Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, June 4, 2015

Amina Salum Ally: Nitatumia miaka mitano kujenga uchumi



Amina Salum Ally 
Amina ni mwanamke pekee katika historia ya Tanzania ambaye amejitosa kuwania nafasi hiyo adimu, akipigana vikumbo na makada wanaume wa CCM, na kwa mara ya kwanza alijitosa kuwania urais upande wa Zanzibar akiwa na Amani Abeid Karume ambaye alipitishwa kwenye Kamati Kuu mwaka 2000.

Dar es Salaam/Zanzibar. Kwa mara ya pili Amina Salum Ally, anasimama kuomba kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amina ni mwanamke pekee katika historia ya Tanzania ambaye amejitosa kuwania nafasi hiyo adimu, akipigana vikumbo na makada wanaume wa CCM, na kwa mara ya kwanza alijitosa kuwania urais upande wa Zanzibar akiwa na Amani Abeid Karume ambaye alipitishwa kwenye Kamati Kuu mwaka 2000.

Amina ambaye ni Mjumbe wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa (UN), na Balozi anayewakilisha Muungano wa Afrika (AU) nchini Marekani, amejitosa tena safari hii akisema wanawake wamekuwa wanyonge kugombea nafasi za juu za uongozi kwa kukosa fedha, lakini sasa ni wakati mwafaka kwao kujiamini na kuthubutu.

“Nimeona nina uzalendo, ninajiamini na ninaweza kuifikisha nchi yangu katika uchumi wa kwanza kwa kutumia rasilimali zetu zikiwamo gesi, mafuta, kilimo na utalii. Ninajiamini kwamba wakati wangu umefika kuwaongoza Watanzania,” anasema Amina.
“Wanawake wengi wanaogopa kujitokeza wakihofia kugombea nafasi za juu za uongozi kwamba kunahitaji fedha, hivyo wanaishia kuwa wanyonge, siyo kweli, wajitokeze kwa wingi ili kutoa mchango mkubwa walionao kwa taifa letu,” anasema.

Vipaumbele vyake
Amina anataja vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kuinua uchumi, kuongeza mapato, kupambana na rushwa, huduma za jamii kuondoa matabaka ya walionacho na wasionacho na kudhibiti mapato ili yaendane na matumizi.
“Tunaambiwa uchumi umekua kwa asilimia saba…, tunataka ukue kwa asilimia 10, hatutaki uchumi wa tatu, kwanini tusifikie uchumi wa kwanza? Anahoji Amina.

“Katika hili, nia yangu ni kuweka mkazo katika maeneo yatakayosaidia kukuza uchumi, ikiwamo kuongeza vitega uchumi vya ndani.”

Anasema ili kuwa na misingi imara ya uchumi endelevu, kinachotakiwa ni kuwawezesha wananchi wafaidi rasilimali zao kwa kuwashirikisha kwa karibu hususani wanawake na vijana.

Amina ameahidi kupambana na ufisadi na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kipindi cha miaka mitano atakapokuwa madarakani, huku akisisitiza serikali yake haitafumbia macho vitendo viovu na atamwadhibu yeyote atakayebainika kuhusika na ufisadi.

Kwa nini anataka urais?

Amina anasema historia inaonyesha Tanzania haijawahi kuwa na kiongozi wa juu wa serikali katika ngazi ya maamuzi ambaye ni mwanamke.

“Nataka nilete changamoto mpya, najua na ninaelewa sana kuwa Tanzani bado ina mfumo dume, hawakubali kuongozwa na mwanamke, najua kuna watu wanabeza lakini mimi nataka kufuta dhana hiyo potofu, nataka niwatoe hofu Watanzania kuwa wanawake ni bora kwenye ngazi ya uongozi kuliko wanaume, muangalieni Dilma Rousseff Rais wa Brazil anafanya mambo makubwa katika taifa lake.

“Nawashangaa wanaobeza eti nipate uzoefu kwanza, ni uzoefu wa aina gani unatakiwa, eti nchi yetu bado changa hivi nchi yetu ni changa au imedumaa?” Alihoji na kuongeza: “Nitapambana kuhakikisha nawavusha Watanzania kutoka hapa tulipo na kwenda sehemu tunapotakiwa kuwa, keki ya Taifa igawanywe kwa usawa sio wengine wapate kidogo, wengine wapate pande kubwa, tabaka la walionanacho na wasionacho linaongezeka kila kukicha huku watu wachache wakinufaika na rasilimali za nchi, hali hiyo nitaiondoa, nitapambana kuhakikisha napunguza kwa kiasi kikubwa kama sio kuondoka tabaka hilo.

“Nitahakikisha uwakilishi wa wanawake katika bodi na paneli katika sekta zote za serikali na binafsi. Nitatokomeza matendo ya ubaguzi kwa misingi ya kijinsia. Nitasimama kinyume na ukatili dhidi ya wanawake.”

Amesema licha ya juhudi za kuongeza nafasi za wanawake katika vyombo vya maamuzi mathalani Bunge, bado haitoshi na hivyo atahakikisha anapigania uwakilishi wa ongezeko la wanawake bungeni na kufikia asilimia 50 kwa 50.

Anasema yeye amekuwa kiongozi tangu enzi za Afro Shirazi Party (ASP), Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na hata katika Umoja wa Afrika (AU) hivyo anao uzoefu wa kutosha katika uongozi.

“Uadilifu, uwezo na malezi ya CCM katika historia yangu ya uongozi, vinanipa nguvu… nafasi iliyobaki kwangu ni kugombea urais.

“Kwa imani na itikadi zangu, nimeona ninao uwezo wa kuifikisha Tanzania mahali na wakati ndiyo huu, naamini naweza kuendesha nchi yetu kwa uadilifu, uzalendo na kujituma.

“Kugombea urais, si jambo la kugombana, ni utaratibu wa chama, lazima mtu achaguliwe, watu wananiuliza huogopi kwa kuwa ni mwanamke, nasema siogopi na sioni tatizo kwa kuwa nina uwezo,” anasema Amina.

Kwa hakika, hata kabla ya harakati zake hizi za urais, Balozi Amina alishajijengea jina Marekani kama mmoja wa wanadiplomasia machachari wa kike wa Afrika; akiwekwa kundi moja na kina Josefina Perpertua wa Angola, Faida Mitifu wa Congo, Molelekeng Ernestina wa Lesotho, Hawa Ndilowe wa Malawi, Barbara Maszekela wa Afrika Kusini na wengine kadhaa waliopata kung’ara wakiwa UN.

Lakini ukweli ni kwamba Balozi Amina ni zaidi ya hao. Wakati hao ni wawakilishi wa nchi zao tu katika Marekani, yeye anawakilisha bara zima la Afrika na amekiri kukutana na changamoto na kudai kuwa wadhifa alionao umetosha kumpa ujasiri wa kuweza kusimama na kuwania urais wa Tanzania na kudhamiri kuwatetea wanawake na kutoa fursa sawa kwa wote.

Amina ni nani

Alizaliwa Oktoba 24 mwaka 1956 na ni msomi mwenye uzoefu katika masuala ya uchumi na masoko. Ukiacha elimu ya msingi na sekondari aliyoipata katika shule mbali mbali visiwani Zanzibar, Amina pia amepata elimu ya juu katika Chuo Kikuu nchini India ambako amefanikiwa kuhitimu Shahada ya Kwanza katika nyanja ya Uchumi na Shahada ya Pili katika nyanja ya Biashara na Masoko.

Kati ya mwaka 1981 na mwaka 1982 alikuwa mchumi mwandamizi katika Tume ya Mipango Zanzibar. Mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Biashara za Nje - Wizara ya Biashara ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mwaka 1983 na1984 alikuwa Katibu katika Bodi ya Biashara Zanzibar na mwaka 1984 na 1985 alikuwa Mchumi Mwandamizi katika Tume ya Mipango kwenye Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar.

Mwaka 1990, Amina aliteuliwa kuwa waziri wa kwanza mwanamke kupewa dhamana ya Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, nafasi ambayo aliitumikia kwa ufanisi wa hali ya juu.

Mnamo mwaka 2000, Amina alikuwa mmoja miongoni mwa wagombea sita wa urais wa Zanzibar; lakini hakufanikiwa. Mwaka 2005, Amina aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Kiongozi baada ya kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani kwa tiketi ya CCM.

Tangu mwaka 2007, Amina ni Balozi anayewakilisha Muungano wa Afrika (AU) katika nchi ya Marekani. Kama mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, Amina amejikita katika kutetea haki za wanawake na watoto.

Vilevile, ni mwanzilishi wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ijulikanayo kwa jina la Zanzibar Women Welfare Trust ambayo lengo lake kuu ni kupambana na magonjwa yanayowakumba wanawake na watoto, ikiwa ni pamoja na Ukimwi.

Kazi nyingine alizopata kufanya na miaka yake kwenye mabano ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1985-1990), Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1985 – 1986) na Waziri wa Nchi wizara ya Mambo ya Nje (1986 na 1989).

Aliwahi pia kuwa Waziri wa Nchi katika Wizara ya Fedha ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1989 – 1990), Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1990-2000), Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Waziri wa Fedha Zanzibar (2001 – 2005), Mjumbe wa Tume ya Mipango, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (2005-2006) na Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (2006) nchini Marekani.

No comments :

Post a Comment