Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, December 22, 2013

Kujiuzulu kwa mawaziri, ndiyo ishara ya uwajibikaji

NA MHARIRI

22nd December 2013


Maoni ya Katuni
Haikutegemewa kama ingetokea kwa mawaziri wanne ghafla kujiuzulu nyadhifa zao kwa pamoja kama ilivyotokea, ingawa sehemu kubwa ya hatua  ya kujiuzulu kwa mawaziri Vuai Shamsi Nahodha wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mathayo David wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ilitokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wabunge baada ya kuanikwa kwa taarifa zenye kashfa kubwa wakati wa Operesheni Tokomeza Majangili na Operesheni Kimbunga.
Operesheni hiyo ilisimamiwa na wizara nne, kila wizara iliwajibika kwa maeneo yake ya utendaji, kuna vitendo vilivyoibuliwa na taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na Operesheni Tokomeza, kwamba kulifanyika vitendo vya unyama, mateso, ubakaji pamoja na mauaji ya watu wasiohusika.
 
Ripoti hiyo, ambayo iliongozwa na mbunge wa Kahama James Lembeli (CCM) ilibaini matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu ambayo yanadaiwa kufanywa na watendaji kutoka wizara hizo, yapo maeneo ambayo Kamati ilifanya mahojiano na wananchi walioathirika na Operesheni hiyo na baadhi yao wakatoa vielelezo vya ushahidi wa kudhalilishwa na majeshi yaliyohusika kwenye Operesheni Tokomeza.
 
Jambo ambalo lilijitokeza na kuwakasirisha wabunge zaidi, ni kwa kuona hakuna hatua za makusudi ambazo zilikuwa zikichukuliwa na mamlaka husika ili kuwawajibisha wote waliokiuka kulingana na kanuni za kazi, aidha iligundulika kuwa vitendo hivyo vilifanyika na askari mbalimbali kinyume na matarajio ya wizara husika ya kupambana na majangili.
 
Kinyume chake, Kamati ilibaini kuwa baadhi ya wananchi wakiwamo viongozi, madiwani na wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watumishi wa serikali mara kadhaa walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza, na Kamati ilibaini pia kuwa baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walikuwa hawajulikani walipo hadi Kamati ilipozuru maeneo hayo.
 
Maafa yaliyowapata waathirika wa Operesheni hii, ni dalili za wazi za namna baadhi ya wanajeshi wa majeshi yetu ya ulinzi na usalama yasivyothamini wala kujali maadili ya kazi zao, utendaji kazi wao umefananishwa na ukatili uliokuwa ukifanywa na majeshi ya kigaidi ambayo mara zote malengo yao ni kuhujumu tu badala ya kutengeneza. 
 
Majeshi yetu yalitegemewa kupambana na uhalifu wa mazingira ya wanyamapori, pamoja na kuwakamata majangili na kuwapeleka katika vyombo vya sheria, badala yake majeshi hayo yalijichukulia madaraka ya kuwa mahakimu.
 
Sisi tunawapongeza mawaziri walioamua kubeba mzigo wa mabaya na uchafu  uliofanywa na watendaji wao, tunafahamu kwa dhati kuwa mawaziri waliojiuzulu, hawakuhusika moja kwa moja na tuhuma za vitendo vya unyama, mateso, ubakaji pamoja na mauaji yanayodaiwa kufanywa wakati wa Operesheni Tokomeza.
 
Mawaziri hao wanne wamefikia uamuzi wa kuachia madaraka yao ikiwa ni ishara ya kuwajibika kisiasa, kulaani vitendo hivyo, kulinda na kutetea heshima ya Watanzania wote walioathirika kwa njia moja au nyingine wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. 
 
Tunaungana na mawaziri waliojiuzulu  kwa  kuwapa pole wananchi wote waliokumbwa na kadhia hizo wakati operesheni hiyo ikiendelea, tunaamini kuwa mfumo wa utekelezaji wa majukumu ya majeshi yetu ya ulinzi na usalama utabadilika na kufuata kanuni halisi za ulinzi wa kudhibiti majangili katika maeneo yote ya Hifadhi za Taifa.
 
Tunaamini kuwa serikali haitaridhika kwa hatua ya mawaziri kujiuzulu peke yake, badala yake itaunda Tume ya Uchunguzi ya Kimahakama ili kuchunguza waliohusika na unyama huo wakati wa Operesheni, kinachosubiriwa ni hatua kwa wote waliohusika na uchafu huo ambao hatimaye umesababisha mawaziri kuwajibika.
 
Hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wahusika wote walioshiriki katika kashfa hiyo ili liwe funzo kwa wengine, na majeshi yetu yarejeshe imani kwa wananchi kwa kuwa waadilifu, wenye nidhamu ya juu pamoja na uzalendo wa kweli kwa nchi na raslimali zake.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment