NA MUHIBU SAID
1st December 2013
Amwaga upupu hadharani…asema kuwatimua Zitto, Kitila ni ujuha
Bregedia Greyson Nyakarungu aibuka na kudai kutishiwa maisha
Chitanda, ambaye alikuwa pia ni Katibu Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema, anakuwa kada wa pili muhimu kujiuzulu, baada ya Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi, kujiuzulu rasmi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa.
Arfi alifikia uamuzi huo siku moja baada ya Kamati Kuu (CC) kumvua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na aliyekuwa Mjumbe wa CC, Dk. Kitila Mkumbo, nafasi zao katika chama hicho, wiki iliyopita.Chitanda katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ametaja sababu mbalimbali zilizomfanya afikie uamuzi huo, ikiwamo kupinga ubaguzi wa kidini, ukabila na upendeleo katika ulipaji wa maslahi miongoni mwa watendaji aliodai kuwamo katika chama hicho.
Sababu nyingine amedai ni uamuzi wa CC wa kumvua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na aliyekuwa Mjumbe wa CC, Dk. Kitila Mkumbo, nafasi zao za uongozi katika chama hicho.
Chitanda amekwisha muandikia barua Katibu wa Chadema Mkoa huo kumuarifu kuhusu uamuzi wake huo, ambayo nakala yake imesambazwa pia kwenye vyombo vya habari.
Katika barua hiyo yenye kichwa cha habari Kujiuzulu uenyekiti wa mkoa, Chitanda, pamoja na mambo mengine, amedai kuwa amefikia uamuzi huo bila ya kushawishiwa na mtu yeyote.
Katika barua hiyo alisema "Matarajio yangu ya kuweza kukomboa wanyonge kupitia Chadema kwa sasa sioni kama yanaweza kufikika.”
Aliongeza kuwa atabaki kuwa mwanachama wa kawaida na kuahidi kuwa mwanachama mwaminifu na atakuwa tayari kusaidiana na viongozi kujenga chama.
Chitanda, ambaye alijiunga na Chadema mwaka 2003 akitokea NCCR-Mageuzi, alisema anapinga CC kuridhia uteuzi wa wakurugenzi watano wa chama hicho.
Alisema pia uteuzi huo unakwenda sambamba na kuboresha maslahi yao kwa kuongeza posho kutoka Sh. 800,000 za awali hadi Sh. milioni 1.5 hadi Sh. milioni 2.5 kwa mkurugenzi na kutoka Sh. 680,000 hadi Sh. milioni moja na Sh. milioni 1.5 kwa Afisa Mwandamizi.
Alisema yupo Chadema kwa miaka 10 sasa na ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa Chama hicho, hivyo haoni sababu ya kutoharakisha kulipa posho ya makatibu wa wilaya na mikoa pamoja na watendaji wengine.
MAAMUZI YA CC DHIDI YA ZITTO, DK. KITILA
Chitanda alisema maamuzi ya CC dhidi ya Zitto na Dk. Mkumbo ni ya kijuha, ambayo yanawafanya Watanzania waangalie mara mbili mbili kama Chadema iko makini na ukombozi wanaouhubiri.
Alisema wamekuwa wakiweka mikakati mbali mbali ya ushindi ili chama kishinde na kutolea mfano, kwamba kabla hata ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, wakati tu ilipobainika anaugua, chama kiliandaa mkakati wa kushinda ubunge wa jimbo hilo na uchaguzi uliporudiwa mkakati ule ulitumika na kushinda.
Chitanda alisema akiwa mtendaji wa ofisi ya katibu mkuu, ameshiriki pamoja na Zitto na Katibu Mkuu, Dk. Slaa kupanga mikakati mbali mbali mizuri na mibaya kwa nchi, lakini hawakuwahi kuitwa wasaliti, wahaini wala hana lolote baya.
Chitanda alisema akiwa katibu wa sekretarieti wamekuwa wakilazimishwa mara kadhaa kuwashawishi wajumbe wengi kutowaunga mkono watu wenye misimamo thabiti ndani ya chama na badala yake wamekuwa wakitumia rasilimali za chama kuwajenga wajumbe ndio.
Aliongeza: “Nafsi yangu haipo tayari kuendelea kuwa sehemu ya upotoshaji dhidi ya Watanzania wenzangu. Nafsi yangu inanikataza kabisa kuendelea kufumbia macho maovu yanayoendelezwa na chama changu.
Nafsi yangu imechoka kuendelea kushuhudia ubaguzi wa kidini na kikabila unaofanywa wazi wazi na viongozi wa chama changu. Nafsi yangu imekataa sasa, haipo tayari tena kuwa kuwadi wa kuwahadaa Watanzania kuyafikia matarajio tunayowapa ambayo kamwe hayafikiki.”
Alisema haamini kwamba kuvuliwa nyadhifa kwa Zitto na Dk. Kitila ni kwa sababu ya waraka wa ushindi, kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, bali anaamini kuvuliwa kwao ni kutokana na hofu ya uchaguzi, ubaguzi wa kikabila na kikanda.
“Kwa kuwa vipaumbele vya Chadema ni kukijenga chama mikoa ya Kaskazini, basi sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi tunawatakia kila la heri, na kwamba waendelee kukijenga chama chao huko huko waliko. Nashukuru wote ambao nilifanya nao kazi pamoja katika kutekeleza majukumu yangu.
ADAI KUTISHIWA MAISHA
Baada ya kuongoza uasi wa wanafunzi wa vyuo vikuu jjini Dar es Salaam, Brigedia Greyson Nyakarungu, ameibuka na kudai anatishiwa maisha na viongozi wa Chadema, wakikasirishwa na hatua yake ya kuongoza wanafunzi kupinga uamuzi wa Kamati Kuu.
Akizungumnza na NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu kutoka mjini Morogoro, Brigedia Nyakarungu, ambaye ni mwanachama wa siku nyingi wa chama hicho, alisema tayari ameripoti polisi kwa ajili ya kupewa ulinzi.
Hivi karibuni, Nyakurungu akiwa na baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali, alitoa tamko la kupinga uamuzi wa kamati Kuu kumvua nafasi zote aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe.
Katika tamko hilo, alitoa tishio la kutangaza uasi nchi nzima endapo uamuzi huo hautaangaliwa upya kwa maslahi ya chama. "Baada ya kutoa tamko lile, nimetumiwa ujumbe wa kuuawa mara moja kwa sababu nataka kukiua chama," alisema Nyakarungu.
Aliwataja baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho (majina yanahifadhiwa) kwa kuhusika na mpango huo. Alisema siri hiyo ilijulikana baada ya kiongozi mmoja ambaye hakukubaliana na mpango huo, kumpigia simu na kumtahadharisha kuwa makini kwani kuna mkakati wa kumuondoa duniani.
Baada ya kupewa taarifa hizo, Nyakurungu alikwenda kituo cha polisi mkoa na juzi kufungua faili la malalamiko. Aidha, alipewa RB yenye namba MOR/RB/12999/13, ambapo alitakiwa kurudi kesho yake kutoa taarifa.
Brigedia Nyakurungu aliingia kwenye chama hicho mwaka 2004 na kupewa nafasi ya utendaji mtendaji makao makuu.
Taarifa hii imeandikwa na Moshi Lusonzo na Muhibu Said
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment