Written by Ghalib of Mzalendo.net
- Mwito wa wananchi wa Bahrain kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Katika upande mwingine, Yusuf Rabei, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain amewaambia waandishi wa habari kuwa inasikitisha kuona kwamba mamluki kutoka nje wanafanya jinai dhidi ya wafungwa wa kisiasa katika jela ya Jow, nchini Bahrain.
Hivi karibuni, askari wa utawala wa ukoo wa Aal Khalifa waliivamia jela ya Jow mjini Manama na kuwashambulia wafungwa wa kisiasa na hadi hivi sasa hakuna taarifa za kina zilizotolewa kuhusu hatima ya wafungwa hao.
Said Shahabi, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Bahrain aliyeko mjini London Uingereza amesema kuwa, maelfu ya familia za wafungwa wa kisiasa wa Bahrain wameliomba Shirika la Msalaba Mwekundu kuwaokoa jamaa zao kutokana na mateso ya kutisha wanayofanyiwa kwenye jela za Bahrain.
Nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi iliingia kwenye maandamano ya wananchi tangu tarehe 14 Februari 2011, wakati wananchi wa nchi hiyo walipomiminika mitaani kupinga utawala wa kiimla na kidikteta wa ukoo wa kifalme wa Aal Khalifa.
Wanachotaka wananchi wa Bahrain ni haki zao za kimsingi, kama vile kujiamulia wenyewe mustakbali wa nchi yao na wanapinga kuhodhiwa kila kitu na watu wa ukoo wa kifalme. Hata hivyo badala ya kusikiliza vilio hivyo vya wananchi, utawala wa Aal Khalifa unazidi kuwakandamiza wananchi hao.
Ripoti zinaonesha kuwa, idadi ya wafungwa wa kisiasa wanaokufa kutokana na mateso inaongezeka siku hadi siku nchini Bahrain. Mateso wanayofanyiwa wafungwa hao ni makubwa kiasi kwamba hata tume na taasisi zenye mfungamano na utawala wa Aal Khalifa zimelazimika kukiri kuweko mateso hayo.
Hivi karibuni, kamati ya kutafuta ukweli iliyoundwa na mfalme wa Bahrain kutokana na mashanikizo makubwa, imelazimika kukiri kuwepo mateso hayo kutokana na ushahidi mwingi uliopo wa kuthibitisha jambo hilo. Kurundikana wafungwa kwenye jela za Bahrain, kupindukia uwezo wa jela hizo, ni ushahidi kuwa, mgogoro wa nchi hiyo ni mkubwa mno.
Wapinzani wa serikali ya Bahrain wanasema kuwa kuna karibu wafungwa 10,000 wa kisiasa nchini humo.
Taasisi mbalimbali za haki za binadamu zikiwemo za kimataifa zimekuwa zikisema katika ripoti zao kuwa, kwa kuzingatia idadi ya wananchi wa Bahrain, utawala wa ukoo wa kifalme wa Aal Khalifa ni miongoni mwa tawala ambazo zina wafungwa wengi zaidi wa kisiasa.
Mashirika hayo pia yanasema kuwa, rekodi za haki za binadamu za utawala wa Bahran, ni miongoni mwa rekodi mbaya mno za haki za binadamu, ulimwenguni.


No comments :
Post a Comment