
Amedai kuna njama hatari zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuvuruga uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa Zec na SMZ zimekuwa zikifanya mambo kadhaa yenye lengo la kuvuruga uchaguzi mkuu ujao na hivyo kuibua tishio la kuirejesha Zanzibar katika machafuko.
Katika maelezo yake, Maalim Seif alieleza kuwa baadhi ya mambo hayo ni kuwapo kwa uandikishaji wapiga kura wenye umri mdogo, kuandikisha watu zaidi ya mara moja, wapiga kura mapandikizi, wapigakura wanaotumia majina na picha ambazo si zao na pia kuwapo kwa wapiga kura wanaozidi idadi.Alidai kuwa ipo mipango ya kuingilia uandikishaji wapiga kura unaotarajiwa kuanza Mei 16 hadi Juni 28, mwaka huu kwa kuandaa wapiga kura haramu na kuonya kuwa jambo hilo ni hatari kwani mara zote, mizozo ya kisiasa Zanzibar huanzishwa na kuchochewa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi kuanzia hatua ya uandikishaji wa wapiga kura, uhesabuji wa kura na utangazwaji wa matokeo ya uchaguzi.
Akitoa mfano, Maalim Seif alidai kuwa kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyopo Chukwani, kisiwani Unguja imekuwa ikitumika kuandikisha mamia ya vijana wakiwamo wengi ambao si Wazanzibari na kuwapatia Vitambulisho vya Uzanzibari (Zan IDs) kwa ajili ya kuandikishwa kama wapigakura. Kwamba, katika majimbo mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba wameandikishwa vijana wanaofikia 20,000 na kupewa Zan IDs na wamepangwa kuandikishwa kama wapigakura kwa kuhamishwa kutoka nje ya majimbo yao.
Aliongeza kuwa wapo vijana 700 waliochukuliwa katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Uzini na kupelekwa kusajiliwa katika Jimbo la Bububu Kisiwani Unguja, vijana 10,000 waliohamishwa kutoka wilaya ya Kati Unguja na kusajiliwa majimbo ya Dimani na Mtoni katika Wilaya ya Magharibi Uguja na majimbo ya Chumbuni na Kwamtipura Wilaya ya Mjini Unguja. Vijana wengine 1,200 wamepatiwa Zan IDs kwa ajili ya kuandikishwa katika Jimbo la Chonga na wengine 1,000 katika Jimbo la Mkanyageni kisiwani Pemba.
Kwa mujibu wa Maalim Seif, mkoa wa Kaskazini Unguja katika Jimbo la Tumbatu watoto wadogo wa miaka 14 hadi 17 huchukuliwa na kupelekwa kituo cha kusajili vitambulisho vya Mzanzibari kilichopo Gamba ambako wamepatiwa Zan IDs na sasa wanasubiri kuandikishwa katika daftari. Madai mengine yaliyotolewa na Maalim Seif ni kuwapo kwa ucheleweshaji wa ugawaji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi kwa nia ya kuinufaisha CCM, hasa kwa kupunguza maeneo yenye wafuasi wengi wa CUF na kuongeza majimbo yenye wafuasi wengi wa CCM.
Kutokana na yote hayo, Maalim Seif alisema kuwa chama chake (CUF) kinapendekeza kuchukuliwa kwa hatua kadhaa, baadhi zikiwa ni kufutwa kwa wapigakura haramu waliopatiwa vitambulisho vya Mzanzibari kichume cha sheria, kutaka wananchi wapatiwe Zan IDs kabla ya uandikishaji wapigakura na pia vikosi vya ulinzi na usalama vikiwamo vya JWTZ na Idara Maalum za SMZ kuacha kutumiwa kisiasa.
Hakika, madai haya siyo ya kubeza. Uzito wake unaongezwa na ukweli kuwa aliyeyatoa ni kiongozi wa juu katika muundo wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar. Ni kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa ipo haja kuona kuwa madai haya yanafanyiwa kazi na vyombo vyote husika na majibu ya kina kutolewa kwa umma, sawa na vile alivyofanya Maalim Seif.
Historia ya Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikigubikwa na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa. Watu kadhaa wasio na hatia wameshapoteza maisha, wengine kupata ulemavu wa kudumu na kwa mara ya kwanza Tanzania iliwahi kuzalisha wakimbizi waliohifadhiwa Shimoni, Mombasa Kenya kutokana na kadhia za vurugu baada ya uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar. Sisi tunadhani kwamba busara na hekima zilizotumika katika uchaguzi mkuu wa 2010 ulioiweka madarakani Serikali ya Umoja wa Kitaifa zinapaswa kudumishwa. Kwa namna yoyote ile, kamwe kusiwe na nafasi ya kurejea kwa machafuko yaliyoshuhudiwa katika chaguzi za miaka ya 1995, 2000 na 2005. Madai mazito ya Maalim Seif yafanyiwe kazi na majibu kutolewa. Hili lizingatiwe kwani wahenga walinena kuwa "tusipoziba ufa, tutajenga ukuta".
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment