dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, February 27, 2015

Tibaijuka ala kibano, bado Ngeleja.

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka.
Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka, alikumbana na ‘kibano’ mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma baada ya kusomewa mashtaka matatu na baraza hilo, likiwamo la kuomba fedha katika Kampuni ya VIP Consultant, inayomilikiwa na James Rugemalira, kinyume cha maadili ya viongozi wa umma.
 
Mashtaka mengine yanayomkabili Prof. Tibaijuka, ambaye alivuliwa Uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Rais Jakaya Kikwete kutokana na kupokea Sh bilioni 1.6, ni kupokea fadhila pamoja na kuingia katika mgongano wa kimaslahi.
 
Prof. Tibaijuka, ambaye aliongozana na Wakili wake, Dk. Rugemaleza Ishara, alikana mashtaka hayo na kusema fedha alizopewa zilikuwa ni za shule na hakuwa na maslahi binafsi.
 
Ishara alisema hakuna sheria yeyote inayomkataza mtu au kiongozi wa umma kujiunga au kushiriki katika taasisi, kupokea zawadi au msaada.Alisema alichokifanya Prof. Tibaijuka ni kuchukua fedha hizo kwa ajili ya kusaidia shule, ambayo yeye ni mlezi siyo kwa maslahi yake binafsi.
 
Ishara alisema yeye kama mwananchi na mwanzilishi wa shule hiyo hakuomba fedha hizo kutoka kwa Rugemalira kutokana na wadhifa aliokuwa nao, bali aliomba kama kiongozi wa shule.
 
Shahidi wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambaye alishiriki katika uchunguzi  wa sakata hilo, Waziri Yahaya, alisema tume ilibaini kwamba, Tibaijuka alikiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
 
Alisema sheria hiyo inakataza kiongozi wa umma kujipatia fedha kwa maslahi ya kiuchumi au kumsaidia mtu mwingine kupata manufaa ya kifedha.
 
Yahya alisema tume ilibaini kwamba Prof. Tibaijuka alipokea Sh. bilioni 1.617 kutoka kwa VIP Februari 2, mwaka jana, ambazo ziliingizwa katika akaunti binafsi ya Prof. Tibaijuka kupitia Benki ya Mkombozi, iliyopo Tawi la Mtakatifu Joseph, jijini Dar es Salaam.
Pia alisema tume ilibaini kuwa Prof. Tibaijuka ni mmoja wa wadhamini wa Shule ya Babro Johnson.
 
Mahojiano hayo, ambayo yalichukua zaidi ya saa nane, yalitawaliwa na maswali makuu manne kutoka kwa wanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
 
Mojawapo ya maswali yaliyoulizwa ni pamoja na sababu za yeye kupokea fedha, ambazo ni za shule, kuwekwa katika akaunti yake.
 
La pili, endapo Prof. Tibaijuka hakuwa na maslahi binafsi iweje asimamie mchakato wa kupata fedha kwa ajili ya kusaidia shule hiyo, badala ya kuiachia bodi ya shule.
 
Tatu, kwa nini fedha hizo zitolewe kwa masharti kutoka kwa mtoaji msaada (Rugemalira) kama haikuwa na maslahi binafsi.
Akijibu maswali hayo, Prof. Tibaijuka alisema fedha alizoomba ni msaada, hivyo asingeweza kutoa masharti kwa jambo, ambalo na yeye anasaidiwa.
 
Prof. Tibaijuka alisema anashangaa kufikishwa alikofikishwa kwa kuwa lengo lake lilikuwa ni kuwasaidia wasichana wenye vipaji wasio na uwezo wa kifedha na ni mradi, ambao ulilenga kujenga shule katika kila kanda nchini.
 
Alisema Babro Johns Foundation ni taasisi iliyolenga kuleta maendeleo kwa watoto wa kike, ambayo tangu mwaka 2010 hadi 2012 ulikuwa unafadhiliwa na watu wa Sweden, ambao baada ya kumaliza mkataba wao, walianza kufanya michakato ya kushawishi ufadhili kwa watu wa ndani na nje.
 
Alisema serikali pia imekuwa ikiisaidia taasisi hiyo na kwamba wakati inaanza serikali ya awamu ya tatu ilitoa eneo kwa ajili wa shule hiyo pamoja na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuchangia Sh. 500,000.
 
Prof. Tibaijuka alisema yeye ni mwanamke mwanaharakati, ambaye amekuwa akitetea  maendeleo ya wanawake na wasichana tangu alipokuwa akifanya kazi katika Umoja wa Mataifa (UN) na hata Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja huo, Koffi Annan alimruhusu kufanya hivyo.
 
“Mimi ni mwanaharakati wa muda mrefu, ambaye hata wakati nikiwa nafanya kazi Umoja wa Mataifa nilikuwa napigania maendeleo ya watoto wa kike, hata Katibu Mkuu alikuwa aliniruhusu na kunipongeza kufanya hivyo, ninashangaa leo hii pamoja na juhudi zangu hizi, nimedhalilishwa na kuitwa mwizi,” alisema Prof. Tibaikuka.  
 
Aliongeza: “Mimi ni Profesa wa Uchumi, ninafahamu mbinu nyingi za kuchakarika kupata fedha na hata misaada ya wafadhili ilipoisha nilichakarika kutafuta fedha kwa ajili ya watoto wa taifa hili, ambao ni kwa manufaa ya taifa hili. Eti leo hii nimefikishwa hapa.  Nijajua kwamba, ukweli utajulikana tu japo ni mrefu.”
 
“Nimetumia nafasi hii kwa kuwa sikupewa nafasi ya kusikilizwa, kujieleza ili msikie ukweli. Wamesema nimekiuka maadili, ninakataa na nitaendelea kukataa kwa sababu sioni kosa mimi kuchakarika kwa ajili ya maendeleo ya taifa. Na kama ndiyo hivi, basi sijui nchi hii itakokwenda.”
 
Alisema hata kama anadhalilishwa namna hiyo, bado yeye ni Mtanzania, hataenda popote, badala yake, ataendelea kupambana kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
 
“Mimi ni Mtanzania japo ninadhalilishwa kwenye nchi yangu na hata mataifa mengine yanaona ninavyodhalilishwa. Ambao waliniamini na walinidhamini, lakini nitaendelea kupambana kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Siondoki, tutabanana hapa hapa,” alisema.
 
Naye Shahidi wa Prof. Tibaijuka, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hiyo, Balozi Paul Rupia, alisema fedha hizo zilitafutwa na Profesa Tibaijuka na zilitolewa  taarifa kwenye bodi hiyo kuwa kuna fedha zimeingia, ambazo zilitakiwa kulipwa madeni.
 
Alisema bodi hiyo haijampa masharti yoyote ya kumaliza kulipa madeni hayo na kwamba hawakuwa na sababu ya kumfuatilia kwa sababu walimuamini kutokana na juhudi zake binafsi za kupata fedha hizo.
 
Shauri hilo lililoanza saa 3.00 asubuhi, liliendelea hadi saa 11.45 jioni.
 
Katika mjadala huo, Prof. Tibaijuka alitoa ushahidi kwa zaidi ya saa tatu, kuanzia saa 6.30 mchana hadi saa 9.30 alasiri.
 
Shauri hilo limeahirishwa hadi Machi 13, mwaka huu, baada ya Wakili wa Prof. Tibaijuka kuomba udhuru wa kwenda nchini Marekani kwa siku 10.
 
Jaji Msumi alikubali ombi hilo na kusema shauri hilo litaendelea siku hiyo na kutolewa uamuzi  huku baraza hilo likiamua namna ya kujadili shauri hilo litaamuliwa kama liwe la uamuzi wa ndani au hadharani.
 
Ndugu, marafiki, wakiwamo baadhi ya wafanyakazi, walifurika katika ukumbi wa Karimjee, ambako baraza hilo linasikiliza shauri hilo.
 
Siku hiyo pia itakuwa zamu ya Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja (pichani), kuhojiwa na baraza hilo kwa tuhuma za kupokea mgao wa Sh. milioni 40 za Escrow. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment