Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, October 10, 2014

Wengi waigunia Katiba Mpya


KWA UFUPI
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wasomi, wanaharakati, viongozi wa dini na wanasiasa, walisema Katiba Inayopendekezwa haijamaliza kiu ya wananchi, hususani katika masuala ya utawala na

Dar/Zanzibar. Saa 24 baada ya Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa, makundi mbalimbali ya watu yameonyesha wasiwasi kuhusu hatima ya mchakato huo kwa maelezo kwamba haijabeba maoni ya wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wasomi, wanaharakati, viongozi wa dini na wanasiasa, walisema Katiba Inayopendekezwa haijamaliza kiu ya wananchi, hususani katika masuala ya utawala na muungano, hivyo kuna kila dalili ya kuleta shida siku zijazo.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mohamed Bakari alisema haitawezekana kupata katiba ya wananchi kwa sababu inayopendekezwa ilipitishwa katika mazingira yasiyoridhiwa na wengi, hususan vyama ya siasa.
“Itakuwa ni ya chama kimoja, kiufupi tutapata Katiba ya CCM kwa sababu ndiyo waliolazimisha mchakato,” alisema Dk Bakari.
Alisema CCM inaweza kufanya vyovyote inavyotaka kuipitisha Katiba hiyo bila ya mtu yeyote kuipinga lakini hali hiyo italeta shari siku zijazo hasa wakati wakudai mabadiliko ya katiba hiyo.
Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Patience Mlowe alisema Katiba itakayopatikana itajibu matakwa ya wanasiasa, hususan chama tawala na siyo wananchi.
Alisema mambo mengi yamegeuzwa na kuwekwa ‘kisanii’ huku watu wasiojua wakifurahia, likiwamo suala la uwiano jinsia wa 50 kwa 50 ambalo kwa sasa halitekelezeki tofauti na lilivyokuwa limeelezwa katika Rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alipoulizwa wananchi wanawezaje kupata Katiba yenye masilahi kwao, Mlowe alisema inategemea nguvu ya ushawishi wa upande wa pili wa wanaopinga Katiba Inayopendekezwa kwa kuelimisha wananchi kutoikubali.
Mtaalamu wa Maendeleo na Utawala wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Emmanuel Mallya alisema bado anaamini katiba ya wananchi itapatikana baada ya pande zinazovutana kufanya mazungumzo na kumaliza tofauti zao, hata kama tayari imeshakabidhiwa kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
“Bado tuna nafasi ya kupata Katiba tunayoitaka pamoja na yote hayo yaliyotokea. Katika harakati za kudai masilahi mapana ya Taifa, hakuna kisichowezekana hususan suala la mazungumzo baina ya pande zinazokinzana na kupata maridhiano,” alisema Mallya na kuongeza:
“Watu wajue kura ya maoni siyo kupitisha kila kitu cha viongozi, watu wanaweza kupinga. Hata kama itapitishwa ni lazima kuwe na kipindi cha maridhiano baina ya viongozi juu ya namna ya kuitekeleza hata baada ya kura ya maoni.”
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema kauli za Rais Kikwete zimeacha maswali mengi kwa wananchi... “Rais anatakiwa kutoa msimamo kama mkuu wa nchi lakini ameendelea kubadilika badilika… anaposema sijui tufanye kura ya maoni au mwanasheria aangalie cha kufanya ni mambo yanayowachanganya wananchi.
“Kama NCCR na kama Ukawa tutaendelea kutetea maoni ya wananchi yaliyopuuzwa na muda mwafaka tutawaeleza hatua za kufanya.”
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kazi wanayoifanya sasa ni kuchambua Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na Katiba Inayopendekezwa kisha wataanza kuwaelimisha wananchi.
“Rais Kikwete tayari ameanza kampeni na yeye amepiga kura ya ‘ndiyo’ na sisi hatusubiri muda wa kampeni uanze, tunachambua mchakato mzima kisha tukimaliza tutaanza kuwaelimisha wananchi,” alisema Dk Slaa.
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi alisema viongozi wa dini wanapotoa maoni yao wanakuwa wanatoa kama raia wengine na wasihusishwe na makundi ya vyama vya siasa.
“Ukizungumza ukweli unaambiwa huyu naye askofu ni Ukawa, lakini tunazungumza ukweli, huwezi kuwa na Katiba ambayo haina uhakika na maisha ya watu tangu wanazaliwa hadi wanakua.”
“Wameweka vitu vya kufurahisha watu mfano vya makundi na kuna haki ambazo haziruhusiwi kudaiwa mahakamani sasa kwa hali hii huwezi kukubali kitu ambacho unaona hakitakuwa na tija,” alisema Askofu Niwemugizi
Aliongeza, “Hata nikifa leo hii, kura yangu itakuwa ni hapana kwani huo ni msimamo wangu na si kama askofu, kwani na mimi ni raia kama walivyo raia wengine.”
Katika hatua nyingine, Chadema kimeeleza kushangazwa kwake na hatua ya Rais Kikwete kwa kushindwa kusimamia maazimio yaliyofikiwa baina yake na vyama vya upinzani, likiwamo la kusitishwa kwa kura ya maoni hadi uchaguzi mkuu wa mwakani.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Profesa Abdallah Safari alisema hakutarajia Rais Kikwete kuonyesha nia ya kufanyika kura ya maoni mapema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani, wakati suala hilo walikubaliana lisitishwe.
Profesa Safari aliyeambatana na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Said Issa Mohamed alisema baada ya kuahirisha suala hilo, mambo mengine ya msingi yashughulikiwe likiwamo la kurekebisha sheria za uchaguzi na muundo wa Tume ya Uchaguzi.
Alisema Chadema wamepata taarifa nyeti na wameanza kuzifanyia kazi kwa uchambuzi wa kina kuwa kura ya kupitisha rasimu ya Katiba ilichakachuliwa.
Mohamed alisema wameshangazwa na Rais Kikwete kuanza kampeni mapema kwa kuwataka watu kupiga kura ya ‘ndiyo’ kabla ya muda wa kampeni.
“Tutafanya kampeni kwa Wazanzibari wote kupiga kura ya ‘hapana’, kwanza Katiba Inayopendekezwa inakiuka Katiba ya Zanzibar wakati Zanzibar ina hadhi ya nchi,” alisema.
Alisema ni jambo la kushangaza Serikali ya muungano ilikaa kimya wakati Zanzibar ikifanya marekebisho ya 10 ya Katiba ambayo yalivunja Katiba yake, sasa sisi Wazanzibari hatutokubali,” alisema.
Mwenyekiti wa Wazee Chadema, Hashim Juma alisema Wazanzibari wanataka mamlaka kamili ya nchi yao, kuanzia uraia, kiti chake Umoja wa Mataifa, kuwa na mabalozi wake nje ya nchi, hati ya kusafiria, sarafu yake na hakuna mwafaka zaidi ya kuwa na serikali tatu.
Imeandikwa na Nuzulack Dausen na Ibrahim Yamola (Dar) na Mwinyi Sadallah
.

No comments :

Post a Comment