AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, April 30, 2015

Wakimbizi wa Burundi wanaoingia Tanzania wahakikiwe kwa umakini.

Katuni.
Katika toleo letu la leo ukurasa wa mbele, tumeripoti kuwa zaidi ya wakimbizi 200 kutoka nchini Burundi, wameingia nchini kupitia mkoani Kigoma.
 
Raia hao wa Burundi wanaikimbia nchi yao kutokana na hofu ya kuzuka kwa vurugu kufuatia Rais wa sasa wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza, kutangazwa kuwa atagombea tena wadhifa huo kwa awamu ya tatu.
 
Baada ya chama tawala cha Burundi cha CNDD-FDD kumtangaza  Nkurunziza kwamba atagombea tena urais wa nchi hiyo kwa muhula wa tatu, wapinzani wa serikali ya nchi hiyo, waliitisha maandamano makubwa ya kupinga hatua hiyo.
 
Wapinzani wa Serikali ya Burundi waliamua kuitisha maandamano hayo makubwa baada ya kutokubaliana na uamuzi huo wa chama tawala kwa kuwa Katiba ya nchi yao hairuhusu mtu mmoja kugombea nafasi ya urais kwa mihula mitatu.Kiongozi wa chama cha FNL kilichopigwa marufuku nchini Burundi, Agathon Rwasa, alipinga vikali uamuzi huo akisema unakwenda kinyume na Katiba ya nchi yao.
 
Kwa mujibu wa Rwasa ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Nkurunziza katika uchaguzi mkuu wa Juni, 2010, kuteuliwa kwa Rais Nkurunzinza kugombea tena urais wa Burundi kwa mara ya tatu, kutasababisha machafuko katika nchi hiyo.
Wapinzani hao wa Serikali ya Burundi, walianza kuitisha maandamano makubwa kuanzia Aprili 26, mwaka huu kupinga hatua hiyo ya chama tawala cha nchi hiyo.
 
Wakati Mwenyekiti wa chama tawala cha Burundi, Pascal Nyebenda, akimtangaza Rais Nkurunziza kwamba atagombea tena urais mwaka huu, aliwataka wapinzani wa serikali kuwa watulivu na kuacha masunduku ya kura yaamue.
 
Waandamanaji hao wamekuwa wakipambana vikali na polisi wa Burundi na hivyo kusababisha vurugu zisizokoma, hali inayotishia amani na utulivu wa nchi hiyo.
 
Ni kutokana na tishio hilo la kutoweka kwa amani nchini Burundi, ndipo baadhi ya wananchi hao wameanza kuikimbia nchi yao na kwenda nchi nyingine ikiwamo Tanzania wanakoamini kwamba watakuwa salama na familia zao.
 
Ni dhahiri kwamba Tanzania tangu enzi, imekuwa kimbilio la wageni wengi kutoka katika nchi zao zinazokumbwa na misukosuko ya kiasiasa.
 
Tanzania ilipokea wapigania uhuru wa nchi kadhaa miaka ya 1960 wakati nchi nyingi zikipigia kujikomboa na hata baada ya nchi nyingine kufanikiwa kupata uhuru, pale palipotokea vurugu za kisiasa, watu wao waliamua kuja hapa nchini kwa ajili ya hifadhi.
 
Kwa ujumla, Watanzania ni watu wema na wanasifika kwa hilo na katika hali ya kibinadamu, hatuwezi kuwaacha binadamu wenzetu wenye matatizo ambao kwa hiari yao, wameamua kuomba hifadhi hapa nchini kwetu.
 
Katika tukio hili la sasa la wakimbizi wa Burundi, tumeambiwa kuwa walianza kuingia mkoani Kigoma tangu juzi na hadi kufikia jana, inakadiriwa kwamba walikuwa wamefikia zaidi ya 200.
 
Kwa mujibu wa habari hizo, wakimbizi hao wamepokelewa na Idara ya Uhamiaji Monyovu mkoani Kigoma na kwamba kulikuwa na matarajio ya idadi hiyo kuongezeka kadiri siku zinavyosonga mbele.
 
Sisi hatuna shida na kupokelewa kwao hapa nchini na kupewa hifadhi, jambo la msingi ambalo tungependa kuzishauri mamlaka zinazohusika na kuratibu shughuli hiyo, ni kuwa makini katika kuwahakiki na kubaini kwamba ni wakimbizi halali na wanaohitaji hifadhi ya kweli.
 
Tunafahamu kwamba katika kuwatambua kuna ugumu kwa kiasi fulani kwani si rahisi kutambua dhamira ya kila mmoja wao.
 
Hata hivyo, tunazidi kuzisihi mamlaka husika kufanya kazi hiyo kwa umakini na weledi mkubwa kwani kutokana na uzoefu wetu wa miaka ya nyuma ambapo licha ya kuwapokea wakimbizi kwa moyo safi, baadaye baadhi yao walitugeuka na kuwa wahalifu tena wengine wa kutumia silaha za moto. Ili kuwadhibiti, ni vema basi wakimbizi hao wakatengewa maeneo yao maalum mbali na makazi ya raia na hata wakawekewa masharti maalum ya kwenda nje ya maeneo hayo. Si nia yetu kuwabagua ndugu zetu wa Burundi, bali ni katika kuhakikisha kwamba pamoja na kuwapokea kutokana na utu wetu, lakini pia ni muhimu kuangalia usalama wa nchi yetu.
 
Tusirudie makosa tuliyoyafanya miaka ya nyuma kiasi cha nchi yetu hususan maeneo ya mipakani kama Kigoma, Kagera na Rukwa ambako wakimbizi hao walipata hifadhi, yakageuka kuwa maeneo ya matukio ya uhalifu kila uchao.
 
Ni matarajio yetu kwamba vyombo husika vitazingatia maoni yetu ili kulinda tunu ya usalama na amani ambavyo nchi yetu imeachiwa na waasisi wa taifa letu.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment