Na Daniel Mjema, Mwananchi
Posted Jumapili,Mei4 2014 saa 15:52 PM
KWA UFUPI
Kikwete akitoa siku 60 tu kwa Katiba katika sherehe za May Day 2014.
Bado najiuliza na sipati majibu kwamba, inakuwaje tuteketeze Sh100 bilioni kutengeneza Katiba Mpya ya wananchi inayotokana na maoni ya wananchi wakati watawala walishaweka msimamo wao?
Nasema wameweka msimamo kwa sababu hata Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwasisi wa mchakato huo wa Katiba amenukuliwa akisema wanaotaka Serikali tatu wasubiri aondoke madarakani.
Sasa kama Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama, anasema Serikali tatu hapana, bali anataka serikali mbili. Kulikuwa na haja gani ya kuteketeza mabilioni haya ya walipa kodi?
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema katika mkutano wa Bunge la Katiba lililositisha shughuli zake mjini Dodoma kuwa Serikali imetumia Sh27 bilioni kuendesha Bunge Maalumu la Katiba kwa siku 67.
Ikumbukwe kuwa Agosti 5 mwaka huu wakati Bunge hilo litakaporejea, Watanzania wataendelea kushuhudia sinema hiyo kwa siku nyingine 60, ambazo kwa uchache zinaweza kuligharimu taifa si chini ya Sh25 bilioni za walipa kodi.
Kabla ya kuanza kwa Bunge hilo, tulielezwa Sh8.6 bilioni zimetumika kukarabati ukumbi wa Bunge hilo na miundombinu yake na kuweka vifaa vya kisasa vikiwamo vifaa vya usalama.
Mbali na fedha hizo, taarifa zisizo rasmi zinaelezwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, nayo imetumia Sh69 bilioni kukusanya maoni ya Wananchi.
Anasema kutokana na pesa nyingi kuelekezwa katika Bunge hilo lenye wajumbe 629, Serikali imesitisha kupeleka, Maji, Umeme na huduma nyingine vijijini ili tu Bunge hilo litupatie katiba bora.
Hapa nawahurumia Watanzania. Nasema nawahurumia kwa sababu wanatoka na wataendelea kutoka jasho kugharimia Bunge hilo lililojaa aibu ya mipasho, kejeli, matusi na kila aina ya sinema.
Bado najiuliza swali lile lile nililoanza nalo mwanzo, inakuwaje tuteketeze mabilioni yote haya kuwapa wanafunzi mtihani wakati jibu linafahamika hata kwa wasio wanafunzi kuwa ni Serikali mbili? Baada ya mabilioni hayo kuteketea, Tume ilikuja na maoni ya wananchi ya Serikali tatu, lakini watawala wetu hawataki kuamini na wanaishutumu kupika takwimu. Hawataki kusikia la mtu!.
Bado najiuliza, Rais Kikwete aliundaje Tume ikakusanye maoni wakati akijua ndani ya utawala wake hataruhusu muundo wa Serikali tatu? Inakuwaje tuteketeza mabilioni haya wakati jibu linajulikana?
Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imefanyiwa mabadiliko (viraka) mara 14 hadi kufikia mwaka 2005. Kwa nini hawakutumia njia hiyo kama lengo lilikuwa serikali mbili?
Katika kitabu cha “Mwongozo wa Katiba kwa Raia” cha taasisi ya Policy Forum mwaka 2011, imeanisha misingi mikuu ya katiba kuwa ni pamoja na iwezeshe wananchi kuridhiana kitaifa.
Pamoja na kwamba katiba siku zote huwa ni tendo la maridhiano, mchakato tunaoupitia unaonyesha mushkeli, kwamba watalawa hawataki maridhiano. Kwao ni Serikali mbili tu.
Nasema hawataki maridhiano kwa sababu hata Rais Kikwete mwenyewe ametamka hivyo na sote tunafahamu, kauli yoyote ya Rais iwe ya utani ama thabiti, huwa ni maelekezo kamili.
Huenda huu ndiyo mtazamo pia wa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuamua kususia Bunge hilo ili kuepuka kuwa Rubber Stamp (muhuri) wa kupitisha matakwa ya watawala.
Ni ukweli usipingika kwamba karibu asilimi 75 ya wajumbe wote ndani ya Bunge hilo ama ni wabunge wa CCM ama ni wajumbe wanaotokana na taasisi hiyo ama uteuzi wao una uhusiano na CCM.
Sasa kama Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM taifa, amesema Serikali mbili, asilimia 75 ya wajumbe ni makada wa CCM, nani atazuia Serikali mbili. Ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mikono.
Kwa hiyo, kama hivyo ndivyo, bado najiuliza kulikuwa na haja gani ya kuteketeza zaidi ya Sh100 bilioni za walipa kodi masikini kuunda Tume, kuunda Bunge wakati kinachotakiwa kinajulikana?
Mimi nataka niitahadharishe Serikali kwamba, kama kweli maoni ya Watanzania walio wengi yalikuwa ni Serikali tatu, basi wajue muundo wa Serikali mbili utakwama kwenye kura ya maoni.
Ushauri wangu, kabla hatujaendelea kutafuta Sh104 bilioni, turudi kwa wananchi ili waamue kwanza kwa kura ni aina gani ya muundo wa Serikali wanautaka baada ya hapo ndipo tuendelee na Bunge.
Tukifanya hivyo tutaokoa mabilioni ya shilingi ambayo yameteketea na yatakayoendelea kuteketea kwa siku zote 127 ambazo Bunge litakutana na mwisho wa siku wananchi wapige kura ya HAPANA!
Tuamue sasa kwa kura muundo tunaoutaka ili tuokoe Sh100 bilioni kuteketea halafu mwisho wa siku tushindwe kupata katiba mpya, tukarudi katiba ya 1977. Tutakuwa tumetwanga maji kwenye kinu!
http://www.mwananchi.co.tz/Katiba/Kuna-maana-gani-kupoteza-mabilioni-haya-kwa-Katiba-/-/1625946/2303406/-/item/1/-/enbqegz/-/index.html

No comments :
Post a Comment