dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, April 27, 2015

Kikwete aaga.

  Akagua gwaride la mwisho la majeshi sherehe za Muungano, Asamehe wafungwa 4,129, kwa mara ya mwisho.

Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, akikagua gwaride la heshima la vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama, wakati wa maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Picha: Khalfan Said.
Rais Jakaya Kikwete, jana alikagua gwaride la mwisho la maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Sherehe hizo zilifanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa serikali, vyama vya siasa, asasi na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
 
Hilo ni gwaride la mwisho kwa Rais Kikwete kulikagua wakati akisubiri kumaliza muda wake wa uongozi wa miaka 10 kwa mujibu wa Katiba ya nchi. 
 
Ataondoka madarakani Novemba, mwaka huu baada ya kuapishwa Rais mpya atakayepatikana katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.Jana Rais Kikwete alikagua gwaride la 10 la Muungano tangu alipoingia madarakani Desemba 30, mwaka 2005, kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Benjamin Mkapa.
 
Alikagua gwaride la Muungano kwa mara ya kwanza Aprili 26 mwaka 2006 la pili Aprili 26 mwaka 2007, la tatu Aprili 26, 2008, la nne Aprili 26, 2008, la tano Aprili 26, 2010, la sita Aprili 26, 2011, la saba Aprili 26, 2012, la nane Aprili 26,2013, la tisa Aprili 26, 2014 na la 10 jana.
 
Kabla ya kukagua gwaride la mwisho jana ikiwa ni ishara ya kuanza kuaga, Rais Kikwete alikamilisha kukagua gwaride la maadhimisho ya miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, mwaka jana ikiwa na maana kwamba Desemba 9, mwaka huu gwaride la maadhimisho ya miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika litakaguliwa na rais atakayechaguliwa Oktoba.
 
Rais Kikwete alikagua gwaride tisa la kuadhimisha Uhuru wa Tanganyika kuanzia Desemba 9, 2006 hadi Desemba 9, 2014.
Siku nyingine za maadhimisho ya kitaifa ambazo vikosi vya ulinzi na usalama huandaa gwaride ni maadhimisho ya siku ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambalo hukaguliwa na Rais wa Zanzibar.  
 
MAADHIMISHO YA JANA
Sherehe za jana zilipambwa na gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo vilipita mbele ya jukwaa kuu kwa mwendo wa pole na haraka, halaiki ya wanafunzi iliyoonyesha maumbo mbalimbali, kwaya na ngoma za asili kutoka pande zote za Muungano.
 
Rais Kikwete aliingia uwanjani saa 4:48 na kuzunguka uwanja kwa gari ya wazi, kukagua gwaride, gwaride kutoa heshima na utii kwa Rais na baadaye kupita kwa mwendo wa pole na haraka na vikosi vya makomandoo.
 
Aidha, halaiki ya wanafunzi ilipambwa na utengenezaji wa maumbo mbalimbali na wengine wakionyesha umbo picha linaloonyesha maneno na masuala mbalimbali ikiwamo ujasiariamali na kupinga mauaji dhidi ya albino na ujangili wa wanyamapori.
 
Pia, ngoma za asili za limbonde, msewe, egumba, kiumbizi na ya Wamakua na vikosi vya ulinzi na usalama vya wanafunzi vikiambatana na makomandoo waliofurahisha umati wa watu waliohudhuria sherehe hizo kwa jinsi walivyomudu kuonyesha ukakamavu.
 
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa ni `Amani na Umoja, ipigie kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa na kushiriki uchaguzi mkuu.'
 
VIONGOZI WALIOHUDHURIA
Viongozi waliohudhuria mbali na Rais Kikwete ni Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal; Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda;  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
 
Wengine ni Jaji Mkuu Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu; Rais mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume; Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho; Naibu Spika, Job Ndugai; Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
 
Wamo pia Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Philip Mangula; Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa; mabalozi na mawaziri.
 
Viongozi ambao hawakuhudhuria maadhimisho hayo ni Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassani Mwinyi; Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa, Cleopa Msuya, John Malecela, Dk. Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba; Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda.
 
WAUELEZEA MUUNGANO
Baadhi ya viongozi walioshiriki maadhimisho hayo walizungumza na waandishi wa habari kuhusu muungano huo.
 
Spika mstaafu, Msekwa, alisema Muungano wa nchi nyingi ulivunjika muda mfupi baada ya kuungana, lakini wa Tanzania upo hadi sasa licha ya kupita katika changamoto mbalimbali na kwamba vijana ndiyo wa kuuendeleza na kufika miaka 100.
 
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema Muungano umelifanya taifa kubaki moja lenye umoja na kuheshimiana.
 
RAIS ASAMEHE  WAFUNGWA 4,129
Wakati huo huo, Rais Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,129 kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Kati ya hao, wafungwa 400 wataachiwa huru na 3,729 watapunguziwa vifungo vyao na kuendelea kubaki gerezani kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
 
Msamaha huo umetolewa kwa kutumia madaraka aliyopewa Rais chini ya Ibara ya 45 (1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak Abdulwakil, wafungwa wote watapunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu cha 49 (1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika ibara ya 2 (i-xix). Taarifa hiyo imeeleza kwamba msamaha huo unawahusu  wafungwa wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu na saratani ambao wako kwenye hali mbaya, wazee wenye umri wa miaka (70) au zaidi na wenye ulemavu wa mwili na akili wathibitishwe na jopo la waganga chini ya Mganga Mkuu wa Mkoa/Wilaya.
 
Wengine ni wafungwa wanawake walioingia na mimba gerezani pamoja na walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya. Hata hivyo, msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa ya kifungo cha maisha au kifungo gerezani, kifungo cha maisha, usafirishaji au matumizi ya dawa za kulevya aina ya cocaine, heroin na bangi.
 
Kadhalika, wafungwa wa wanaotumikia adhabu ya makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo, kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali, shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.
 
Wafungwa wengine ambao msamaha huo hautawahusu ni waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha makosa ya kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi/sekondari waliotenda makosa hayo wakiwa na miaka (18) na kuendelea. Pia hautawahusu wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari, pikipiki, matumizi mabaya ya madaraka, waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa rais na bado wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo chao, waliozuia watoto kupata masomo, kutekanyara watoto na biashara ya binadamu.
 
Wamo pia wa kukutwa na viungo vya binadamu na ukatili dhidi ya albino, usafirishaji nyara za serikali na ujangili, ubadhirifu wa fedha za serikali, kutoroka na kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment