NINAIANGALIA nchi hii ya Tanzania na ninaona matatizo tu. Nikigeuka huku naona matatizo ya kisiasa. Nikigeuka kule naona matatizo ya kimaisha. Umasikini umeikaba roho Tanzania.
Nikimwangalia Rais wake, Jakaya Kikwete, naona kuwa hawezi kufurukuta. Hawezi kuchukua hatua atakazo. Amekuwa mateka wa chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho pengine kinavuta pumzi zake za mwisho.
Nikiiangalia tena Tanzania kwa mintarafu ya Afrika ya Mashariki, ninaliona taifa lililo dhaifu lenye kiongozi dhaifu asiyeweza kuwa kiongozi wa eneo linalogeuka kuwa sugu kwa matatizo chungu nzima, likiwa pamoja na lile la ugaidi wa kimataifa.
Lakini wakuu wa dunia hii, akiwemo Rais Barack Obama wa Marekani, wanatwambia vingine. Wanatwambia kwamba tuna Rais mzuri, wanatwambia kuwa uchumi wa Tanzania unastawi na Serikali yake inazifuata sera za Uwazi, Utawala bora na Uwajibikaji.
Wakiwa ofisini mwao katika Benki Kuu ya Dunia, kwa mfano, wataalamu wa Benki hiyo wanatwambia kwamba Tanzania ni moja ya nchi za Kiafrika zinazostahiki kupigiwa mfano kwa namna uchumi wake unavyokua.
Wanazinukuu takwimu lakini sote tunaijua tabia ya takwimu; ya kusema uongo zinapohitajiwa ziseme uongo.
Ijumaa iliyopita tu mtaalamu mmoja wa uchumi wa Benki Kuu ya Dunia alisema kwamba mwaka jana uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 6.9. Hata hivyo, aliona bora atutanabahishe kwamba tukiziangalia hesabu za kitaifa tutaona kwamba ni sekta tano tu zilizochangia takriban asilimia 60 ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania baina ya 2008 hadi 2012.
Sekta hizo ni mawasiliano, shughuli za banki na huduma za kifedha, biashara ya rejareja, ujenzi na uzalishaji wa bidhaa viwandani. Sekta zote hizo ni sekta za mijini zenye kuwanufaisha zaidi waishio mijini.
Wa vijijini je? Huko ndiko wanakoishi wanane kati ya kila masikini 10 wa Tanzania. Ndiyo maana Serikali haikuweza bado kuupunguza umasikini uliozagaa nchini.
Laiti tungeliweza kupanda juu ya mlima tukaunadi ukweli. Tungeliweza kueleza jinsi mafisadi wa nchi hii walivyojitajirisha na jinsi hali za walio masikini zinavyozidi kudidimia.
Au jinsi wanasiasa walivyozugwa na ufisadi wakapoteza dira ya kuwaongoza wapi walipeleke taifa hili.
Au jinsi matajiri walonufaika kwa ufisadi wanavyowalaumu masikini kwa kuwa masikini na kwa namna wanavyousarifu umasikini wao.
Niliwahi kumsikia tajiri mmoja akijinata kwa kusema: “Mimi nnaujua umasikini; na nnajua namna ya kuishi nikiwa masikini. Na ninaitumia mikakati hiyohiyo kuendelea kujitajirisha.”
Kwa nini ulimwengu hautambui kwamba si jambo la buraha wala furaha mtu kuusarifu umasikini wake? Ni kazi ya jasho. Na ni kazi inayohitaji msaada mkubwa wa Serikali.
Ifanye nini nchi hii hata iweze kuzigeuza takwimu za ukuaji wa uchumi ili ziwe na manufaa kwa walio masikini kwa kuweza kuyastawisha maisha yao na kuupunguza umasikini wao?
Kwanza itahitaji viongozi walio imara wanaoendesha nchi kwa misingi ya utawala bora, ya uwazi na ya uwajibikaji.
Lakini tena Obama anaisifu Tanzania kuwa tayari tuna utawala bora. Na sote tunayajua mazingira ya waandishi wetu wa habari. Mmoja wao kauliwa; wengine wameshambuliwa; wengine wamefungiwa magazeti yao.
Huo ndio uwazi na uwajibikaji anaoutaja Obama. Anatudanganya na tunadanganyika. Obama ameisifu Tanzania kwa kutia saini Makubaliano na Ushirikiano wa Serikali Wazi ambayo yanalenga kupandisha nafasi ya asasi zisizokuwa za Kiserikali katika Utawala Bora, Uwazi na Uwajibikaji katika Serikali.
Marekani haichezi kwetu tu; inacheza mbele ya macho yetu kwenye ardhi nzima ya Afrika ya Mashariki. Juzi ilipeleka wanajeshi wake wanamaji nchini Somalia kupambana na Al Shabaab.
Baada ya mapigano makali majeshi hayo yalibidi yarudi nyuma na kujiondokea. Kuna maswali mengi yanayozuka kuhusika na hatua hiyo ya Marekani. Inaonyesha kuwa huo ndio utaokuwa mtindo wa majeshi yake katika nchi zetu. Watajiingilia watakavyo na watafanya watakacho.
Marekani imezizushia balaa tu nchi zetu. Kenya, kwa mfano, imetumbukia katika janga isolilalia wala kuliamkia. Tuombe tu kwamba Wakenya na sisi sote tunatambua kwamba tatizo wanalolikabili la ugaidi wa kimataifa si lao peke yao. Ni tatizo la kanda nzima ya Afrika ya Mashariki.
Hili ni tatizo lililojipenyeza katika kitovu cha eneo lililokuwa na amani na lililotulia barani Afrika. Sasa kanda yetu imegeuka kuwa moja ya maeneo moto duniani.
Tulikuwa na fursa ya kunyosha mikono yetu na kushirikiana na wafuasi wa Muungano wa Mahakama ya Kiislamu (Ittihād al-mahākim al-islāmiyya), kundi la mahakama za Kiislamu zilizoungana kuwa na utawala unaopingana na ule wa Serikali ya Mpito ya Somalia.
Lakini Marekani ilitushauri vingine. Ilisema jamaa hao ni Waislamu wenye misimamo na sera kali wataoanzisha utawala wa Kiislamu wenye kufuata Shari’a nchini Somalia.
Hivyo, Marekani ikaishawishi Ethiopia kupeleka majeshi yake kuwatimua wafuasi wa Mahakama ya Kiislamu kutoka Mogadishu na sehemu nyingine walizokuwa wamezishika.
Matokeo yake ni kuzuka kwa makundi ya Waislamu wenye vichwa mchungu zaidi, yaani makundi ya Al Shabaab na Hizbul Islam. Tunavuna walichotupandia Marekani.
Eneo letu lilikuwa na akiba kubwa ya amani na maendeleo. Na ilikuwa Kenya. Lakini viongozi wa Kenya waliifuja akiba hiyo walipounda Serikali ya Ubia baina ya Mwai Kibaki na Raila Odinga.
Viongozi hao walilipuuza eneo la Afrika ya Mashariki badili yake walishughulika wakizozana kuhusu mambo ya ndani ya nchi yao. Hawakuweza kutabiri kwamba yanayowafika sasa huenda yakawafika.
Kweli Kenya ilikuwa inauimarisha mfumo wake wa demokrasia lakini hiyo demokrasia ya Kenya leo inalitafuna eneo zima la Afrika ya Mashariki. Eneo hilo hivi sasa limo katika hali mbaya kuliko ilivyokuwa 2008.
Tanzania kwenyewe kuna mivutano ya kijamii Bara na madai ya kutaka mamlaka kamili Zanzibar. Kuna fitina nyingine ya kuzichochea iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar. Nayo ni gesi asili na mafuta yalioko katika maji ya Bahari ya Zanzibar.
Iwapo masuala hayo hayatopatiwa ufumbuzi wa kuwaridhisha walio wengi kuna uwezekano mkubwa wa kuzuka fujo za kuifanya Tanzania isiweze kukalika.
Mambo yanatokota Rwanda. Na pakiripuka Rwanda basi Congo-Kinshasa huenda ikagawika na kuwa nchi mbili au tatu.
Safari hii Watutsi wameazimia. Hawatokubali tena waonewe, wauliwe kama kuku. Watajiundia taifa lao jipya.
Mashindano yatazidi ya umilikaji visima vya mafuta Kenya, Uganda, Sudan ya Kusini na Sudan na huenda zikazifanya nchi hizo ziingie vitani.
Somalia itaendelea vivi hivi ilivyo kwa muda mrefu ujao na majeshi ya kigeni yalioko huko huenda yakayageuza maeneo yanayoyashikilia yawe maeneo yao ya kuyatawala. Matokeo yake ni kwamba Somalia itakuwa uwanja wa mapigano ya kimataifa. Kuna fitina nyingine pia huko: mafuta.
Ni vigumu kuona jinsi hali hiyo itavyonusuriwa. Kwa bahati mbaya hatuna dola kama Nigeria au Afrika ya Kusini katika eneo letu. Tumetupwa kwa mijibwa ya mwitu na kwa chui waliovaa ngozi za kondoo.
Hasara yetu ni kwamba hatuna historia yenye kutuunganisha. Kwa muda wa miaka 1,700 tumekuwa tukipigana wenyewe kwa wenyewe, tukizikuza tafauti zetu badala ya udugu wetu. Ndiyo maana ninawahusudu wenzetu wa Afrika ya Magharibi kwa namna wanavyochukuliana na kuvumiliana.
Sisi hatuna uvumilivu kama huo. Tuna matatizo na mazongezonge. Tunalala na kuamka nayo. Tanzania ingeliweza kuwa kiongozi wa eneo hili lakini siku hizi inazidi kuimarisha funganisho zake na eneo la kusini mwa Afrika na kuzidhoofisha za Afrika ya Mashariki.
Na taifa lisilo na uongozi imara wa kuliongoza halitaweza kamwe kuliongoza taifa lolote jingine. Laiti ningeweza kupanda juu ya mlima nikaunadi ukweli huo.
Chanzo: Raia Mwema

No comments :
Post a Comment