dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, May 27, 2015

Makongoro Nyerere autaka urais.

Mtoto wa Baba wa Taifa, Charles Makongoro Nyerere.
Mtoto wa Baba wa Taifa, Charles Makongoro Nyerere amevunja ukimya juu ya uvumi ulioenea kwamba yeye ni miongoni mwa watu wanaotarajiwa kuchukua fomu ya kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kusema hata yeye anajisikia na yuko tayari kiafya, kiakili na ana nguvu ya kulitumikia Taifa kwenye nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
 
Hata hivyo, Makongoro alisema kuwa dhamira hiyo ataiweka wazi kwa kuzungumza na wandishi wa habari siku mbili au tatu kabla ya tarehe iliyopangwa na CCM ya kuanza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
 
Makongoro aliyasema hayo juzi jijini Mbeya wakati akipokea kwa niaba ya familia ya Baba wa Taifa, Tuzo ya Uongozi uliotukuka na Uzalendo ambayo ilitolewa na viongozi wa dini za Kiislamu na Kikikristo mkoani Mbeya kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kutambua mchango wake kwa Taifa la Tanzania.Makongoro alilazimika kulisema hilo, baada ya watu mbalimbali waliokuwa wakizungumzia wasifu wa Hayati Baba wa Taifa kila mara kugusia uvumi unaomhusisha na kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
 
“Kwa kuwa kuna maneno yanapita na mimi nimeyasikia, na kwa kuwa nanyi mmenitaka niseme ninachoweza kuwaeleza hata mimi najisikia na niko tayari kulitumikia taifa katika nafasi hiyo (urais), nimesikia CCM wametangaza ratiba ya kuchukua fomu, hivyo ninachoweza kuwathibitishia ni kwamba siku mbili au tatu kabla ya tarehe iliyopangwa na CCM kuanza kuchukua fomu nitazungumza na waandishi wa habari kuelezea uamuzi wangu juu ya suala hilo,” alisema Makongoro.
 
CCM tayari imetangaza ratiba na utaratibu kwa wale wanaotaka kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, na tarehe ya kuanza kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo itakuwa Juni 3, mwaka huu.
 
Aidha, alisema wiki ya kwanza ya kuanza kuchukua fomu za kugombea urais kupitia CCM, atakuwa mjini Dodoma kwa ajili ya ama kuwashuhudia wale wanaochukua fomu hizo au yeye mwenyewe kuchukua fomu.
 
Kwa kauli hiyo, Ni dhahiri kwamba mtoto huyo wa Baba wa Taifa ameingia rasmi kwenye orodha ya makada wa CCM walioonyesha nia ya kutaka kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini anachelea tu kukiuka kanuni na taratibu za Chama chake cha CCM kama atatangaza uamuzi wake mapema. 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment