NA WAANDISHI WETU
Dawa za sangoma kuongeza nguvu za kiume balaa
Watumiaji wadai zinapunguza au kuzimaliza kabisa
Zimo `mkuyati`, `heshima ya ndoa`, `super power`, `jeki`Yale maelezo kuwa supu ya pweza pamoja na dawa za mitishamba zinazotolewa na ‘sangoma’ zinaongeza nguvu za kiume huenda yakawa si kweli baada ya kuwapo taarifa kuwa dawa hizo zinapunguza kama si kumaliza nguvu hizo.
Baadhi ya jamaa na wateja wanaotumia dawa hizo wameliambia gazeti hili kuwa ndugu zao na baadhi yao waliojipiga ‘jeki’ kuongeza nguvu, wameshindwa kufanya tendo la ndoa.
Walisema wakati wengine walivyoanza kuzitumia walipata uwezo wa kindoa, hali ilibadilika na nguvu zilikwisha na sasa wanajuta.
Walidai kuwa waganga wa miti shamba na wapishi wa supu ya pweza wanawahadaa wateja kuwa wana dawa lakini wanachotumia ni kuchanganya dawa zao na ‘viagara’.Walisema kuna baadhi ya hoteli na migahawa inasifika kutengeneza dawa hizo zinazowavuta wateja na kuwalazimisha kufunga safari kwa gharama kwenda kunywa supu hizo, lakini kinachoongezwa ili kusisimua misuli ya viungo vya uzazi ni tiba za kisasa na vingine vyote ni viini macho.
SERIKALI YALALAMIKIWA
Watu hao wanailalamikia serikali hasa mamlaka za usimamizi wa chakula, lishe na dawa kuwa hazitimizi majukumu yake hasa kufuatilia na kukagua dawa zinazodaiwa ni tiba mbadala au za miti shamba na vyakula vinavyotumiwa kama tiba ikiwamo supu ya pweza.
“Tatizo linaanza Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), taasisi ya miti dawa ya Hospitali ya Muhimbili na Shirika la Chakula na Lishe (TFNC).
Je, vyombo hivi vinatembelea migahawa, kununua vyakula ili kuvipima na kuchunguza kiwango cha dawa, tiba inayopatikana kubaini madhara yaliyokuwamo? “ aliuliza mteja aliyeathirika jina linahifadhiwa.
Aliongeza kuwa watendaji kwenye taasisi za umma hawafiki kwa waganga wanaojitangaza kuwa wana dawa, wanasubiri hadi madhara yanapojitokeza na matokeo yake ni kama hili la dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo ni bomu linaloathiri vijana wengi kutokana na kuongeza nguvu kwa kutumia dawa ambazo si tiba.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini waganga hao wanapata pesa nyingi kwani kuna umati wa wateja wanaomiminika kwenye biashara zao wakiwa tayari kuwalipa gharama kubwa ili kupata tiba ya kuongeza nguvu za kiume.
MAJINA YA DAWA ZINAZOTUMIKA
Ziara ya NIPASHE Jumapili, nyumbani kwa waganga hao jijini Dar es Salaam ilikutana na dawa hizo zilizokuwa zimepewa majina kama ‘mkuyati’, ‘heshima ya ndoa’ ‘super power’ ‘jeki’ na ‘mulume power’.
Uchunguzi ulibaini kuwa makundi ambayo ni wateja wakubwa na dawa hizo ni vijana wenye umri kati ya miaka 25 hadi 40 na wengine ni wenye miaka kati ya 45 na 65.
“Dawa hizi zinaokoa ndoa nyingi zisivunjike, zimesaidia kurudisha heshima ya ndoa na uhusiano, vijana wengi wanakuja hapa kununua dawa kwa ajili ya kuimarisha uanamume wao,” alisema mtaalam mmoja anayeendesha shughuli zake Mbagala.
Mganga huyo huuza ‘mulume power’ kwa gharama kati ya shilingi 20,000 na 30,000 kutegemeana na uwezo wao wanaume hao.
Mtaalamu huyu alipohojiwa kama amefanya uchunguzi wa kutambua kama kuna madhara, alitamba kuwa hayapo kutokana na uzoefu alio nao pia hajawahi kupokea malalamiko.
Mganga mwingine anayetoa dawa hizo alisema anatumia mizizi ya mti wa 'mkuyati' ambayo huchemshwa kabla ya kutumiwa na wateja na kwamba gharama yake ni shilingi 10,000 kwa dozi na kwamba mteja anatakiwa kunywa kabla ya kuanza tendo la ndoa.
"Unapoitumia lazima uwe tayari kujamiana, inaleta usumbufu kidogo, ndiyo maana vijana wanapokuja hapa nawaambia wasinywe wakiwa katika shughuli zao, waitumie wakiwa wana wenza na wamejiandaa kufanya hivyo,” alisema.
Lakini waganga hawa wa tiba mbadala wanakanusha kutumia dawa za kisasa ambazo ni pamoja na viagara.
Akizungumzia matumizi ya dawa hizo hasa zilizochanganywa na ‘viagra’, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke Dar es Salaam, Dk. Amaani Malima, alisema ni kosa kuwapa watu dawa bila kufuata maelezo ya kitaalamu.
Alisema ni kinyume cha sheria za tiba kutoa dawa kwa mgonjwa ambaye hujui chanzo cha tatizo lake, mathalani kama hana nguvu za kujamiiana ilitakiwa kwanza achunguzwe ifahamike ana tatizo lipi, na tiba yake ni nini siyo kukimbilia ‘viagra’.
Aliwaonya waganga hao kuwa ‘viagra’ ina athari kubwa kwa wenye matatizo ya presha hasa ya juu na kisukari kwani ina sisimua misuli na kupandisha zaidi presha hivyo inapotumiwa inaweza kusababisha kifo.
“Dawa hizo zinatakiwa kutolewa kwa dozi siyo kuchanganya kidonge kwenye supu au kwenye dawa za mizizi, mambo haya yanaweza kuathiri zaidi watumiaji,” alionya na kuongeza kuwa athari mbaya kama kuongeza tatizo la moyo na presha ya juu ni mambo yanayotarajiwa iwapo wagonjwa watakunywa dawa bila utaalamu na kuchunguzwa.
Dk. Malima alisema wenye tatizo hilo waanzie hospitalini kuchunguzwa kwanza kabla ya kikimbilia kwa waganga ambao pengine hawafahamu kwa undani matatizo yao kwani uchunguzi na vipimo vya kitaalamu ndiyo unaeleza ni dawa gani mtu anastahili kupewa.
MAELEZO YA SERIKALI
Waziri wa afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, akizungumzia dawa hizo, alisema ni kosa kwa mtu kuchanganya dawa za miti shamba na za viwandani na kuonya kuwa atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema sheria ya matumizi tiba mbadala na asili inaeleza kwamba ni kinyume kufanya jambo hilo.
“Itakuwa wanafanya makosa kama mtu atachukua miti, majani au mizizi na kuchanganya dawa ya unga iliyotengenezwa kiwandani kwa sababu inaleta athari kwa watumiaji, “ alionya Dk. Rashid.
Alisema ni hatari kwa vile kitendo hicho kitasababisha mtumiaji kutumia dawa ambayo ina kiwango kikubwa au chini ya dawa kinachohitajika.
“Mtu anatakiwa kutumia dawa kutokana na kipimo sahihi, katika mchanganyiko wa aina hiyo mgonjwa atajikuta anatumia dawa kwa wingi au ‘over dose’ au kiwango cha chini ‘under dose’ na kujiweka kwenye hatari zaidi,”alisema.
Aliongeza kuwa katika utaratibu wa tiba, lazima kuwapo kwa malezo sahihi ya matumizi ya dawa na endapo mtu hajui kitu gani anachotumia anahatarisha afya yake.
Alieleza moja ya athari za matumizi ya dawa ya kuongeza nguvu za kiume kuwa ni pamoja na matatizo ya moyo kwenda kasi na kuhatarisha maisha.
Hata hivyo, Waziri huyo alikiri kuwa ni vigumu kupiga marufuku tiba za asili kutokana na jamii kujenga imani na matumizi ya dawa hizo na huku wengi wakiamini kuwa zinawaletea nafuu.
Alisema serikali inachofanya ni kuwapatia uwezo watu wanaojihusisha na tiba hizo ikiwa pamoja na kuwajengea kiwanda Dar es Salaam kwa ajili ya kusindika dawa hizo ziweze kuwa na ubora na viwango vinavyokubalika.
Aidha hatua nyingine zinazochukuliwa ni kuwaelemisha kutumia vitengo vya utafiti vilivyopo hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wizarani hapo kwa ajili ya kuchunguza dawa zao kama ni salama kwa matumizi ya tiba.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment