Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, November 5, 2013

Sita mbaroni kupigwa mapanga Dk. Mvungi

NA WAANDISHI WETU

5th November 2013


Daktari akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal (kulia) kuhusiana na maendeleo ya afya ya Kamishina wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi aliyelazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kucharangwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa majambazi nyumbani kwake jijini Dar es Salaam juzi.
Jeshi  la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu sita wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kumvamia na kumjeruhi kwa mapanga Mjumbe wa  Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 7:30 usiku eneo la Mpigi Magohe jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo watuhumiwa hao waliiba kompyuta mpakato (laptop) moja aina ya HP, simu mbili na fedha taslimu Sh. 1,000,000.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, alisema baada ya kupokea taarifa ya tukio hilo, polisi walianzisha msako kuanzia eneo la tukio na kwa kushirikiana na raia wema, waliwatilia shaka baadhi ya watu na kuwakamata.

Kova alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa walipekuliwa na kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi puli 17 na gongo lita 15.

“Msako mkali unaendelea kwa kushirikiana na polisi wa Mkoa wa Pwani ili kuhakikisha kuwa yeyote aliyehusika na tukio hilo ni lazima akamatwe ili kukamilisha hatua za kiupelelezi na hatimaye kufikishwa mahakamani,” alisema Kova na kuongeza:

“Tulienda asubuhi  ya leo (jana) kumpa pole Dk. Mvungi na hali yake inatupa matumaini.”

Aidha, alikataa kuwataja watuhumiwa hao kwa maelezo kuwa ni sababu za kiupelelezi.

Wakati huo huo, hali ya Dk. Mvungi inaendelea vizuri ingawa bado hajapata fahamu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, hali ya Dk. Mvungi inaendelea kuimarika ukilinganisha na wakati alipofikishwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi) juzi.

Hata hivyo, Mbatia alisema hali ya Dk. Mvungi inatia matumaini baada ya kufanyiwa vipimo na kuanza kupatiwa matibabu kwenye taasisi hiyo.

Mbatia aliwashukuru watu wote wanaomwombea hasa viongozi wa dini na kuwaomba watu wote waendelee kumwombea ili afya yake izidi kuimarika haraka hasa ukizingatia kuwa Dk. Mvungi ni mtaalamu wa Katiba na ni mtu muhimu katika mchakato wa Katiba mpya.

Aidha Mbatia amewaasa wananchi wote wenye mapenzi mema ambao wanapenda kwenda kumuona Dk. Mvungi hospitalini hapo kuendelea kumwombea kwani kutokana na hali yake, watu hawajaruhusiwa kumtembelea.

Aliongeza kuwa misa ya kumuombea Dk. Mvungi inatarajiwa kufanyika leo jioni katika Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.

Mbatia alimshukuru Rais Jakaya Kikwete; Mkuu wa Jeshi la Polisi,  Said Mwema na Wajumbe wa Tume ya Katiba wakiongozwa na Jaji Joseph Warioba ambao wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa.

Alisema anatumaini Jeshi la Polisi litatimiza wajibu wake kwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wa tukio hilo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment