DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Fax: 255-22-2113425
|
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
Kikwete: ICC inaharibu mahusiano yake na Afrika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amesema kuwa mwenendo wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC)
kuhusu Bara la Afrika na viongozi wake, unainyima Mahakama hiyo nafasi kubwa ya
kuungwa mkono na Bara la Afrika.
Rais Kikwete pia amelaani vikali mashambulizi yanayoongezeka dhidi
ya vikosi vya kimataifa vya kulinda amani katika nchi mbali mbali duniani
wakiwamo walinda amani wa Tanzania.
Rais Kikwete alitoa
msimamo huo wa Tanzania mwishoni mwa wiki wakati alipohutubia Kikao cha Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mwaka huu, kwenye Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa mjini New York, Marekani.
Katika hotuba yake fupi na iliyowavutia wasikilizaji, Rais Kikwete
alisema kuwa ni dhahiri kuanzishwa kwa ICC kutokana na Mkataba wa Rome kulikuwa
ni hatua muhimu sana katika mfumo wa kimataifa wa kupambana na makosa ya jinai.
“Kwa hakika kuundwa kwa Mahakama hiyo kuliweka mfumo mzuri wa kuondokana na watu kutenda vitendo vya jinai na kuweza kuepukana na kuwajibika kwa vitendo hivyo na Mahakama hiyo ilianzishwa kwa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Afrika.
“Kwa hakika kuundwa kwa Mahakama hiyo kuliweka mfumo mzuri wa kuondokana na watu kutenda vitendo vya jinai na kuweza kuepukana na kuwajibika kwa vitendo hivyo na Mahakama hiyo ilianzishwa kwa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Afrika.
“Hata hivyo,
muongo mmoja tu baada ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo, ni dhahiri kuwa mvutano
umezuka kati ya ICC na Bara la Afrika. Sasa Mahakama hiyo inaonekana kama
taasisi isiyojali maoni na msimamo wa Afrika, kwa mambo ambayo kwa maoni yangu,
ni hofu halali ya Waafrika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Bado Mahakama hiyo inaendelea kupuuza
maombi ya mara kwa mara ya Umoja wa Afrika. Ni jambo la kutia huzuni kuwa
maombi ya kubadilisha muda wa kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya na Naibu Rais William Ruto yalipuuzwa na hata hayakujibiwa
kabisa.”
Ameongeza Rais: “Tabia
hii imekuwa ni hitilafu kubwa ambayo inaleta kikwazo kwa ICC kushindwa kutimiza
wajibu wake wa kupambana na tabia ya watu wanaofanya makosa ya jinai
kutokuchukuliwa hatua. Kwa hakika, kugangamara kwa ICC hata katika masuala
yaliyo wazi, kumethibitika kuwa kunainyima Mahakama hiyo nafasi ya kuendelea
kuungwa mkono Barani Afrika.”
Rais Kikwete alisema pia kuwa Tanzania sasa imekuwa moja ya nchi ambazo
zinashiriki zaidi katika shughuli za kimataifa za kulinda amani chini ya Umoja
wa Mataifa. Tanzania ina zaidi ya walinda amani 2,500 katika Darfur, Sudan;
Lebanon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuwa ni nchi ya sita katika
Afrika na ya 12 duniani kwa kutoa walinzi wa amani duniani.
“Kwa hakika tunaridhishwa na mchango wetu
mdogo katika shughuli hii. Na tunajua kuwa wakati mwingine tunalipa gharama
kubwa na maisha ya vijana wetu kwenye shughuli hizi kama ilivyotokea majuzi
katika Darfur na DRC. Waliopoteza maisha yao ni mashujaa wa taifa letu ambao
maisha yao hayakupotea bure.”
Aliongeza Rais Kikwete: “Vifo
vya walinda amani wetu ni ukumbusho wa kutosha wa hatari zinazowakabili walinda
amani wote duniani. Ni jambo la kuudhi, kwamba vikundi vyenye silaha na
waharibifu wa amani duniani wanaongeza mashambulizi hayo dhidi ya watumishi wa
amani. Ni lazima tulaani mashambulizi haya kwa nguvu zetu zote kwa sababu
hakuna sababu yoyote ya kuhalalisha mashambulizi haya ya kinyama ambayo
ni kosa la kimataifa la jinai chini ya Sheria za Kimataifa.”
Alisisitiza: “Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo wajibu wake mkuu ni kulinda amani na
usalama wa kimataifa lazima liwe mstari wa mbele katika kulaani vitendo hivyo
vya kinyama na haraka tu vinapotokea.”
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi katika Marekani na Canada
ameondoka New York usiku wa leo, Jumamosi, Septemba 28, 2013, kurejea nyumbani
ambako atawasili Jumatatu mchana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Septemba, 2013
No comments :
Post a Comment