Akihutubia mkutano wa hadhara jijini Arusha jana, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alitaja majukumu hayo kuwa ni kuzuia au kukataa njama zozote za kuahirisha Uchaguzi Mkuu, kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura na kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi.
Arusha. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umetaja majukumu makuu matano yanayopaswa kutekelezwa na Watanzania wenye mapenzi mema kuelekea Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu.
Akihutubia mkutano wa hadhara jijini Arusha jana, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alitaja majukumu hayo kuwa ni kuzuia au kukataa njama zozote za kuahirisha Uchaguzi Mkuu, kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura na kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi.
Lissu alilitaja jukumu lingine ni kuchagua wagombea wanaotokana na vyama vinne vinavyounda Ukawa, kulinda na kuchunga kura zao zisichakuchuliwe na hatimaye kuking’oa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye pia alihudhuria na kuhutubia mkutano huo, alionya kuwa kitendo chochote cha kujaribu kubadilisha Katiba ili kumwongezea muda Rais Jakaya Kikwete na CCM kuongoza nchi ni kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa Taifa.
“Tunashuhudia yanayotokea nchi jirani ya Burundi kwa sababu watawala hawataki kuachia madaraka kikatiba. Hatutaki Taifa letu liwe na taswira ya kutotawalika,” alisema Kafulila.
Alisema kwa muda wa zaidi ya miaka 50 ambayo CCM imeongoza nchi kwa majaribio imetosha, hivyo wananchi wana jukumu la kukiondoa madarakani chama hicho kupitia sanduku la kura kwa kuchagua wagombea wa Ukawa.
“Tanzania ni kati ya nchi iliyojaaliwa rasilimali nyingi, yakiwamo madini, mito mingi, maziwa na misitu lakini bado wanafunzi wetu wanakaa chini madarasani kutokana na kukosa madawati, huku uhaba wa maji ukiwa kati ya matatizo sugu nchini,” alisema Kafulila.
Awali, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliuambia mkutano huo kuwa hana hofu na watu wanaojitokeza na kujitangaza kuwania jimbo hilo kwa sababu ana uhakika atashinda kwa kishindo kuliko ilivyokuwa 2010 alipomshinda mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian kwa zaidi ya kura 20,000.
“Jukumu la kulinda na kushinda jimbo na kata za Arusha naliacha mikononi mwa viongozi wa Ukawa na wananchi wa Arusha,” alisema Lema.
Mbunge huyo alitaja ushindi wa vyama vinavyounda Ukawa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana kama ishara njema ya ushindi dhidi ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
No comments :
Post a Comment