Nchemba alitoa wito huo jana wakati akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Kituo cha Redio One nchini.
“Kuficha fedha nje ni uhujumu uchumi kwani fedha yeyote iliyofichwa nje ni lazima itakuwa imepatikana kwa njia zisizokuwa halali na mtu wa namna hiyo anatakiwa fedha zake zitaifishwe zisaidie katika maendeleo na kusomesha yatima,”alisema.
Alisema takwimu zinaoonyesha kuwa fedha zinazoombwa katika mataifa yaliyoendelea duniani zinazotoroshwa na kufichwa nje kutokana na rushwa au matumizi mabaya ya madaraka hali inayodidimiza maendeleo ya nchi.Alisema serikali ilishaanza kuchukua hatua kwa kushirikiana na vyombo vya nje kuchunguza watu walioficha fedha nje ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
“Tuna chombo kinachojulikana kama Financial Intelligence Unit (Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu), ambacho kinashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya usalama kudhibiti masuala kama hayo,”alisema.
Aliyataka mataifa makubwa yasisubiri tu kufuatilia fedha za misaada yanayotoa katika nchi za Afrika badala yake yasaidie kuchunguza ili kuunga mkono nchi zinazoendelea kukabiliana na watu wanaoficha fedha nje.
“Kama mtu amewekeza fedha katika ujenzi wa kiwanda kwa mfano katika nchi za Zambia, DRC Congo au Malawi na fedha ya uwekezaji huo anaziweka katika benki ya nchi husika hilo ni jambo jema lakini kutorosha fedha nje kwa maana ya rushwa au matumizi mabaya ya madaraka hilo lina hasara kwa taifa, ”alisema.
Hivi karibuni ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ), ulifichua kuna Watanzania 99 wenye akaunti za siri nchini Uswisi zenye mabilioni ya fedha.
Taarifa ya Swiss Leaks ilionyesha kuwa Watanzania hao, wakiwamo wanasisa na maofisa wa juu wa serikali, wana akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni 114, ambazo ni sawa na Sh. bilioni 199.6.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania iko nafasi ya 100 kati ya nchi zenye kiasi kikubwa cha fedha kwenye akaunti za siri nchini humo.
Msingi wa ripoti hiyo ulitokana na aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya kimataifa HSBC, Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya kuacha kazi.
Mwaka 2008, alivujisha siri za akaunti za siri za baadhi ya watumishi wa umma na wanasiasa wa Ufaransa ambazo mamlaka za kodi nchini humo ilizifanyia uchunguzi kuthibitisha.
HSBC ni benki kubwa ya biashara duniani ambayo ilianzishwa mwaka 1836. Kwa mujibu wa Swiss Leaks, matokeo ya uchunguzi huo yanatokana na aina tatu za taarifa ndani ya benki kwa vipindi tofauti.
Mosi ni taarifa za wateja na uhusiano wao na akaunti za benki nchini Uswisi kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1988 hadi 2007.
Pili, ni picha kamili ya kiasi cha juu cha fedha kilichokuwapo kwenye akaunti ya mteja katika kipindi cha mwaka 2006 na 2007 na tatu, ni mawasiliano kati ya mteja husika na wafanyakazi wa benki katika kipindi cha mwaka 2005.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa taarifa za kiuchunguzi kutoka kwenye benki nchini humo zinaonyesha kuwa akaunti hizo zinahusishwa na baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na watumishi wa umma ambao wamejipatia utajiri wa siri unaotokana na kuanzishwa kwa kampuni hewa.
Hata hivyo, ICIJ haikutaja majina ya Watanzania wenye akaunti hizo, bali wanaeleza kuwa baadhi ya wateja wanaweza kuwa na akaunti nyingine zaidi nje ya Uswisi au kwenye nchi mbalimbali duniani.
Mwaka jana Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alikaririwa akisema kuwa wapo watu waliopata fedha kihalali, lakini wanazificha na mali zao nje ya nchi ili kukwepa kodi na kwamba, wengi wao ni wafanyabiashara wakubwa.
Zitto alisema vilevile Tanzania imepoteza dola bilioni 1.25 za Marekani kati ya mwaka 2001 na 2012 kwa njia hiyo ya kuwapo kwa Watanzania wanaoficha fedha zao Uswis.
Kufuatia hoja hiyo ya Zitto, Serikali iliunda timu kutokana na Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka juzi ambayo ilikuwa inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Frederick Werema.
Viongozi wengine wanaounda tume hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment