NA MHARIRI
5th November 2013
.jpg)
Ripoti ya utafiti iliyofanywa na wataalamu wa idara ya takwimu wa kampuni ya The Guardian na kuchapishwa na gazeti hili jana imedhihirisha msiba mkubwa wa kiuchumi unaoletwa na foleni za magari katika barabara mbalimbali za jiji la Dar es Salaam; sawa na tafiti nyingine kadhaa zilizowahi kufanywa na taasisi nyingine mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa utafiti huo, gharama za kiuchumi peke yake zinaonyesha kuwa takriban Sh. bilioni 411 hupotea kila mwaka kutokana na foleni.
Gharama hizi ni kubwa kuliko fedha zilizotengwa na serikali kwa ajili ya ruzuku ya mbolea katika bajeti yake ya sasa (2013/2014), ambayo ni Sh. bilioni 349.2.
Aidha, hasara hiyo kiuchumi kwa mwaka inayoletwa na foleni peke yake ingeweza pia kuisaidia serikali kwa kiasi kikubwa wakati huu ambapo imekuwa ikitoka jasho kutafuta Sh. bilioni 500 zilizotengwa katika bajati ya mwaka huu wa fedha (2013/2014) kwa ajili ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB).
Hii maana yake ni kuwa, uchumi wa taifa letu unaendelea kuathiriwa sana kutokana na mabilioni yanayopotea kila uchao kiasi cha kuathiri mipango ya maendeleo kwa kiwango kikubwa.
Gharama hizi ni mbali ya gharama za madhara ya kiafya yanayoletwa kwa wananchi wanaokaa muda mrefu ndani ya magari. Hasara hiyo haijahusisha pia uchafuzi wa mazingira utokanao na uzalishaji mkubwa wa gesi ukaa inayozalishwa na moshi mwingi wa magari yanayotumia muda mrefu barabarani.
Ripoti hiyo ilionyesha vilevile kuwa kati ya bilioni 411 zinazopotea kwa mwaka kutokana na foleni, Sh. bilioni 120.4 peke yake hupotezwa na waajiri kwa kuwalipa watumishi wao mishahara ya bure katika saa wanazotumia barabarani. Hili pia ni tatizo kiuchumi kwani huwapunguzia faida waajiri na mwishowe kuwakosesha uwezo wa kuajiri watu wengi zaidi.
Ni dhahiri kwamba madhara yote hayo yaletwayo na foleni ni mzigo mkubwa kwa taifa letu ambalo lingali likihaha kujikwamua kutoka katika kundi la nchi maskini sana duniani. Ni kero kubwa kwa wananchi inayopaswa kumalizwa haraka kwa vitendo na siyo mipango ya kwenye makaratasi.
Sisi tunatambua kuwa serikali haifurahii hali hii. Tunajua vilevile kuwa tayari ilishapokea mapendekezo kadhaa ya kitaalamu kuhusiana na namna ya kumaliza janga hili.
Uanzishwaji wa miji mipya nje ya jiji, uboreshaji wa barabara za pembezoni na ujenzi wa barabara za juu katika maeneo ya makutano ya barabara kubwa ni miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa na Wataalamu ili kukabiliana na tatizo la foleni.
Kwa nyakati tofauti, serikali kupitia wizara yake ya Ujenzi ilishatangaza mikakati kadhaa ya kupunguza foleni jijini Dar es Salaam. Kwa mfano, iliainisha barabara kadhaa za pembezoni mwa jiji zitakazoboreshwa ili wananchi wazitumie na kuepuka foleni.
Katika Bunge la Bajeti, Waziri wa Ujenzi alisema kuwa kasma 4138 imetengewa fedha za matengenezo ya barabara za Kimara - Kilungule (bilioni 1), Mbezi - Malamba mawili - Kinyerezi - Banana (bilioni 2), Tegeta - Kibaoni - Wazo - Goba - Mbezi (bilioni 2.1), Tangi Bovu - Goba (bilioni 1) na Kimara Baruti (milioni 577).
Zipo pia barabara nyingine kadhaa za pembezoni mwa jiji zinazotakiwa kutengenezwa ili kukabiliana na tatizo hili.
Serikali pia iliwahi kutangaza dhamira yake ya kujenga barabara za juu katika makutano ya barabara za Morogoro na Mandela kwenye eneo la Ubungo na Mandela na Nyerere katika eneo la Tazara.
Hata hivyo, mipango yote hiyo mizuri bado haijatekelezwa kwa kiwango cha kujivunia. Ipo miradi ambayo haijaanza kabisa. Mingine ingali ikisuasua na michache tu ndiyo iliyotekelezwa.
Sisi tunaona kwamba madhara yanayoletwa na foleni ni makubwa mno na hivyo hayapaswi tena kushughulikiwa kwa ahadi na mipango ya kwenye makaratasi.
Bali, tuwekeze nguvu zetu katika kutekeleza kivitendo mapendekezo yote ya wataalamu. Barabara za pembezoni mwa jiji zitengenezwe kwa kiwango bora, barabara za juu zitengenezwe mara moja na nyingine zinazoonekana kuwa nyembamba zipanuliwe sasa ili kuokoa uchumi wa taifa na pia kumaliza kero hii kubwa kwa wananchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment