NA MWANDISHI WETU
2nd December 2013
.jpg)
Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa uwekezaji katika sekta nyingi za uchumi zimefanya vizuri isipokuwa sekta ya kilimo.
Akizindua ripoti hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, alisema serikali bado inaendelea kuyafanyia kazi maeneo mbalimbali ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji nchini.
“Kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta za madini na gesi ili kuisaidia nchi kupata faida zaidi na kutumia fursa hiyo kujenga miundombinu katika sekta ya ya Kilimo ili nayo iweze kuvutia uwekezaji zaidi,” alisema.
Alisema ripoti hiyo imeonyesha kuwa mazingira ya uwekezaji nchini ni mazuri na yanavutia wawekezaji kuja kuwekeza.
Nagu alisema katika mazingira hayo serikali ingependa kuona ongezeko hilo la uwekezaji linaenda sambambana na maendeleo ya uchumi wa watanzania wa kawaida.
Ripoti hiyo imekuja baada ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Ofisi ya Taifa Takwimu (NBS), kufanya utafiti ambao umekuja na majibu yaliyolenga kuonyesha hali halisi na changamoto zilizopo ili kupata fursa ya kufanya maboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Dkt.Nagu alisema kuwa serikali itatumia ripoti hiyo na kuhakikisha inakuwa ni sehemu ya kufanyia maboresho ya sera ya uwekezaji ambayo itaweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC), Juliet Kairuki alisema utafiti huo uliohusisha kampuni zilizowekeza Tanzania Bara na Visiwani utatumika katika kupanga mikakati zaidi ya kuongeza uwekezaji.
Naye Mkurugenzi wa Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, alisema utafiti huo umefanyika kwa kufuta vigezo vya Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa .
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment