Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Posted Jumapili,Decemba15 2013 saa 5:12 AM
Posted Jumapili,Decemba15 2013 saa 5:12 AM
KWA UFUPI
- Mawaziri 7 waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali juzi walihojiwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete, ambapo jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema wamemshauri Rais Kikwete mam
- bo matatu; kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye kazi.
Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtupia mpira Rais Jakaya Kikwete wa kuamua hatima ya mawaziri saba, wanaotuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Mawaziri hao waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali juzi walihojiwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete, ambapo jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema wamemshauri Rais Kikwete mambo matatu; kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye kazi.
“Kamati Kuu imetoa maazimio saba ambayo yote yanazihusu wizara saba zinazoongozwa na mawaziri hao. Tumemshauri Rais Kikwete, yeye ndiye ataamua nini cha kufanya kwa sababu ndiye aliyewateuwa mawaziri hao,” alisema Nape.
Wakiwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma katika ziara ya chama hicho, Nape pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana aliwatupia lawama mawaziri hao wakati wakielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Nape alisema mawaziri hao waliitwa kuhojiwa na kutakiwa kutoa maelezo ya masuala yaliyoibuliwa wakati wa ziara hiyo ambayo pia iliwahusisha baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari jana, Nape aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Christopher Chiza, Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya (alihojiwa kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa).
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Sakata la kutaka mawaziri ‘mizigo’ kutoswa limekuwa likiibuliwa na wabunge mbalimbali katika mikutano ya Bunge mjini Dodoma, huku baadhi wakipendekeza hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda naye atoswe kutokana na kushindwa kuwasimamia mawaziri.
Ushauri wa CCM kwa JK
Nape alisema kuwa kazi ya Kamati Kuu ni kushauri, “Kazi yetu ni kushauri na siyo kufukuza. Rais Kikwete ndiye amewateua mawaziri hao, ameupokea ushauri na yeye ndiye mwenye uwezo wa kuwafukuza, kuwahamisha au kuwasukuma watende kazi. Hiyo siyo kazi yetu”
Alipobanwa zaidi kueleza ushauri ambao Kamati Kuu ilimpa Rais Kikwete Nape alisema, “Kuna ushauri mwingine ambao tumempa Rais Kikwete hatuwezi kuuweka hadharani.”
Alisema kuwa wakati wa kuhojiwa kila waziri alikuja na majibu yanayoihusu wizara yake kutokana na udhaifu ulioelezwa na wananchi.
“Katika kikao kijacho cha Kamati Kuu moja ya mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na kuangalia utekelezaji wa mambo saba tuliyoishauri Serikali kupitia hizo wizara saba,” alisema.
Nape alisema kuwa walipoeleza udhaifu wa mawaziri hao hawakueleza kuwa ni mzigo kwa Serikali, bali walilenga kueleza upungufu wao katika kusimamia masuala mbalimbali.
“Mfano Waziri wa Kilimo kwa miaka minne hajawahi kwenda mkoani Ruvuma ambako kuna ghala la chakula pia hajawahi kushughulikia matatizo yanayowakabili wakulima wa korosho na mahindi,” alisema.
Hata hivyo, Nape alisema kuwafukuza mawaziri siyo dawa na kuweka mambo sawa kwa maelezo kuwa wakati mwingine utendaji kazi ndani ya Serikali unakwenda ovyo kwa sababu ya mfumo na sheria mbovu.
“Watu wanadhani ushauri tuliompa Rais Kikwete ni kuwafukuza mawaziri, wakati mwingine kufukuza siyo mwisho wa suluhisho. Kwa mfano tumebadili mawaziri Tamisemi lakini kila mwaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha udhaifu katika wizara hiyo,” alisema Nape.
Maagizo
Nape alisema agizo la kwanza ni kuhusu kilimo cha pamba ambapo Kamati Kuu iangalie upya Serikali ipitie upya upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa pamba nchini.
Alisema kuwa kuhusu kilimo cha mkataba kwa wakulima wa pamba, Serikali imetakiwa kuratibu utaratibu wa kilimo hicho ikiwamo kutowalazimisha.
“Kwa mfano Waziri husika hajafika kwa muda wa miaka minne na nusu mkoani Ruvuma ambako ndiko kuna ghala la chakula na tulipofika Tunduma tulikuta foleni pale mizani huku watumishi wakiwa wanafanya kazi kwa saa tisa, lakini baada ya kueleza udhaifu huo sasa wanafanya kwa saa 24,” alisema.
Aliongeza, “Chama kimeiagiza serikali kutowalazimisha wakulima kutumia mbegu ya Quiton, badala yake elimu itumike zaidi badala ya nguvu.”
Alisisitiza kuwa Kamati Kuu imeitaka Serikali kuangalia upya urasimu katika uwekezaji wa viwanda nchini, hasa vinavyoongeza thamani ya mazao na kutoa ajira.
Kwa upande wa wakulima wa korosho, Nape alisema kuwa Kamati Kuu imeisisitizia serikali kujipanga kutatua tatizo la korosho na kuhakikisha inabanguliwa nchini.
“Serikali inatakiwa kuangalia upya orodha ndefu ya makato kwa wakulima hasa wa korosho na vyama vya msingi au mamlaka zinginezo, ili kuondoa makato yasiyo ya lazima na kuongeza kipato cha mkulima,”
“Kuhusu pembejeo za ruzuku Kamati Kuu imepokea taarifa ya malalamiko ya wakulima juu ya ufanyaji kazi wa mbolea ya Minjingu na kuagiza wananchi wawe huru kutumia mbolea wanayoitaka badala ya kulazimishwa,” alisema.
Kwa upande wakulima wa mahindi alisema kuwa serikali imetakiwa kumalizia malipo yaliyobaki na kuhakikisha wanakomesha utaratibu wa kuwakopa wananchi mazao yao bila kuwalipa.
“Utaratibu uwekwe wa kufanya tathmini mapema ya mahitaji na uwezo wa kununua mahindi wa serikali ili kuepusha utaratibu wa kuchukua mahindi ya wakulima bila kuwalipa,”alisema.
Nnauye alisema kwa upande wa madai ya walimu Kamati Kuu imeiagiza Serikali kukamilisha uhakiki wa madai ya walimu na kuwalipa haki zao ikiwamo kuhakikisha madeni hayazaliwi tena.
Kamati hiyo pia imekemea watendaji wachache wanaojihusisha na ubadhirifu kwenye halmashauri mbalimbali nchini.
“Serikali imeshauriwa kuangalia upya sheria kama zinakidhi mahitaji ya wakati na mazingira ya sasa ili kuongeza uwezo wa udhibiti na kuokoa pesa za walipakodi zinazopotea kwa walafi wachache kwenye halmashauri mbalimbali nchini,” alisema Nnauye.
Kwa upande wa matatizo ya upatikanaji wa maji safi na salama serikali imeagizwa kufanya mkakati wa makusudi na wa dharura kulitafutia ufumbuzi wa haraka na wa kudumu tatizo hilo ikiwamo kuangalia upya utaratibu uliotumika kuwamilikisha watu wachache maeneo makubwa ya ardhi, ambao wameshindwa kuyaendeleza badala yake wanayatumia kuwakodishia wakulima wadogo.
No comments :
Post a Comment