BY MHARIRI
1st October 2013
.jpg)
Ni wiki ambayo serikali iliendelea kuitumia sheria ya Magazeti namba 3 ya mwaka 1976 ambayo inatoa madaraka yasiyohojiwa kwa serikali kufungia vyombo vya habari, kwa kile ambacho kimekuwa kinadaiwa kuwa ni kuendesha uchochezi.
Katika maamuzi hayo ambayo hata hivyo wadau wa aina mbalimbali wameyakosoa, serikali imelifungia kwa siku 14 gazeti la MWANANCHI wakati gazeti la Mtanzania limefungiwa kwa siku 90 yaani miezi mitatu. Adhabu hizo ziliaza Septemba 27, mwaka huu.
Katika taarifa ya serikali ya kufungia magazeti hayo ambayo huchapishwa kila siku, habari tatu na makala moja vimetajwa kuwa chanzo cha uamuzi huo mkali na unaoumiza siyo magazeti hayo na kampuni zao tu, bali tasnia nzima ya habari nchini, bila kusahau maisha ya wahariri, wanahabari, familia zao na wote wanaopata kipato kwa kujihusisha kwa njia moja ama nyingine na usambazaji na uuzwaji wa magazeti hayo.
Siyo nia yetu kuingia katika mjadala wa usahihi au makosa ya habari na makala husika, kwa maana habari kuhusu Waislamu kusali chini ya ulinzi mkali na mishahara mipya serikalini 2013 zilizotolewa katika matoleo tofauti ya MWANANCHI na habari ya Mapinduzi hayaepukiki urais wa damu na makala ya mapinduzi hayaepukiki ambavyo vilichapishwa kwenye matoleo tofauti ya Mtanzania, ila ni msimamo wetu wa siku zote kwamba mfumo wa serikali wa kuadhibu vyombo vya habari kwa kuwa mlalamikaji na hakimu, haukubaliki katika taifa linalioendeshwa kwa mfumo wa kidemokrasia tena ya vyama vingi.
Ieleweke kwamba siyo kazi yetu kutetea udhaifu wowote katika tasnia ya habari, kadhalika ieleweke kwamba sisi siyo mashabiki wala wafuasi wa kuandika habari za kuvunja kanuni, maadili na weledi wa taaluma ya uandishi wa habari, ila ni watetezi wakubwa wa kutaka utawala wa sheria unaozingatia haki ya kusikilizwa kufuatwa na kuheshimiwa kwa kila anayetaka kumuhukumu mwingine katika taifa hili.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba tangu mwaka 1992 Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipopendekeza kuwa kama taifa hili litaamua kufuata mfumo wa vyama vingi, kama ambavyo Tume hiyo ilipendekeza, basi sheria 40 zilianishwa kwamba ni lazima ama zifutwe au zirekebishwe ili ziendane na mfumo mpya wa vyama vingi. Miongoni mwa sheria hiyo ni hii ya Magazeti namba 3 ya mwaka 1976.
Kwa bahati mbaya sana, tunasisitiza kwa bahati mbaya, serikali imekataa kuona mantiki ya pendekezo la Tume ya Jaji Nyalali yapata miaka 20 na ushei sasa. Bado serikali imeendelea kukumbatia sheria hii ambayo kwa kweli inaathiri sana uhuru wa habari na haki ya msingi ya wananchi kupata habari, vyombo vya habari ni nyenzo ya wananchi kufikia habari ili kufanya maamuzi.
Wadau wa habari kwa zaidi ya miaka 10 sasa wamekuwa katika harakati nyingi za kutaka kutungwa kwa sheria mpya ya habari, ambayo pamoja na mambo mengine itaanisha haki ya kupata habari, wajibu wa vyombo vya habari lakini pia wajibu wa serikali katika kufanikishwa kwa kazi hii muhimu. Hakuna ubishi habari ni haki ya kila mwananchi na ni nyenzo mmojawapo ya kuwawezesha wananchi kuchukua maamuzi juu ya taifa lao na mustakabali mzima wa maisha yao.
Haki ni haki tu. Haki ikiwekewa vikwazo ni sawa kabisa na kuopora. Siyo vema serikali ikaonekana kuwa kinara wa kuminya haki za wananchi wake, hasa kwa kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja misingi halisi ya utawala bora na demokrasia. Haipendezi.
Tunajua wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wote kwa ujumla wao ni wanadamu kama binadamu mwingine yeyote; wanafanya makosa makubwa kwa madogo, wanateleza kama ambavyo ilivyo kwa watendaji wengine katika tasnia nyingine nchini; kwa maana hiyo ni rai yetu kwamba katika kuteleza huko kuwe kwa makusudi au kwa bahati mbaya ni vema na haki anayedhani kuwa amekosewa katika udhaifu huo akawasilisha malalamiko yake kwenye chombo huru ambacho kinasikiliza hoja husika na kuziamulia kwa haki.
Msingi huu ndiwo unajenga dhana nzima ya utawala bora, haki ya kusikilizwa na kwamba hakuna mwenye haki ya kusikiliza shauri lake mwenyewe na kuliamulia.
Sote tunaelewa hakuna mwandishi wa habari au mhariri yeyote anayekataa kushitakiwa, kusikilizwa na kukubali hukumu itakayotolewa na chombo huru kama vile mahakama. Ni wajibu wa juu kabisa kwa mwanahabari au mhariri na hata mchapishaji kutii na kukubaliana na maamuzi ya kimahakama.
Kwa kuonyesha ukomavu huo, vyombo vya habari vyote vya Tanzania vinakubaliana kabisa na misingi ya kuwako kwa usuluhishi wa mashauri ya kihabari kupitia Baraza la Habari Tanzania (MCT) kama chombo cha hiari chenye majukumu pamoja na mambo mengine kusikiliza na kuamua malalamiko dhidi ya vyombo vya habari.
Serikali inatambua kuwapo kwa Baraza hili kwa zaidi ya miaka 17 sasa tena likitekeleza wajibu wa kusikiliza mashauri na kuamua, kikubwa ni kwamba maamuzi yake yamepokewa na kuheshimiwa na wadau wote kwa zaidi ya asilimia 99.
Tunafikiri serikali itambue kwamba katika zama za sasa siyo sawa na kwa kweli hajijengei picha nzuri ndani na nje ya nchi kwa kuendelea kutumia sheria mbaya na kandamizi wakati ikitajwa kuwa miongoni mwa mataifa yaliyoridhia mikataba ya kujiendesha kwa uwazi.
SOURCE: NIPASHE
No comments :
Post a Comment