MASUALA ya unyanyasaji wa wanaume, hali ya watoto ombaomba pamoja na hali ya watu wenye ulemavu, ni baadhi ya matatizo yaliyopendekezwa kuingizwa katika mpango kazi kwa kupewa kipaumbele cha kuyakomesha.
Aidha, Wizara inayohusika na majukumu hayo imetakiwa siku zijazo, kuyaingiza masuala hayo katika mpango kazi wake kwa kuyafanyia utafiti zaidi.
Agizo hilo lilitolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein katika mkutano wa kuhitimisha uchambuzi wa taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana na Watoto kwa mwaka 2012/2013 na robo ya mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Dk Shein akiagiza katika hotuba yake mjini Zanzibar jana, alisema serikali imelivalia njuga suala la unyanyasaji wa kijinsia na kuitaka Wizara kuyafanyia kazi ipasavyo matokeo ya utafiti wa suala hilo.
Aliipongeza Wizara hiyo kwa kufanya utafiti ambao umewezesha kuibua changamoto katika maendeleo ya jamii, hususan unyanyasaji wa kijinsia unaozidi kushamiri, Zanzibar.
Aliitaka Wizara hiyo kuzidi kupanua wigo katika utafiti wake kwa kujumuisha suala la unyanyasaji wa wanaume, unaofanywa na wanawake ndani ya jamii.
Dk Shein, alisisitiza kwa watendaji wa Wizara umuhimu wa kuimarisha na kuwa na mkakati wa ufatiliaji na tathimini maalumu. Aliitaka Wizara kuwatumia wafanyakazi wenye ujuzi na uwezo, ili kupata ufanisi.
Alisifu Wizara hiyo kwa kufanya utambuzi wa watoto wanaokabiliwa na mazingira magumu na kushauri kuandaa mpango madhubuti ambao utavutia pia taasisi nyingine, kuweza kusaidia watoto.
Naye, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alitaka Wizara hiyo kuendelea kufanya shughuli zake kwa uadilifu zaidi kwa kuwa inahudumia wananchi wanaohitaji uangalizi na huduma maalumu.
Kupitia mkutano huo uliyoshirikisha viongozi wakuu wa Zanzibar, Wizara hiyo katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, inakusudia kutekeleza malengo makuu saba.
Mapema akiwasilisha taarifa yake Waziri wa Wizara hiyo, Zainab Omar alitaja baadhi ya malengo kuwa ni kuitanua programu ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Alisema kuwa ni pamoja na kuziangalia upya sheria na sera zinazohusu watoto, wanawake, vijana na wazee ili kufanya mabadiliko ya mahitaji mapya na ya sasa.
Chanzo: HABARILEO.
No comments :
Post a Comment