NA EDITOR
21st May 2015

Taarifa hiyo imebainisha kuwa katika kipindi hicho, serikali imepoteza zaidi ya Sh. bilioni moja kwa kuendelea kulipa mishahara hewa kwa watumishi wa umma waliofariki dunia, waliostaafu na waliofukuzwa kazi katika halmashauri 36 nchini. Kiasi hicho kimesababisha hasara kubwa kwani fedha hizo zilitengwa ili zitumiwe na halmashauri na serikali za mitaa. Fedha nyingine kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 140 zililipwa kwa wafu, wastaafu na watumishi wa umma walioacha kazi.
Taarifa hiyo ilifichua vilevile kuwa zipo kampuni za madini zilizoisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 22.33 kwa kuhujumu misamaha ya kodi waliyopewa. Maeneo mengine ambayo wizi umeisababishia serikali hasara ni ule wa kuisamehe kodi ya zaidi ya Sh. milioni 465 kwa kampuni moja ya Arusha, Sh. bilioni 2.3 zilizotumiwa na Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro kwa kununua bidhaa zisizokuwa na sababu ya msingi; Kampuni ya Simu ya TTCL kufanya manunuzi yasiyokuwa ya lazima yenye thamani ya Sh. milioni 381.97 na pia kasoro nyingine zimebainika katika Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambako kumefanyika manunuzi bila kushindanisha wazabuni, thamani yake ikiwa ni Sh. bilioni 1.75. Yapo pia maeneo mengine mengi yaliyoainishwa na CAG, na ambayo kwa ujumla yameisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha za walipa kodi.
Sisi tunaona kwamba hali hii haipaswi kuachwa. Haivumiliki. Kuna kila sababu kwa serikali kutumia vyombo vyake vya dola kuhakikisha kuwa watu wote waliohusika katika wizi wa fedha hizi za umma wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria. Na hili linapaswa kutiliwa mkazo. Vinginevyo, taarifa hii ya CAG itakosa maana.
Isipofanyiwa kazi haraka na wahusika kuchukuliwa hatua, ni wazi kuwa hata taarifa yenyewe (ya CAG) itakuwa ni muendelezo tu wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma kwani uandaaji wake ulitumia fedha nyingi na muda katika kuikamilisha. Isitoshe, kwa kuwachukulia hatua wahusika, ni wazi kwamba kutatoa somo kwa watu wengine wenye kujihusisha na vitendo hivyo kutambua kuwa fedha za umma hazipaswi kuchezewa. Ni wazi vilevile kuwa wananchi wenye kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi watafarijika kusikia kuwa walaji wa fedha zao wanachukuliwa hatua zinazostahili. Wala si vinginevyo.
Kadhalika, ikumbukwe kuwa taifa hili ni changa sana kiuchumi. Kwa vigezo vyovyote vile, nchi yetu kwa sasa haiwezi kukosekana katika kundi la nchi maskini sana duniani. Na ndiyo maana licha ya kuwapo kwa jitihada zinazoendelea kila uchao katika kujikwamua kiuchumi, bado kuna changamoto nyingi mbele yetu. Kuna utitiri wa vikwazo katika kutekeleza miradi mbalimbali ili hatimaye kutimiza malengo tuliyojiwekea kupitia 'Dira ya Taifa ya Mwaka 2025'.
Kwa mfano, hakuna asiyefahamu kuwa maeneo mengi ya nchi yetu yanakabiliwa na ukosefu wa huduma za kijamii. Hadi sasa baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru, kuna maeneo mengi bado hayana maji safi na salama. Yapo maeneo mengi pia yasiyofikika kwa urahisi katika muda wote wa mwaka kutokana na ukosefu wa barabara. Upatikanaji wa huduma za afya ya msingi pia ni tatizo kubwa, sawa na ilivyo kwa elimu ambako jitihada zinaendelea kufanywa kukabiliana na uhaba wa walimu, ukosefu wa nyumba za kuishi za walimu, ukosefu wa miundombinu muhimu na inayoendana na idadi ya wanafunzi kama maabara na pia ukosefu wa vitabu na vifaa vya kufundishia.
Katika hali kama hii, ndipo sisi tunapoona kwamba watu hawa waliokosa uzalendo, watu hawa wanaotumia mbinu mbalimbali zikiwamo za kukiuka taratibu za fedha tulizojiwekea ili kujinufaisha binafsi, kamwe hawastahili kuhurumiwa. Wachukuliwe hatua kali ili kuliepusha taifa na aibu hii ya kuwapo kwa vitendo vya ufisadi kila uchao.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment