dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, April 27, 2015

Tuenzi Muungano kwa kudumisha amani

BY MHARIRI

26th April 2015
Print
Maoni ya Katuni
Amani ya nchi yetu ni moja ya tunu tunayopasa kujivunia Watanzania. Muungano wetu leo umetimiza miaka 51 tangu waasisi wetu, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume  (kwa sasa wote ni marehemu), walipoziunganisha nchi zetu mbili za Jamhuri ya Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Muungano huo, hakika umedumu kwa miaka yote hiyo kutokana na misingi imara iliyowekwa na waasisi wetu tangu walipofikia maamuzi ya  kuziunganisha nchi zetu hizi mbili.

Na katika kipindi chote hiki, zipo changamoto mbalimbali ambazo pande hizi mbili zimepitia hasa zilzizohusu kero za muungano, lakini kutokana na busara na hekima za viongozi wetu, zimeweza kutatulia hatua kwa hatua na kwa njia ya maridhiano ya amani.

Kwa mfano, Aprili 7, 1972, siku aliyouawa Sheikh Abeid Amani Karume , mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba yalikuwa 11, lakini yalifanyika marekebisho baadaye na hadi Mwalimu Nyerere anaondoka madarakani mwaka 1985, yalikuwa  yamefika 21 kwa mujibu wa Katiba.

Mwaka 1994 kulipozuka kundi la G-55 ndani ya Bunge la Muungano likidai Serikali ya Tanganyika, baada ya Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), Rais Ali Hassan Mwinyi (kwa wakati huo) aliunda tume iliyoongozwa na William Shelukindo kuchunguza kero za Muungano.

Ndipo Tume ya Shelukindo ilibaini kero 31 ambazo zilishughulikiwa. Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani zilikuwa zimebaki kero 13 na ameshughulikia tisa, zimebaki nne na tatu kati ya hizo zinahitaji marekebisho ya Katiba.

Mchakato wote huo umewezekana kwa amani kutokana na jinsi viongozi wetu na Watanzania  wanavyopenda mambo yafanyike kwa umakini kwa mustakabali wa Taifa letu.

Tunayo imani kubwa sana na serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jinsi ambavyo imeweza kusimamia mchakato wote wa muungano tangu kuasisiwa kwake na waasisi wetu.

Imefanya kazi kubwa na nzuri katika kuhakikisha Muungano unadumishwa kwa amani miaka yote hii 51na pia kushughulikia kero zinazojitokeza ambapo hivi sasa tumejielekeza katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ambapo tayari ipo katiba pendekezwa ikisubiri maoni ya wananchi.

Kusema ukweli lengo kuu la waasisi wa muungano mwaka 1964 lilikuwa kuwaweka karibu wananchi wa pande hizo mbili kwa lengo la  kujenga nguvu ya pamoja kwa ustawi wa nchi. Na ukaribu huo, ulijikita katika msingi wa kudumisha amani ya nchi na watu wake.

Ndiyo maana leo hii tunajivunia amani na utulivu, tunu ambazo zimetokana na mafanikio ya Muungano. Bila amani mafanikio haya yasingeonekana jinsi yalivyo. Huu ndiyo ukweli usiopingika kwa yeyote anayelipenda taifa letu hili la Tanzania.

Nchi nyingi duniani zinakabiliwa na vurugu na hiyo inatokana na kutojali uwepo wa amani. Nyingi zimejikuta katika mazingira hayo ya vurugu kutokana na chimbuko la taifa kughubikwa na vurugu ikiwamo zinazotokana na ung’anganizi wa madaraka, vita vya kidini na kadhalika.

Zingine ni tajiri wa maliasili ikiwamo madini na mafuta lakini utajiri huo hauwasaidii kutokana na baadhi miongoni mwao kutawaliwa na tamaa na ubinafsi usiojalimaendeleo ya wananchi walio wengi.

Ni suala lisilopingika kwamba kila jambo lina changamoto zake na sisi tunaamini mjadala unaondelea kuhusu upi ni muundo sahihi wa Muungano ni changamoto ambazo utafika wakati zitakwisha na hatimaye Watanzania watapata kile walichokikusudia.

Wakati tunaadhimisha kumbukumbu sherehe za Muungano, ni muhimu sana suala la amani ya nchi kuhubiriwa kwa nguvu kubwa. Viongozi wa dini na wanasiasa wanaopaswa kushikilia bango dhana hii kuwakumbusha na kuwasisitizia wananchi manufaa ya kudumisha amani tuliyo nayo nchini.

Viongozi wa kisiasa na wale wa dini badala ya kutupiana vijembe wenyewe kwa wenyewe, wajikite zaidi kuhimiza amani ya nchi ili hata ratiba za kitaifa zilizopo mbele yetu, ukiwamo uchaguzi mkuu mwaka huu zifanyika katika misingi ya utulivu na amani.  Kama hakuna amani, hata maeneo wanayoongoza yatakuwa hayana maana yoyote kwao. Tuuenzi Muungano wetu kwa kudumisha amani.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment