
Uongozi wa Chama cha ACT-Tanzania, umesema ni wakati mwafaka kwa Zitto Kabwe kujiunga nao.
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa ACT, Samson Mwigamba, alisema Zitto amekuwa msikivu kwa washauri wake na amefanya jambo la kishujaa kwa kuwa hawezi kuendelea kuwa ndani ya kundi la watu aliodai wasio wazalendo na wasiopigania maslahi ya wengi bali ya wachache.
“Tunamtaka asiache siasa bali atangaze kujiunga na ACT-Tanzania, ndicho chama sahihi kwake,” alisisitiza Mwigamba mara baada ya kupata taarifa za Zitto kutangaza kuachia Ubunge.
Awali, Mwigamba aliliambia NIPASHE kuwa mara kwa mara wamemuomba Zitto kujiunga na chama hicho na kwamba amewaomba wampe muda afikirie zaidi.“Tulikuwa naye Chadema, sisi hatukuwa na cha kupoteza ndiyo maana tulikubali kufukuzwa, lakini Zitto alilazimika kwenda mahakamani ili kulinda ubunge wake, sasa wamemfukuza nafikiri ni wakati mwafaka wa kijiunga na ACT kwa kuwa hakuna chama kingine kinachomfaa,” alisema na kuongeza:
“Zitto anabeba maono yanayoendana na ACT, tangu tukiwa Chadema mimi, Prof. Kitila Mkumbo na Zitto, tulikuwa na maono yanayofanana ya kukibadili Chadema kujiendesha kisayansi zaidi kwa kufanya mabadiliko ambayo Zitto angekuwa Mwenyekiti Taifa, baada ya kutoka tumeyaendeleza na wengine wengi na sasa ni wakati wake kuungana nasi.”
Alisema hali ilivyo sasa hakuna uwezekano wa Chadema kuwa na mahusiano mema na Zitto na kwamba hawaoni chama kinachomfaa zaidi ya ACT-Tanzania.
“Tumemshauri asikate rufaa, bali aje tuungane pamoja katika kujenga ACT ambayo ndiyo mbadala wa vyama vingine kwa kuwa kinaendeshwa kwa demokrasia na msingi thabiti,” alisema.
Aliongeza kuwa Katiba ya ACT inaeleza kuwa mwanachama atashika nafasi ya uongozi kwa vipindi viwili pekee.
Alisema chama hicho kinatarajia kusimamisha mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na wabunge kwa kuwa kwa sasa ni chama cha 22 kwa kusajiliwa, lakini ni chama cha tano kwa kukubalika kwa Watanzania na wanahitaji kushika nafasi ya kwanza.
Alisema atakayechaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa ACT, kama atatimiza sifa zinazotakiwa atagombea urais kwa tiketi ya chama hicho.
UCHAGUZI
Mwigamba alisema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi za uongozi wa taifa ndani ya ACT- Tanzania, unaendelea huku nafasi ya kiongozi mkuu wa chama ikiwa wazi hadi sasa.
Uchaguzi ndani ya chama hicho utafanyika Machi 28, mwaka huu, na kufuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu utakaofanyika Machi 29, mwaka huu.
Nafasi zinazowaniwa ni Kiongozi Mkuu, Mwenyekiti wa Taifa, Makamu wenyeviti wa taifa bara na visiwani na wajumbe wa Halmashauri Kuu.
Mwigamba alisema Mkutano Mkuu utakuwa na ajenda tatu ambazo ni taarifa ya shughuli za chama tangu kianzishwe Mei 5, mwaka jana, marekebisho na kupitisha Katiba mpya ya chama, uchaguzi wa viongozi wa kitaifa.
Aliwataja wanachama waliochukua fomu na nafasi wanazogombea kuwa ni Estomih Mala na Anna Mghwira (Mwenyekiti), yeye Mwigamba atagombea ukatibu, huku wengine wakiomba kugombea ujumbe wa Kamati Kuu ambao ni Ramadhani Kasisiko, Abibu Mchange na Wilfred Kitundu.
Alisema uchaguzi huo utasimamiwa na kamati ya uchaguzi taifa yenye wajumbe watano chini ya wamasheria wa chama, Thomas Matatizo.
VIGOGO ZAIDI KUJIUNGA ACT
Mwigamba alisema vigogo mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara na wabunge wanatarajia kujiunga na chama hicho na kwamba kwa sasa hawajitokezi hadharani kwa kuhofia kupoteza nafasi za uongozi walizonazo.
Alisema ACT itasimamisha wagombea ubunge kwenye majimbo mbalimbali nchini na kwa sasa wanajipanga.
MWANAWE NKRUMAH KUWA MGENI RASMI
Alisema mtoto wa rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, Samia Nkruma, ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa chama cha CPP Ghana na Mbunge mstaafu, atakuwa mgeni rasmi.
Alisema kwa sasa wanawasiliana na Jaji Mark Bomani na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Bukuku, ili mmoja wao awe mgeni rasmi kwa upande wa Tanzania.
Alisema uzinduzi huo utafanyika Diamond Jubilee, Machi 29, mwaka huu na kuhudhuriwa na zaidi ya watu 1,000.
Alisema Katibu Mkuu wa ODM –Kenya, amethibitisha kuhudhuria na kuwa Msajili wa Vyama vya siasa nchini, viongozi wa vyama vya siasa, wabunge, mawaziri, wanafunzi wa vyuo vikuu na viongozi mbalimbali wa serikali pia watahudhuria.
Alisema katika uzinduzi huo, Kiongozi Mkuu wa chama ataeleza mwelekeo wa chama hicho, uzinduzi wa tovuti ya chama na ilani ya mwaka 2015, ufafanuzi wa Katiba na kutangaza rasmi kanuni na maadili kwa viongozi.
“Pia tutazindua upya Azimio la Arusha kwa kuchukua yote yaliyopo kwenye azimio hilo na kuyafanya yaendane na mazingira ya sasa ili kuweka miiko ya viongozi,” alifafanua Mwigamba.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment