake, na sote
tunakumbuka namna ambavyo Zanzibar iliupokea mswada huo ambapo wananchi
waliungana na Serikali yao kufika hadi Mswada ule kuchanwa hadharani.—————– *
Zanzibar Law Society (ZLS), Waandishi wa Habari za Maendeleo ya
Zanzibar (WAHAMAZA), ZanzibarYouth Forum (ZYF), Umoja wa Walemavu Zanzibar
(UWZ), Zanzibar Female Lawyers’ Association(ZAFELA), Tanzania Media Women
Association, Zanzibar (TAMWA), na Pemba Press Club (PPC) .
Inastaajabisha sana kwamba Bunge limesahau tukio hilo baada miaka
miwili tu na kurudia makosa yaleyale ya kupitisha sheria zinazohusu mambo ya
Muungano bila ya kuishirikishaZanzibar ambayo ni mshirika mwenza katika
Muungano.
Tumeambiwa hadharani na Mhe.Abubakar Khamis, Waziri wa Sheria na
Katiba wa Zanzibar, kwamba safari hii SMZilipelekewa Mswada unaorekebisha
vifungu vinne tu, na wakaipitia na kurekibisha ipasavyo.Makamo wa Pili wa Rais,
Mhe. Seif Ali Idi akapokea ripoti iliyotumwa kwake na MheAbubakar akishirikiana
na Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na yeye Makamo wa Pili akaituma kwa Waziri
Mkuu wa Muungano, Mhe. Pinda.
Lakini, ulipopelekwa Bungeni,mswada ulikuwa na vifungu 11 ambavyo
vingi ya vifungu hivyo viliingizwa baada yaMakamo wa Pili kupeleka ripoti yake.
Kitendo hichi kimefanywa kwa makusudi kuwadanganya Wazanzibari na Serikali yao
na ni kitendo cha dharau ya mwisho kwamshirika mmoja wa Muungano kumfanyia
mshirika mwenziwe.
Vitendo kama hivi ndivyovilivyopelekea wananchi wa Zanzibar kuona
kwamba Muungano huu hauwatendei hakiWazanzibari bali pia unaidhalilisha SMZ kwa
kiwango cha kuitia aibu mbele yaWazanzibari.
Kwa kuwa uundwaji wa Katiba lazima ushirikishe wananchi wa pande
zote mbili, basi haikutosha Serikali ya Muungano kushirikiana na SMZ tu (hata
kama ushirikishwaji wenyewe ni wa kisanii), bali walipaswa kuwashirikisha
wananchi wa Zanzibar pia. .
Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba ilijua hivyo, na ilikutana na
asasi za kiraia za Tanganyika lakini Kamati hiyo haikuona haja ya kukutana na
hata asasi moja kutoka Zanzibar. Ingawa baadhi ya Wajumbe wa Kamati
walisisitiza kutaka kufika Zanzibar na fedha kwa ajili hiyo zilikuwepo, lakini
Kamati ya Bunge haikufika Zanzibar; hii ni jeuri na kibri wanayofanyiwa
Wazanzibari kama kwamba wao si sehemu muhimu ya Muungano wa Tanzania.
Ubaya wa kutoshirikishwaji katika majidiliano juu ya marekibisho
ya Sheria ya Katiba ni kwamba wananchi hawakuweza kutoa maoni yao juu ya
masuala muhimu ya kikatiba yaliobadilishwa kwa haraka haraka, na kwa kiasi
kikubwa, yanapunguza uhalali wa Katiba ijayo.
Hii ni kinyume na azma ya Rais Kikwete alipotangaza uanzishaji wa
mchakato mzimawa kuandika Katiba Mpya ya kwanza kwa ridhaa ya wananchi tarehe
mosi Januari, 2011.
2. Kupitisha Katiba Mpya
Mbali na ushirikishwaji wa Wazanzibari
katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, suala lapili muhimu sana katika mchakato
huu ni kupata ridhaa ya wananchi kwa uwingi (consensus)ili nchi isigawike
baadaye.
Katika dunia nzima, na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yenyewe
ilivyokiri katika kifungu cha 26, ili Katiba iweze kupitishwa katika Bunge
Maalum, itahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya idadi ya wajumbe kutoka
Tanganyika na idadi hiyo hiyo kutoka Zanzibar.
Kinyume chake, sheria sasa imerekebishwa kuonesha kwamba Katiba
nzima kwa ujumla itapigiwa kura mara ya kwanza kutazama kwamba inapata theluthi
mbili ya pande zote mbili;na kama haipati, basi Mwenyekiti wa Bunge Maalum
ataorodhesha mambo yanayokosa ridhaa ambayo yatapigiwa kura mara ya pili mbali
mbali; na kama itashindikana kupata theluthi mbili ya pande mbili basi, na hapa
ndio Bunge limeteleza kikatiba kukubali nusu ya Bunge tu (simple majority)
kupitisha mambo yalioshindwa kupata ridha ya theluthi mbili ya wajumbe kutoka
kila upande.
Sasa hii inawafanya wapuuzi (stupid) wale wote waliodhani kuweka
theluthi mbili ni kulinda maslahi muhimu kwa Washirika wa Muungano.Kama kifungu
hiki kilihitaji kurekebishwa, basi ilikuwa kueleza mchakato wa kupitisha huo
Katiba wa mpango wa busara na hekima, kuipitia ibara kwa ibara ili kila ibara
iweimejadiliwa na imepata theluthi mbili pande zote mbili, na mwisho wake
kupitisha Katiba nzima kwa uwingi hitajika, lakini sio kubadilisha msingi
muhimu wa kikatiba wa theluthi mbili. Kama sehemu moja ya Wabunge iliokosa
kupata theluthi mbili itakuwa mkaidi, basi hawatakuwa na haja ya kupata
maridhiano (compromise) wakijuwa kwamba mwisho wake wataweza kuipitisha kwa
aslimia khamsini tu. Na pengine wataweza kupitisha sio ibara tu bali Katiba
nzima kwa aslimia 50% tu. Hii haitakuwa Katiba ya maridhiano bali mtego tu
utakaozaa mauaji mwisho wake.
3. Muundo wa Bunge la Katiba
Suala la tatu ni muundo wa Bunge Maalum la Katiba. .
Kifungu cha 22 kinaeleza kwamba Bunge litakuwa na
:a) Wabunge wote wa Bunge la Muungano, waliochaguliwa mwaka 2010
kabla ya kuletwa suala la Katiba Mpya, na tuonavyo sisi hawa wote hawana
uhalali(legitimacy) ya kuwawakilisha Watanzania juu ya suala hili;
b) Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar waliochaguliwa
mwaka 2010 ambao nao vile vile hawana uhalali;
c) Wajumbe 166 wataoteuliwa na Rais kwa makubaliano na Rais wa
Zanzibar.
Hali halisi ilioko sasa ni asilimia 72 ya Wabunge na Wawakilishi
wanatoka chama kimoja ambacho kimeshatangaza msimamo wake juu ya suala la
Katiba. Tayari kimemfukuza Mwakilishi mmoja ambae alikuwa na msimamo tofauti,
na inaweza kutumia kanuni ya‘three-line-whip’ kuwalazimisha Wabunge hawa
kufuata msimamo wa Chama hicho tawala,na kutishia kuwafukuza kwenye chama chao
wale wataokataa kutii amri ya chama.
Katika hali hii ilikuwa haina haja kuandaa Katiba Mpya na kupoteza
mabilioni ya shilingi ya wavuja jasho kama chama kimoja tu kitaweza kuamua
mustakbali wa Katiba yetu, na ilikuwa hamna haja kabisa kupoteza muda wa
Watanzania eti kwa lengo la kupata Katiba ya “wananchi wenyewe”.
Jambo la pili liliojitokeza sasa ni kwamba wale Wajumbe 166
watateuliwa na marais wawili ambao hao vile vile wanatoka kwenye chama kile
kile kimoja. Baada ya Serikali ya Muungano kuukataa usawa katika Bunge la
Katiba kati ya Zanzibar na Tanganyika, idadi hii ya 166 ikabuniwa kuipa
Zanzibar angalau theluthi moja tu ya hawa 166 katika bunge lile,ikidaiwa kwamba
Zanzibar bado itaweza kuzuia chochote katika Katiba kwa sababu kutakuwa na
kanuni ya theluthi mbili katika kupitisha Katiba.
Sasa tumeshaona kwamba theluthi mbili sasa imeyayuka, na Zanzibar
haina kinga tena, kwa sababu, pamoja na theluthimoja ya hawa 166 wataoteuliwa
na Rais wa Zanzibar, jumla ya Wazanzizbari wote katika
Bunge la Katiba watakuwa asilimia 36 tu, na chochote watachotaka kupitisha Watanganyika
Bunge la Katiba watakuwa asilimia 36 tu, na chochote watachotaka kupitisha Watanganyika
basi wataweza kukipitisha bila khofu. Hapo tutaanza “Kero za
Shirikisho.”
Lakini bado liko suala la vipi hawa 166 watateuliwa na marais
wawili. Marekibisho ya Sheria iliopitishwa na Bunge hivi karibuni inaeleza kwamba makundi
yaliyotajwa katika kifungu cha 22 (NGOs, asasi za kidini, vyama vya siasa, taasisi za elimu
ya juu, makundi ya walemavu, jumuiya za wafanyakazi, wakulima, na ya wafugaji, n.k.),
yataalikwa kupendekeza majina tisa ambamo marais watateua watatu kutoka kila
kikundi. Katika hali halisi tulionayo, bila kuwatilia shaka wataoteua hawa wajumbe,
itakuwa vigumu kuwahakikishia wananchi na vyama vya siasa vya upinzini na
kuridhika, kwamba maslahi na matakwa ya ubinafsi hayatotumika. BAKAZA lilipendekeza kwamba
makundi haya ndio wanayojuwa nani wanaweza kutetea maslahi yao katika Bunge la
Katiba, na ni bora kuwaachia wawachague wawakilishi wao wenyewe, kama ni watatu, basi
wawe watatu, na haina haja marais kuwachagulia.
Kwa vyovyote vile, hata hawa wajumbe 166, ambao theluthi moja tu
ndio watatoka Zanzibar,na wakijumuishwa na Wabunge wa Muungano na Wawakikilishi kutoka
Zanzibar,hawatobadilisha ukweli kwamba Bunge Maalum la Katiba bado
litahodhiwa na chama kimoja kwa zaidi ya theluthi mbili. Kwa bahati mbaya, namna Bunge
lilivyotenda kazi yake na kupitisha mswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba bila kuijadili kwa undani, inaondowa matumaini kabisa kwamba Wabunge hawa wataweza
kusimamia upatikanaji wa Katiba Mpya ambayo itakuwa ya kidemokrasia na ya
uadilifu. Ndio maana BAKAZA ilipendekeza kwamba Wabunge wa Bunge Maalum wangechaguliwa
kwa kazi maalum ya kuandika Katiba tu ili kupata ridhaa (mandate) ya
wananchi juu ya aina ya Katiba wanayotaka wakati huu, na kuepuka matatizo tunayopata sasa. Na kwa
sababu Katiba tarajiwa ni ya Muungano wa nchi mbili zilizoungana 1964, basi
ingetakiwa kuwa na Wabunge sawa ili Mshirika mmoja asione anaonewa kwa udogo wake wa
ardhi, uchumi au idadi ya watu wake.
4. Kuuliwa kwa Tume ya Katiba
Katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, kazi kubwa imefanywa na
Tume ya Marekibisho ya Katiba iliyoundwa mwaka 2011. Tume hii ni chombo peke yake
kilichoheshimu usawa kati ya washirika wawili waliounda Muungano 1964 kwa sababu kila
upande ulitowa wajumbe 15. Wajumbe wote hawa waliteuliwa na Marais wawili wa
Muungano na wa Zanzibar. Hesabu iliyofanywa na wadadisi wa habari ilionesha
kwamba kiasi thuluthi mbili kati yao walitoka au walikuwa karibu na chama tawala, na wengi sana
kati yao walikuwa waumini wa Muungano wa Serikali mbili hapo mwanzoni. Lakini, baada
kuwasikia wananchi kote nchini kutoka Zanzibar mpaka Kagera, Kilimanjaro mpaka
Songea, na kutathmini hali halisi na matakwa ya wanachi wakati huu, wengi wao wameshawishika
kwamba, kama tunataka Muungano uendelee, lazima mfumo wa Muungano urekebishwe.
Na ndio maana wamependekeza mfumo wa Shirikisho la serikali tatu. Kwa kazi hii
iliyokuwa si rahisi kwa waumini wa serikali mbili, wajumbe wa Tume wameonesha ukweli na
uadilifu mkubwa na kwa hiyo wanastahiki kupongezwa sana na wananchi. Mhe. Rais
Kikwete mwenyewe aliwapongeza kwa kazi nzuri waliofanya kujaribu kutatua “Kero za
Muungano.”Lakini, kitu kilichowashangaza wananchi sana ni kuona Tume hii
chini ya Mhe. Warioba,ambaye alikuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere, na aliwahi kuwa
Mwanasheria Mkuu na Jaji, na hata Waziri Mkuu chini ya Rais Nyerere na Ali Hassan
Mwinyi, sasa inalaumiwa eti kutaka kubomoa Muungano kwa kupendekeza mfumo mbadala wa Muungano.
Ushabiki wa kichama ulitawala sana katika Bunge lililopitisha Mswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwanzoni mwa mwezi wa Septemba, 2013.
Chini ya kifungu 20 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
iliyopitishwa mwaka 2011, baada kukamilisha Rasimu ya Pili na kuwasilisha kwa Rais, Tume hii
ilikuwa inategemewa kutoa ufafanuzi utakaohitajika wakati wa majadiliano katika Bunge
Maalum, na pia kuwaelimisha wananchi juu ya suala la Katiba Mpya na Kura ya Maoni itakayopigwa
kukamilisha mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya. Baada ya kupata uamuzi wa
wananchi ndio Tume hii ilikuwa ivunjwe chini ya kifungu cha 37 cha Sheria hiyo.
Lakini, namna Rasimu ilivyowakera Wabunge kadhaa, na kutumia hoja
ya nguvu waliokuwa nayo katika Bunge la sasa, wameamua kuiuwa Tume mara tu baada ya
kuwasilisha Rasimu ya Pili! Hata hivyo, wamelazimika kukubali chini ya kifungu 20(4)
kwamba bado watahitaji msaada wa Mwenyekiti, Makamu wake au mjumbe wowote wa Tume
kulisaidia Bunge la Katiba baada ya kuvunjwa. Namna utashi wa kichama ilivyotawala
majadiliano katika
Kamati ya Sheria na Katiba na katika Bunge lenyewe, Wabunge hawa
wameugeuka uamuzi wao wenye kupitisha makisio ya Tume hiyo ya Shilingi bilioni 32
muda mfupi tu kabla ya Tume kuitoa Rasimu ya Kwanza.Kwa ujumla, Bunge la Muungano limeonesha wazi wazi kwamba
limeshindwa kuonesha busara katika maslahi ya nchi ya muda mrefu katika suala la Katiba
Mpya, na kwa kiasi hicho limejionesha kwamba haliwezi kutegemewa kujali maslahi mapana
zaidi ya ustawi wa nchi hii. Kama Bunge hili ndilo litakuwa sehemu kubwa ya Bunge Maalum
la Katiba, basi tamaa gani tunaweza kuwa nayo kupata Katiba Mpya ya kidemokrasia ya
karne ya 21?
5. Ombi kwa Mheshimiwa Rais Kikwete
Mheshimiwa Rais, Tarehe mosi Januari ya mwaka 2011, katika salamu
zako kwa wananchi wa Tanzania, ulitangaza azma yako ya kuipatia Tanzania Katiba Mpya
ili iweze kuiongoza nchi katika karne mpya. Kwa nia safi kabisa, ulionesha kwamba
ulikuwa unatarajia Katiba hiyo, kwa mara ya kwanza katika nchi yetu toka kupata uhuru, iwe
imewashirikisha wananchi wenyewe katika uundwaji wake. Kwa dhamira nzuri kwa nchi
yetu, sisi hatuna budi tukupongeze na tukushukuru kwa kuonesha njia vizuri.
Katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya, sasa hivi tuko kwenye
njia panda; ama tutekeleze azma yako ya kuwa na Katiba ya demokrasia iliyopatikana
kwa njia ya kidemokrasia na iliowashirikisha wananchi wote, au kutumika hoja
ya nguvu Bungeni, na kwa makusudi kuwapuuza wananchi wa sehemu moja ya Muungano huu. Ni
dhahiri kwamba “Kero za Muungano” ndizo zilikuwa sababu kubwa ya kuhitajika
Katiba Mpya. Kama tutapotea njia wakati huu, na kuendelea kuwapuuza wananchi wa
Zanzibar mara nyengine tena, si Serikali ya Mapinduzi tu, wala si asasi za kiraia tu,
bali wananchi kwa ujumla, basi tujitayarishe kufungua kitabu cha pili cha “Kero za Muungano.”
Zanzibar ilikuwa nchi huru kamili ilipoungana na Tanganyika mwaka
1964 katika Muungano wa Tanzania, na inastahiki kuheshimiwa si kwa maneno tu bali
kivitendo, pamoja na kikatiba. Kama Katiba Mpya itashindwa kukubali usawa wa Zanzibar
na Tanganyika katika Shirikisho la Tanzania, basi Shirikisho hilo halitakuwa halali na
halitadumu. Kwa miaka 50 ya Muungano, Zanzibar siku zote imekuwa ndugu mdogo mbele ya kaka
yake. Miaka 50 imetosha kabisa kwa ndugu mdogo huyu kuwa baba kamili anaehitaji
usawa na kaka yake mkubwa. Zanzibar inahitaji usawa sio katika mchakato wa kuunda
Katiba Mpya tu, lakini pia katika Katiba Mpya na Shirikisho jipya linalotarajiwa kuundwa.
Katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya, Tume ya Katiba chini ya
uwenyekiti wa Mhe.Joseph Warioba, wewe mwenyewe ulikiri kwamba Tume ilifanya kazi
nzuri ya kuwasikiliza wanannchi nchi nzima, na kupendekeza Rasimu ambayo inajaribu
kushughulikia mahitaji ya kizazi kipya cha karne mpya, na kuacha nyuma “kero za Muungano”
zisizokwisha. Tume hio ilipangiwa kazi ya kuibeba Katiba mpaka mwisho wake kupata ridhaa
ya wananchi katika kura ya maoni, au tuseme, kura ya uamuzi, kwa sababu wananchi ndio
wakutoa uamuzi wa mwisho. Kwa hivyo, tumeshangazwa sana kuona kwamba Bunge la
Tanzania limeamuwa kuiuwa Tume hii mara tu baada ya kumaliza Rasimu ya Pili, bila
kutoa sababu za maana au sababu zozote. Kwa kuwa na nia safi toka mwanzoni mwa mchakato huu, bado
hatujachelewa tunayo nafasi ya kujirekebisha kwa kujali hadhi, nafasi na haki sawa kwa kila
mshirika wa Muungano katika hatua zote zilizobakia kutengeneza Katiba Mpya yenye ridhaa
ya pande zote mbili.
Ulazimishaji wa matumizi ya nguvu katika hatua yoyote ni
kutoitendea haki demokrasia na ni kinyume na maumbile ya Tanzania, taifa ambalo linajisifia kuwa ni
la kidemokrasia. Inawezekana Bunge limeteleza katika mabishano na mivutano ya
kivyama, lakini uamuzi wao wa haraka utaondoa uhalali wa Katiba tarajiwa. Kitu
kinachohitajika sasa ni busara kuliokoa jahazi lilioanza kwenda mrama. Tunakuomba Rais Kikwete
kuirejesha Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Bungeni
kwa kufikiria zaidi, na kuipa nafasi SMZ na asasi za kiraia za Zanzibar ili kupata ridhaa
ya pande zote mbili za Muungano. Tunakumbushwa wosia aliopewa Mwinyi Mkuu wa Unguja
iliochongwa kwenye ngoma yake iliopo Beit al-Ajaib, inayosema:
“Matendo yako ni kioo cha uongozi Hivyo wakusanye watu wenye muelekeo tafauti Kwa sababu mtu wa busara huwajumuisha na kuwatosheleza watu wote.”
Kinyume chake, tunaogopa kufikiria madhara yanayoweza kuikabili
nchi iliyogawanyika mapande mawili makubwa.
Chanzo: Mzalendo
Chanzo: Mzalendo
No comments :
Post a Comment