NA MOSHI LUSONZO
2nd November 2013
.jpg)
Madiwani hao walitaja viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Wakala wa uendelezaji wa Mji wa Kigamboni (KDA) kuwa wamejiingiza kinyemela na kupima viwanja bila kushirikisha Manispaa hiyo, kitu ambacho wamesema hakikubaliki.
Tuhuma hizo zilitolewa juzi wakati wa kikao cha Madiwani, ambapo walidai Jiji na KDA zimeanzisha mchakato wa upimaji viwanja eneo la Gezaulole bila utaratibu na kukiuka Mamlaka ya utawala za mitaa nchini.
Madiwani hao walitoa tamko la kusitisha shughuli zote za upimaji na uuzwaji wa viwanja hadi hapo serikali itakapotoa ufafanuzi.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Meya Maabad, hali kwenye ukumbi wa mkutano ilionekana kubadilika kutokana na madiwani wengi kuwa na jazba, huku baadhi ya madiwani walionekana kuwaandama wenzao wa kata zilizoingizwa kwenye mradi huo kwamba ni vigeugeu kimsimamo.
Diwani wa Mbagala Kuu, Anderson Chale, ambaye anaongoza kamati ya Miundombinu na mazingira, alisema kitendo cha Halmashauri ya Jiji kutangaza mradi wa upimaji viwanja ndani ya Manispaa ya Temeke, ni kitendo cha kihuni na hawatakikubali.
"Haitawezekana ndani ya Temeke kuwa na mamlaka tatu zenye maamuzi, haiwezekani sisi tunaangalia tu, miradi hii isitishwe haraka kwa sababu haitambuliki," alisema Chale.
Alisema kibaya zaidi kwenye mradi huo, jiji inashirikiana na mtu binafsi katika mradi huo, ambapo kisheria kama mtu anataka kupima viwanja vyake lazima aishirikishe manispaa hiyo.
"Kinachoshangaza sasa kila kitu kinakuwa kiholela ukiuliza eti hatuna mamlaka kwa sababu lipo mradi wa mji mpya wa Kigamboni," aliongeza kusema.
Hamisi Msombo diwani wa Temeke, alisisitiza kwamba vibali vya kufanya kazi hiyo vilivyotolewa na KDA na Halmashauri ya jiji ni batili, hivyo uongozi wa Manispaa ya Temeke uweke zuio la haraka kwa maslahi ya wananchi.
Aidha, madiwani hao walionya kuna dalili manispaa hiyo kumegwa vipande vipande kwa manufaa ya wakubwa, kinachohitajika kuharakishwa kwa majibu ya maombi yao ya kuachiwa kata tatu za Pembamnazi, Kisarawe 11 na Kimbiji zilizoingizwa kwenye mradi bila taarifa.
Kaimu Mkurugenzi, Erick Kurangwa, aliwataka madiwani hao kuwa na subira katika tatizo hilo kwani tayari wanafanya utaratibu wa kuomba ufafanuzi kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya makazi.
"Pamoja leo tumesitisha kazi hiyo, ninachoomba waheshimiwa tusubiri majibu yetu tuliyopeleka ofisi ya Waziri Mkuu, pia tutafanya utaratibu wa kuomba ufafanuzi kwa Wizara husika kila kitu kitakwenda sawa," alisema Kilangwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment