Toleo la 337 Raia Mwema
5 Feb 2014
WAKATI
Tanzania na Malawi zinaweza kuwa zinaendelea na mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa
(Ziwa Malawi) Idara ya Mazingira ya Wizara ya Mazingira na Mabadiliko ya
Tabianchi ya Malawi imetangaza kuanza kusikiliza maoni ya umma juu ripoti ya
Athari za Jamii na Mazingira (ESIA) ya kampuni ya mafuta ya Surestream
Petroleum, inayotaka kutafiti mafuta ndani ya ziwa hilo.
Taarifa
iliyosambazwa mwishoni mwa mwezi uliopita (Januari 2014) nchini Malawi kupitia
mitandao mbalimbali inawahimiza raia wake kupeleka maoni yao kuhusiana na
athari zinazoweza kutokea katika utafiti huo na hatimaye uchimbaji mafuta.
Kampuni
ya Surestream Petroleum ya Uingereza imepewa kibali cha utafiti wa mafuta
katika maeneo mawili yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,000 ndani ya ziwa
hilo tangu mwaka 2011.
Ziwa hilo lina ukubwa wa kilometa za mraba 29,000.
“
Kama ilivyotangazwa, umma unaalikwa kupitia ripoti ya ESIA kama inavyoagizwa na
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (1996) na kutoa maoni kwa Idara ya Mazingira
ifikapo Februari 12, 2014, kabla ya uamuzi wa serikali wa ama kuzuia au
kukubaliana na shughuli za utafiti za Surestream,” inasema taarifa hiyo
inayoambatana na mkanda wa video wa Surestream, unaoitwa: Malawi A New Dawn
(Kumekucha Malawi) http://www.surestream-petroleum.com/video-3.htm
unaozungumzia jinsi Malawi itakavyonufaika na mafuta.
Mzozo
unaorejewa katika utangulizi unahusu mvutano wa mpaka kati ya Tanzania na
Malawi, nchi mbili jirani zinazochangia Ziwa Nyasa (kwa Tanzania) na Ziwa
Malawi (kwa Malawi) na ambazo huko nyuma zilipata kuvutana kuhusu ulipo mpaka.
Malawi imekuwa ikidai kuwa inamiliki maji yote ya ziwa hilo huku Tanzania
ikisema mpaka uko katikati ya ziwa.
Kila
nchi ina sababu zake. Malawi inasema inafuata makubaliano ya Mkataba wa
Heligoland wa Julai 1, 1890, kati ya Ujerumani na Uingereza unaoonyesha kwamba
Malawi inamiliki maji yote ya ziwa mpaka kwenye ufukwe wa upande wa Tanzania.
Kwa
upande wake, Tanzania inasema inafuata makubaliano ya baada ya Vita ya Kwanza
ya Dunia kuelekea mwaka 1920 baada ya kuwa Ujerumani imeshindwa katika vita
hiyo, iliingia makubaliano na Uingereza, mpaka ukawekwa katikati kwa maana ya
kila nchi ambazo wakati huo (Tanganyika na Nyasaland) zilikuwa zinatawaliwa na
bwana mmoja, Uingereza, kila moja imiliki asilimia 50 ya maji ya ziwa.
Nyaraka
kadhaa zinaonyesha kwamba huo ni mzozo wa muda mrefu kati ya Tanzania na Malawi
uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 na japo sasa umefikishwa mbele ya usuluhishi wa
rais wa zamani wa Msumbiji, Joaqium Chissano, na wakubwa wenzake, taarifa
kwamba Surestream inaweza kuendelea na utafiti wa mafuta ndani ya ziwa
zinaupasha moto zaidi sasa, pamoja na mambo mengine, taarifa za utajiri wa
mafuta zikizingatiwa.
Katika
hatua nyingine, akihutubia katika kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 37
ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete alisema
Watanzania wanaoishi kando ya Ziwa Nyasa wasiwe na hofu kwani suala hilo la
mzozo wa mpaka linashughulikiwa na wazee wenye busara.
“Kama
kuna mwanasiasa analizungumzia suala hili anatafuta umaarufu tu. Lipo katika
hatua nzuri na Kamati ya Chissano itatueleza ukweli,” alisema Kikwete Jumapili,
Februari 2, 2014, kwenye sherehe hizo mjini Mbeya alikohutubia kama Mwenyekiti
wa CCM.
Ukiacha
hayo ya Tanzania na Malawi, umekuwapo mvutano wa waziwazi kati ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ) kuhusiana na umiliki wa mafuta yanayoelezwa kuwa huenda
yakapatikana Zanzibar, hasa maeneo ya Pemba.
Baadhi
ya wanasiasa wa Zanzibar, akiwamo Ismail Jussa Ladhu, kwa nyakati mbalimbali,
wamekuwa wakieleza kwamba pindi yakipatikana mafuta, basi utajiri huo utakuwa
ni wa watu wa Zanzibar.
Katika
mwendelezo wa fikra hizo, Juni 28, 2012, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliliambia
Bunge kwamba Serikali ya Muungano haikuwa na pingamizi kwa Zanzibar kuanzisha
utafiti na uchimbaji mafuta Visiwani.
Akizungumza
katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu bungeni, Dodoma, Waziri Mkuu Pinda
alisema Serikali ilikuwa inaangalia taratibu za kuiwezesha Zanzibar kuendelea
na utafiti wa mafuta huku ikipitia vipengele vya sheria na Katiba kuamua kama
suala la mafuta liendelee kubaki kuwa la Muungano au la.
Alikuwa
akijibu swali la Mbunge wa Konde (Pemba), Khatibu Said Haji (CUF), aliyetaka
kujua msimamo wa Serikali ya Muungano juu ya taarifa ya Waziri wa Nchi wa SMZ,
Mohamed Aboud, kwamba utafiti na uchimbaji mafuta Zanzibar utafanywa na SMZ.
Kwa
mujibu wa mbunge Khatibu Said Haji, katika swali lake kwa Waziri Mkuu Pinda,
suala la mafuta ya Zanzibar lilikuwa kati ya changamoto nyingi zilizokuwa
zikiusukasuka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kwamba msimamo wa Zanzibar,
ambao alisema tayari ulikwisha kuelezwa kwa uwazi, ulikuwa ni mafuta hayo
yachimbwe na Zanzibar.
“
Binafsi sioni tatizo hapa… iwapo Zanzibar itagundua mafuta, sisi hatutapoteza
chochote, badala yake tutakuwa tukipata mafuta jirani, bei itakuwa
nafuu,” alijibu Waziri Mkuu Pinda na kuongeza kwamba tatizo lilikuwa ni kwenye
sheria na Katiba na kwamba jitihada zinafanyika utafiti uendelee huku taratibu
za kisheria na Katiba zikiendelea kwa vile “utafiti na uchimbaji mafuta
huchukua mpaka miaka minane”.
Mwishoni
mwa mwaka jana, SMZ iliingia makubaliano ya awali (MoU) na kampuni ya Uingereza
ya mafuta na gesi asilia, Shell, wakati wa ziara ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali
Mohamed Shein. Taarifa zinasema Mtendaji Mkuu wa Shell, Peter Voser, alisaini
mkataba huo kwa niaba ya kampuni yake huku Waziri wa Nishati, Ramadhan
Abdallah Shaaban, akisaini kwa niaba ya SMZ.
Taarifa
zinasema chini ya mkataba huo SMZ imeipatia Shell idhini ya kutafiti na
hatimaye kuchimba mafuta katika vitalu vinne Zanzibar: vitalu namba 9,10,11 na
12.
Nyaraka
zinasema kwamba katika kauli mbalimbali, magwiji wa sheria na Katiba nchini,
Profesa Issa Shivji na Dk. Rugemeleza Nshala, waliuita mkataba huo kati ya SMZ
na Shell kuwa ni batili na uliokwenda kinyume cha Katiba ya Tanzania.
Akizungumza
mwishoni mwa mwaka jana kutokea Kilwa Masoko katika mafunzo ya wanahabari ya
mafuta na gesi, yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Profesa
Shivji, alisema mafuta na gesi ni mambo ya Muungano, na kwa hiyo ni Serikali ya
Jamhuri ya Muungano pekee yenye uhalali wa kisheria kusaini mkataba wowote
unaohusiana na jambo hilo.
“Masuala
ya mafuta na gesi yaliongezwa kwenye mambo ya Muungano na Mzee Karume (Abeid
Amani Karume, rais wa kwanza wa SMZ) mwenyewe mwaka 1968. Zitafuteni Hansard
(taarifa za mazungumzo bungeni) zipo. Hao wanaopiga propaganda kwamba mambo
hayo yaliingizwa kinyemela kwenye mambo ya Muungano ni watu wa kupuuzwa,”
alisema Profesa Shivji.
Dk.
Nshala alisema kwa kusaini makubaliano hayo, SMZ na Shell walikuwa wamevunja
Katiba kwa vile si wahusika sahihi.
“Mwenye
mamlaka ya kisheria kusaini mkataba wowote unaohusu nishati na madini, kwa
mujibu wa Katiba, kwa niaba ya Serikali (ya Muungano) ni Waziri wa
Nishati na Madini. Suala la mafuta na gesi asilia viko chini ya
Muungano.…unajua kuna watu wanataka kutumia kipindi hiki ambacho tuko kwenye
mchakato wa kuandika Katiba mpya kuvuruga Muungano,” alisema Dk. Nshala ambaye
ni mbobezi katika mikataba ya madini, mafuta na gesi.
Mkanganyiko
wanaouzungumzia Profesa Shivji na Dk. Nshala ulipata kutajwa katika muongo
uliopita kwenye utafiti uliofanywa mwaka 2009 na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi
na Kijamii (ESRF) kwa niaba ya The Norwegian People’s Aid chini ya mada:
Petroleum Exploration Study.
Inasema
sehemu ya utafiti huo kuonyesha changamoto mbalimbali zinazoigonganisha Serikali
ya Muungano na SMZ kuhusu milki ya maliasili kama mafuta kwenye masuala ya
sera: ” utafiti umeonyesha kwamba si Tanzania (Serikali ya Muungano) wala
Zanzibar yenye sera timilifu ya kitaifa ya utafiti na maendeleo ya mafuta.
Serikali
ya Muungano ina Sera ya Taifa ya Nishati (1992 na 2003) na sera nyingine
zinazowezesha ukuzaji wa sekta ya mafuta Tanzania. Serikali ya Zanzibar haina
sera timilifu ya nishati. Ndiyo kwanza iko katika mchakato wa kukamilisha sera
yake yenyewe ya nishati ”.
Utafiti
huo unataja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na Katiba. “Serikali ya Muungano
ina sheria mbalimbali zinazoathiri maendeleo ya shughuli za mafuta, kwa kuanzia
na (1) Katiba ya Jamhuri ya Muungano, (2) Sheria ya Petroli ya mwaka
1980; Sheria ya EWURA ya 2001, na (3), Sheria ya
uhifadhi wa Petroli ya 1987, ambayo sasa imerekebishwa na Sheria ya 2008.
“Kuna
changamoto nyingi bado. Ibara ya 4 (3) ya Katiba inasema maliasili kama madini,
mafuta na gesi zipo chini ya usimamizi wa Jamhuri ya Muungano. Kwa ajili ya
uendeshaji mzuri wa mambo ya Jamhuri ya Muungano na kwa kutoa mamlaka kwa
vyombo vinavyotajwa katika Ibara hii. Aya ya 15 ya jedwali la kwanza la Katiba
chini ya Ibara ya 4 inasema kwamba madini, mafuta na gesi ni masuala ya
Muungano. Na hapo ndipo penye mkanganyiko na panapozua mjadala wa je, mafuta ni
suala la Muungano au la.”
Kama
itapitishwa ilivyo kuwa Katiba, Rasimu ya Katiba mpya inaweza kutoa suluhisho
la mvutano uliopo kati ya Serikali ya Jamhuri na SMZ kuhusu suala la umiliki wa
mafuta.
Rasimu
inapendekeza katika Ibara ya 63 kwamba: “ Kwa ajili ya utekelezaji bora wa
shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa
madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika Ibara ya 61,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka juu ya mambo ya Muungano
kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Katiba hii”.
Ibara
ya 61 (1) kwa upande wake inasema: “ Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa
ndiyo chombo chenye mamlaka ya utendaji, Bunge litakuwa na mamlaka ya kutunga
sheria kwa mambo ya Muungano na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali
ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama itakuwa ni chombo cha utoaji haki; (2) Kila
chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake kwa
kufuata masharti ya Katiba hii ”.
Aidha,
Rasimu ya Katiba mpya katika Nyongeza: Mambo ya Muungano inataja mambo saba tu
kuwa ndiyo yasimamiwe na Serikali ya Muungano. Hayo ni Katiba na Mamlaka
ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania; Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania; Uraia na Uhamiaji; Sarafu na Benki Kuu; Mambo ya Nje; Usajili wa
Vyama vya Siasa; na, Ushuru wa Bidhaa za mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na
Mambo ya Muungano.
Mivutano
ya maeneo ya mipakani inayotokana na nchi kutaka kumiliki rasilimali kama
madini, mafuta na gesi si mipya katika Afrika ingawaje sasa inaonekana sana
ndani ya Afrika Mashariki na eneo zima la Maziwa Makuu.
Kwa
nini Afrika Mashariki? Sababu ni kwamba eneo hilo lipo karibu na China na India
kulinganisha na maeneo mengine.
Nyaraka
kadhaa zinasema kwamba huko nyuma eneo hilo halikufahamika kwa wengi kuwa
lingekuwa na utajri mkubwa wa gesi na mafuta. Ndiyo kwanza wengi wamefahamu.
Kwa
mujibu wa nyaraka hizo za kwenye mitandao kama wa www.nextoilrush.com,
sifa au kivutio kikubwa kitakuwa ni nafasi ya kijiografia ya eneo hilo kuwa
karibu na bara la Asia, na hasa, kuwa karibu na China na India, nchi mbili
ambazo sasa ziko mbele katika maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji. Ukaribu huo
unalifanya eneo la Afrika Mashariki kuwa kivutio zaidi kwa China na India
katika gesi na mafuta.
“Mahitaji
ya mafuta ya China na India bado yako chini kulinganisha na nchi zilizoendelea
za Magharibi. Lakini idadi ya watu wa China inakaribia bilioni 1.34. India
inaifuatia China kwa karibu ikiwa na watu wapatao bilioni 1.21.
“Ulaya
ina idadi ya watu wapatao milioni 500, Marekani inao kiasi cha milioni 300.
Unaweza kuona ni kiasi gani cha mafuta kitaweza kutosheleza idadi ya karibu
Wachina na Wahindi wapatao bilioni 2.5 ambao karibuni wataanza kutumia mapipa
zaidi ya mafuta kwa kila mtu katika matumizi ya kuongeza joto majumbani, umeme,
magari, usafiri na huduma nyingine,” zinasema nyaraka hizo.
Zinaongeza
nyaraka hizo: “ Yatakapokuwa mahitaji hayo yanaanza kukua, kampuni kubwa za
mafuta zitahitaji kuwa na hazina ya mafuta na gesi katika vituo vya karibu na
masoko makubwa, yaani China na India, na vituo hivyo ni Afrika Mashariki.
“Kukodisha
meli za kusafirishia gesi na mafuta ni gharama kubwa na gharama hizo hulipwa
kila siku. Gharama hizo kutoka kwenye chanzo hadi sokoni hurundikiwa mnunuzi
kwa hiyo ina maslahi kama mnunuzi atapata shehema karibu na kwake. Hii ndiyo
sababu iliyosukuma kujengwa kwa Mfereji wa Panama.”
Nyaraka
hizo zinasema ni ukaribu wa aina hiyo kwa masoko ya China na India uliozivuta
kampuni kubwa duniani kama Chevron, Exxon Mobil na ConocoPhilips, Total na
Shell kuwekeza karibu dola za Marekani bilioni 200 katika miradi ya gesi
Australia. Wakati tayari Australia imeanza mchakato wa uzalishaji, itachukua
miaka hata 10 kwa Afrika Mashariki kuweza kuanza kuzalisha mafuta.
- See more at:
http://www.raiamwema.co.tz/mafuta-bahari-ya-hindi-ziwa-nyasa-mtego-mpya-mipakani#sthash.fV5e7aBS.dpuf
No comments :
Post a Comment