NA WAANDISHI WETU
7th September 2013
Huenda akahusishwa na makosa ya jinai
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema hayo jana wakati akizungumza bungeni, baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa hoja ya kuahirisha Bunge hadi Oktoba 29, mwaka huu.
“Hata kama kuna kinga na inapotokea mtu anampiga askari pale bungeni sidhani kama ile kinga inamkinga”, alisema Ndugai.
Kaimu kamanda wa Polisi Susan Kaganda amethibitisha kuwa Sugu amejisalimisha polisi lakini hakutoa ufafanuzi zaidi kwa maelezo kuwa yuko kikaoni na kuahidi kutoa taarifa baadaye. Lakini hadi tunakwenda mtamboni hakupatikana kwa simu.
Lakini habari za tetesi ni kwamba Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu wanadaiwa kumsindikiza huko polisi.
Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), hakuyataja makosa yanayoweza kumkabili Sugu, badala yake alisema yapo mazingira yanayoondoa kinga ya Mbunge, anapobainika kujihusisha na kosa la jinai kwenye maeneo ya Bunge.
Kwa mujibu wa Ndugai, kinga dhidi ya Mbunge inatakiwa katika mazingira yanayoendana na uhuru wa mawazo.
Alitoa mfano kuwa, hata Jaji wa Mahakama Kuu atakapoghafirika na kumpiga mtuhumiwa mahakamani, haiwezekani akashindwa kushitakiwa kwa jinai.
Hata hivyo, Ndugai, alisema suala hilo linashughulikiwa na vyombo vya Dola kabla ya kuchukua hatua zinazostahili.
UTATA WA KISHERIA
Wakati Ndugai akibashiri kushtakiwa kwa Sugu, vifungu vya tano na sita vya Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge ya mwaka 1988, vinakataza Mbunge kukamatwa, au kuhudhuria mahakamani wakati akiwa ndani ya eneo la Bunge au wakati Bunge limekutana bila kuwapo kibali cha Spika.
Kwamba Mbunge anapotuhumiwa kufanya kosa hawezi kuletewa haki ya kuitwa ama polisi au mahakamani akiwa bungeni.
Eneo la Bunge limetafsiriwa na kifungu cha pili cha sheria hiyo kuwa ukumbi unaotumiwa kwa vikao vya Bunge, pamoja na ofisi, vyumba, vibambaza, maeneo ya wageni, bustani na maeneo mengine yaliyowekwa kwa ajili ya shughuli za Bunge.
Juzi, wabunge wa upinzani walishambuliana na askari wa ulinzi na usalama wa Bunge, huku Sugu akiondolewa kutoka ndani ya ukumbini kwa nguvu, akiwa amebebwa ‘mzobe-mzobe’.
Sugu, anadaiwa kupigwa na askari hao, hali inayotafsiriwa kuwa kichocheo cha kumfanya apandwe jazba na kutishia kulipiza kisasi kwa askari kwa kumpiga aliyehusika ‘kumsulubu’.
Askari anayedaiwa kushambuliwa na Sugu, anatajwa kuwa ni Koplo Nikwisa Nkisu na kwamba katika tukio hilo, alijeruhiwa jicho.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment