KAMBI za wasaka urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) zina majina matatu ya Wazanzibari wanaotakiwa kuchukua nafasi ya mgombea mwenza (Makamu wa Rais) kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, imefahamika.
Majina hayo matatu ni Dk. Hussein Mwinyi ambaye ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Samia Suluhu Hassan ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) na Waziri Kiongozi mstaafu na Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha.
Ingawa hakuna sheria inayolazimisha Rais ajaye atoke Bara, kuna kila dalili kwamba Rais ajaye atatoka Tanzania Bara kutokana na aina ya maandalizi yaliyofanywa na watu wanaotajwa kutaka kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Mahojiano mbalimbali yaliyofanywa na Raia Mwema na watu walio katika mchakamchaka wa kuwania kupitishwa na CCM kuwania urais yameonyesha kwamba majina hayo matatu ndiyo yaliyopitishwa na kambi kuu zinazotaka urais.
Gazeti hili limeambiwa kwamba Mwinyi anapendelewa zaidi na kambi inayohusishwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Nahodha akihusishwa na kambi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe huku Samia akihusishwa na ile ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
“Pinda ameshasema tayari kwamba yeye anayemtaka ni Samia. Hapo hakuna ubishi tena. Huyu ni mwanamama anayeijua vema Zanzibar na ana kete ya jinsia. Kwenye hili Pinda hawezi kuyumba tena,” alisema mmoja wa watu wanaohusishwa na kambi ya Pinda.
Alipoulizwa endapo amewahi kufuatwa na mojawapo ya watu wanaotajwa kutaka kuwania urais mwakani ili awe mgombea mwenza, Dk. Mwinyi alisema; “Nikwambie ukweli ndugu yangu, miye sijafuatwa na yeyote katika hao unaowasema.
“Hapa unavyoniona naendelea na kazi zangu za kutumikia taifa na wananchi wangu na sina mawazo yoyote kuhusu 2015. Kama wao wanaona ninafaa ninashukuru lakini kufuatwa bado,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu Mwinyi, Msemaji wa Lowassa, Abubakar Liongo, aliomba apewe muda kumuuliza Waziri Mkuu wa zamani kuhusu taarifa hizo lakini hakuweza kujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Mmoja wa wachambuzi wa siasa za Zanzibar, Ally Saleh, alisema anasikia kuhusu utafutwaji huo wa wagombea wenza kutoka Zanzibar, ingawa alisema Wazanzibari wangependa Rais ajaye atoke Visiwani.
“Miaka hamsini baada ya Muungano, Zanzibar imetawala miaka kumi tu ya Mzee Mwinyi (Ali Hassan, Rais wa Awamu ya Pili). Imefika wakati sasa tuseme Mzanzibari naye anataka nafasi.
“Hivyo la kwanza mimi siungi mkono hili la Wazanzibari kuonekana wanafaa kuwa wagombea wenza tu. Ndiyo maana namuunga mkono Ali Karume anapotangaza kwamba atawania urais ingawa sasa itaonekana kama nchi inakuwa ya Kisultani sasa,” alisema.
Alisema kama angekuwa msaka urais kutoka Bara, angeangalia sifa kuu tatu za mgombea mwenza ambaye angemtaka kutoka Zanzibar; Anayejua siasa za Zanzibar, aliyewahi kufanya kazi Zanzibar na mwenye ufahamu wa mambo ya Muungano na Kimataifa.
Alisema mgombea mwenza anaweza kuja kuwa Rais endapo Rais atakumbwa na tatizo lolote na hivyo naye ni lazima aonekane anaweza kuwa Rais.
Akichambua sifa binafsi na wanasiasa hao watatu alisema; “Samia namfahamu sana. Nimewahi kufanya naye kazi miaka ya nyuma. Ni mtulivu. Hana jazba na amewahi kufanya kazi Zanzibar kama Waziri na anazijua siasa za huko.
“Nafahamu mawaziri wa Bara ambao hawajui hata mikoa ya Zanzibar. Faida ya kupata mgombea anayekubalika Zanzibar ni kwamba utapata pia kura nyingi za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka Zanzibar. Ukipata Makamu anayeijua Zanzibar kindakindaki, maana yake nawe utaifahamu vizuri na atakusaidia kwenye ushauri.
“Kwenye hilo kwa kweli nadhani Samia amepasi vizuri. Tatizo lake ni wizara aliyopewa Bara. Imemfunga sana na Watanzania wamekosa kumjua vizuri uwezo wake.
“Nahodha amewahi kuwa Waziri Kiongozi kwa miaka kumi. Tena alikuwa katika wakati ambapo siasa za Zanzibar zilikuwa ngumu sana kabla ya mwafaka. Ukitaka mtu anayezijua vizuri siasa za visiwani basi Nahodha ameiva.
“Siku hizi amejiongeza kwenye elimu. Anasoma Shahada ya Uzamivu (PhD). Anaifahamu Zanzibar. Muungano anaufahamu na ana uzoefu mzuri wa uongozi katika ngazi za juu.
“Nina shida mbili na Nahodha. Mosi kutokuwa kwake waziri baada ya kuondolewa kumempunguzia nguvu kidogo. Unajua kushindana ushawishi na watu ambao ni mawaziri na wewe sio ni kitu kigumu. Kama bado angekuwa Waziri wa Ulinzi, basi shughuli ingekuwa pevu. Kuwa nje kunaweza kumwathiri.
“Pili haonekani kama mtu anayejitegemea kiuamuzi. Shamsi ni kiongozi ambaye huwezi kukumbuka ni lini alifanya uamuzi mgumu ingawa alikuwa Waziri Kiongozi kwa miaka kumi.
“Mwinyi ni mtulivu na anafanya kazi katika wizara nyeti. Amekuwa waziri mzoefu sasa. Anaufahamu Muungano na ni mtu anayeonekana anaweza kuwa hata Rais wa Tanzania ukiondoa kile ninachokiona kama Usultani wa kutawaliwa na watu wa familia moja.
“Nafikiri tatizo lake kubwa ni ukweli kwamba hajafanya kazi sana Zanzibar. Bado ni mchanga kwenye siasa za Zanzibar na hili linaweza kumsumbua huko mbele ya safari. Lakini ni mtu mzuri,” alisema Saleh ambaye ni mwandishi wa habari na mwanasheria kitaaluma.
Mchambuzi huyo alisema wapo wanasiasa wengine wa Zanzibar wazuri ambao kama angekuwa anataka urais angeweza kuwafikiria kuwa wagombea wenza huku akitoa mfano wa Waziri wa zamani wa Fedha wa Zanzibar, Amina Salum Ally.
Chanzo: Raia Mwema

No comments :
Post a Comment