Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimebaini mchezo mchafu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya maofisa waandikishaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) wa kusajili wapiga kura usiku bila kuhusisha mawakala wa vyama vya siasa, jambo lililoelezwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Chadema, Benson Kigalila, akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa alisema uandikishaji wapiga kura umeanza kwa hujuma zinazolenga kuibeba CCM.
Alisema ofisa wa NEC katika Manispaa ya Dodoma Helen Maungo, alikutwa katika kituo cha kuandikisha wapiga kura cha Kiwanja cha Ndege akiandikisha wapiga kura saa 2:05 usiku wakati kituo chake cha kazi ni Mlimani C.
Kigaila alisema Maungo alifunga kituo cha kazi saa 12:00 jioni kama kanuni na sheria za NEC zinavyoelekeza na kuhamia kituo cha Mlimani C akiendelea kuandikisha wananchi usiku bila mawakala wa vyama vya siasa.
Alisema ofisa huyo wa NEC alikutwa na mawakala wa Chadema akiandikisha wananchi katika kituo hicho kukiwa na foleni ya watu wengine na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Agustino Kalinga, alipojulishwa akilifika eneo la tukio akiwa na maofisa wengine wakiwamo polisi na kumchukua.
Kigaila alisema kilichofanywa na waandikishaji ni kosa na ni hujuma inayoonekana ni mbinu ya viongozi wa Manispaa ya Dodoma kuwaandikisha watu kinyemela kwa manufaa ya CCM.
Alisema kutokana na hujuma hizo zilizoanza kufanyika, kuanzia jana vijana wa Chadema watakuwa wanazisindikiza mashine za Biometric Voters Registartion (BVR) zinazotumiwa kuandikisha wapiga kura hadi sehemu zinakohifadhiwa ili zisichukuliwe na kwenda kuandikisha watu kinyemela.
“Kuanzia leo tutahakikisha tunafanya msako wa Helen Maugo katika vituo vyote 102 na tukimkamata tutamfikisha polisi, na makawala mkimuona mtoe taarifa kwa viongozi wa juu wa chama,”alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Taifa (Bawacha), Kunti Majala alisema kuwa kazi ya uandikishaji wapiga kura imegubikwa na changamoto hususani maeneo ya vijijini vijana ambao wana miaka 17 na miezi nane wamekuwa wakizuiwa kuandikishwa na mabalozi, watendaji wa vijiji na kata licha ya sheria ya uchaguzi inawaruhusu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Kalinga alipotafutwa ili kuelezea suala hilo licha ya kukiri kulifahamu alisema hawezi kuzungumza zaidi kwa kuwa yupo katika mkutano.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema kuwa hana taarifa kuhusiana na suala hilo kwa kuwa mambo ya uandikishaji yanamhusu Mkurugenzi wa Manispaa.
Wakati viongozi hao wakikwepa kueleza aliko Helen Maugo, taarifa amabzo NIPASHE Jumapili ilizipata ni kwamba amefichwa kwa ajili ya kulinda usalama wake.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

No comments :
Post a Comment