dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, August 25, 2014

Tukuze Sayansi kwa vitendo

Muandishi Bw. Salim Said Salim

Tanzania Daima

Na Salim Said Salim
KATIKA mashindano ya utafiti wa sayansi kwa wanafunzi wa somo hili nchini yaliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Shule ya Lumumba ya mjini Unguja ilinyakua nafasi ya kwanza.
Shule karibu 100 kutoka kila pembe ya Jamhuri ya Muungano zilishiriki katika mashindano haya yaliyoandaliwa na mradi wa wanasiasa wachanga wa Tanzania.
Karibu wanafunzi 100 kutoka shule mbali mbali nchini walishiriki mashindano haya.
Kutokana na ushindi huu, shule ya Lumumba sasa itaiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika nchini Ireland baadaye mwaka huu.
Vile vile wanafunzi wawili wa kidato cha sita wa shule hiyo waliofanya utafiti huo watapatiwa ufadhili wa masomo ya shahada ya kwanza nchini Ireland na pia walipewa zawadi ya sh. milioni moja.
Kwa kweli kiwango hiki cha zawadi ni kidogo sana na inaonekana kama tunafanza mzaha na kutojali elimu kama tunavyofanya kwa ngoma na mashindano ya urembo ambapo mshindi huzoa mamilioni.
Wanafunzi waliofanya ubunifu huu, Dhariha Amri Ali na Salma Khalfan Omar, walilenga kuwawezesha Watanzania kutumia mali ghafi zinazopatikna hapa nchini kuuwa au kukimbiza nzi na mbu badala ya kutumia kemikali zinazoagizwa kutoka nchi za jirani na mbali.
Baadhi ya kemikali hizi zimesemekana kuwa na athari kiafya na kimazingira na baadhi yao hata husemekana kuwa zimepigwa marufuku kutumika hata katika hizo nchi zinapotengenzwa.
Lakini sisi Tanzania kwa vile tumekubali kugeuzwa jalala tunaendelea kusema…lete kwetu unachotaka, kiwe kipya au ni mtumba,  kwa vile sisi tumeamua kuendelea kuwa wakarimu sana na maisha yetu sio muhimu.
Miongoni mwa sababu ziliopelekea shule hii kujipatia ushindi ni utafiti uliofanywa na wanafunzi wake uliobainisha matumizi mbadala ya dawa ya kuua au kukimbiza nzi na mbu kwa kutumia karafuu, mchaichai na kitungu thomu (kitungu saumu).
Pamoja na kuwapatia wanafunzi hawa mafunzo zaidi ni muhimu kwa serikali kuvienzi na kuvitunza vipaji hivi kwa vile hii ni hazina inayoweza kuisaidia sana Zanzibar na Tanzania kwa jumla hapo baadaye.
Uzoefu umeonyesha mara nyingi kuchomoza vipaji kama vya hawa wasichana wawili wa Zanzibar huwa tunafurahia mafaniki yao kwa wakati ule, lakini huwa hatuzingatii baadaye njia muafaka za kuwaendeleza hao wabunifu na mafanikio yao.
Kwa mfano mwanzoni mwa miaka ya 1980 alikuwepo mhandisi mmoja kule Iringa, Thabit Nassor Lipangile, ambaye ndiye aliyebuni njia ya kusafirisha maji kwa kutumia mianzi, badala ya mabomba ya chuma au plastiki.
Katika utafiti huo mianzi ilitumika kama mambomba ya kusfirishia maji na hata kujenga matangi ya kuhifadhia maji katika maeneo mengi ya Iringa vijijini.
Utafiti wake huo ambao ulibezwa sana hapo mwanzo, lakini marehemu Lipangile hakukata tamaa na baadaye baada ya kukubalika ulikuja kuwaondolea maelfu ya watu wa Iringa shida ya kupata maji safi na salama.
Ubunifu wa mwananchi huyu ulisaidia kuipunguzia serikali gharama kubwa inayotumia kufanikisha huduma ya kuwapatia wananchi maji safi na salama.
Kwa bahati mbaya hii leo, Watanzania wengi hawajui mchango mkubwa uliotolewa na mhandisi huyu katika kuipatia nchi hii maendeleo kama anavyojulikana binti yake Zainab Thabit Lipangile (Zay B au Super girl) ambaye ni msanii na moja ya nyimbo zilizompatia umaarufu dada huyu ni Nipo Gado wakati baba yake kawekwa kando.
Hata Watanzania wanapoadhimisha Siku ya Maji Duniani kila mwaka husikii jina la Thabit Nassor Lipangile kutajwa sio mafanikio yake tu katika sekta ya maji, bali hata kuwa kiumbe huyu wa Iringa.
Mhandisi huyu aliyekufa miaka michache tu iliopita na ambaye ubunifu wake haujafuatiliwa kwa karibu mpaka alipoiaga dunia, hakupewa hata heshima ya kupata tunzo ya taifa kwa utumishi uiliotukuka kama tunavyofanya kwa kuwapa wanasiasa wengi na wasanii, wakiwemo wale ambao badala ya kuhimiza amani huwa wanawachonganisha wananchi.
Hii ndio Tanzania yetu ambayo tunaona kubwa hupuuzwa na kuwa dogo na dogo hukuzwa lionekane kubwa.
Ukichunguza utaona wamejitokeza watu wengi hapa nchini waliofanya ubunifu mkubwa wa kimaendeleo siku za nyuma, lakini ufuatiliaji wa mafanikio waliyoyapata ni sufuri.
Ni vizuri sasa tukabadilika na mafanikio kama ya wasichana hawa wa Zanzibar tukayaendeleza ili hatimaye Watanzania waweze kutumia dawa hii ambayo ina weza kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara ya nzi na mbu na kuacha kutegemea dawa zinazotengenzwa nchi za nje.
Katika nchi nyingi mafanikio kama waliyoyapata hawa wasichana baada ya kujituma sana kwa kufanya utafiti hutumika kuwashajiisha wanafunzi vijana ili nao wajitume zaidi na kujitahidi kuwa wabunifu.
Hivi sasa hapa nchini, Visiwani na Bara, pamekuwepo na uhaba mkubwa katika shule zetu kwa wasichana kupenda masomo ya sayansi kwa vile wanayaona ni magumu sana.
Tunaweza kama panakuwepo mpango ulioandaliwa vizuri, kutumia mafanikio ya wanafunzi hawa wa shule ya Lumumba, kuwachochea wasichana wengine nchini kupenda masomo ya sayansi.
Vyombo vya habari hapa nchini navyo vinaweza kusaidia sana kama vitatangaza zaidi mafanikio ya wasichana hawa wawili wa Zanzibar na wengine waliopata mafanikio kama haya kutoka shule mbali mbali ili jamii ikapata maelezo zaidi.
Kuelezea kwamba palikuwepo kwa mashindano ya wanasayansi vijana hapo Dar es Salam na nani alikuwa mgeni wa heshima haitoshi.
Ni muhimu kutoa maelezo kamili ya mambo yaliokuwepo katika maonyesho hayo, mafanikio yaliyopatikana hapa nchini kwa kufanya mashindano kama haya miaka iliopita na changamoto wanazopambana nazo wanafunzi na walimu wao katika masomo ya sayansi.
Hapo panaweza kuzuka mjadala mrefu wa wanasayansi wazoefu na wachanga na hatimaye pakapatika kitu kitakachosaidi nchi hii kwenda huku tunakosema tunataka kifikia kwa kuwa nchi inayokwenda sambamba na sayansi na teknolojia.
Vyenginevyo kila siku tutaendelea kuimba sayansi na teknolijiana wakati muziki tunaopiga ni tafauti na nyimbo hio.
Kwa upande wake serikali nayo ifikirie upya ni nani hasa wanaofaa kupewa tunzo na kutangazwa kama wananchi waliotoa mchango uliotukuka pale tunapotoa nishani za kitaifa.
Badala ya kushilia  kuwapa nishani hizi za uhuru, Mapiduzi na Muungano wale ambao mchango wao ulikuwa zaidi wa porojo za kisiasa na wengine wakiwa ni watu waliokubuhu kwa kututoa kauli za matusi na kashfa.
Tukiendelea na mwendo huu tuliokuwa nao hivi sasa ni wazi kuwa hiyo safari yetu tunayoipigia debe mara kwa mara kama afanyavyo kondakta wa dala dala ya kuwa nchi inafaidika na maendeleo ya sayansi na teknolojia, itabaki kuwa ndoto.
http://www.freemedia.co.tz/daima/tukuze-sayansi-kwa-vitendo/

No comments :

Post a Comment