
Hadi kufikia jana taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilikuwa zikionyesha kuwa dola moja ya Marekani ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh. 2,092.91, kiwango kinachoashiria kuporomoka shilingi kwa wastani wa asilimia 16.5 kulinganisha na thamani ya sarafu hiyo katika kipindi cha miezi mitatu tu iliyopita. Machi mwaka huu, taarifa za BoT zilionyesha kuwa dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na Sh.1,797.06.
Aidha, katika baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha jijini Dar es Salaam jana, dola moja ya Marekani ilikuwa ikiuzwa hadi wastani wa Sh. 2,300.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kupitia takwimu za BoT unaonyesha kasi ya sasa ya kuporomoka kwa shilingi ni kubwa kuliko kipindi chochote tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, iliyoingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.Katika takwimu hizo, inaonekana kuwa thamani ya shilingi ilikuwa ikiporomoka kulinganisha na dola ya Marekani kwa tofauti ndogo kulinganisha na sasa.
Kufikia Desemba 2005, dola moja ya Marekani ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh.1,163.95; Desemba 2006 (Sh. 1,261.64); mwaka 2007 (Sh.1,147.33); 2008 (Sh. 1,280.30) na Desemba 2010 ilibadilishwa kwa Sh. 1,327.22.
Kadhalika, baada ya serikali ya awamu ya nne kuingia tena madarakani mwaka 2010, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa Sh.1,613.23 kufikia Desemba 2011; Desemba 2012 ikabadilishwa kwa Sh. 1,578.40; Desemba 2013 kwa Sh. 1,604.38; Desemba mwaka jana Sh. 1,725.76 na sasa, imefikia Sh. 2,092.91 kwa taarifa za jana za BoT.
Kwenye maduka mbalimbali ya mitaani shilingi ilionekana kuporomoka zaidi dhidi ya dola ya Marekani kiasi cha kubadilishwa kwa Sh. 2,300.
Takwimu hizo za BoT zinaonyesha vilevile kuwa Desemba mwaka 1999, dola moja ilikuwa sawa na Sh. 797.33; Desemba mwaka 2000 ikawa Sh. 803.28; Desemba 2001 (Sh. 916.04); Desemba 2002 (Sh. 976.65); Desemba 2003 (Sh. 1,061.88) na Desemba 2004 ilibadilishwa kwa Sh. 1,042.77.
SABABU ZA SHILINGI KUPOROMOKA
Akizungumza na NIPASHE jana, mtaalamu wa masuala ya uchumi, Prof. Humphrey Moshi, alisema shilingi inaporomoka kwa kasi hivi sasa kutokana na sababu kubwa tano.
Mosi; mfumo mbaya wa uchumi unaotoa fursa ya kuagizwa zaidi bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kuliko zinazoagizwa. Matokeo yake hali hiyo husababisha kuwapo kwa mahitaji makubwa ya fedha za kigeni na hivyo kuporomosha thamani ya shilingi.
Pili, alisema ni kashfa ya ufisadi wa fedha za Escrow anayoamini kuwa kwa kiasi kikubwa ilisababisha baadhi ya wafadhili kusitisha fedha walizoahidi kutoa na hivyo kupunguza kiasi cha fedha za kigeni ambazo vinginevyo zingeingia na kutumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Tatu, Prof. Moshi alisema kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu husababisha pia kuadimika kwa fedha za kigeni kwani baadhi ya matajiri huamua kuhifadhi zaidi fedha za kigeni kwa tahadhari kuwa pengine kunaweza kuibuka matafaruku katika kupokezana madaraka na hivyo wawe na nafasi ya kwenda nje ya nchi wakiwa salama wao na fedha zao.
Prof. Moshi aliitaja sababu ya nne kuwa ni kuongezeka kwa watu wanaotumia fedha za kigeni kutokana na hofu inayoendelea kuwapo juu ya kuporomoka kwa shilingi kila uchao.
"Hali hii ya kuporomoka shilingi kila uchao inasababisha baadhi ya watu ku-panic (kuhamaki). Kwa sababu hiyo hata watu wasiokuwa na mazoea ya kutumia dola ya Marekani wanaingia katika mkumbo wa watumiaji wa fedha hizo za kigeni na jambo hili huchangia kuporomoka zaidi kwa thamani ya shilingi," alisema Prof. Moshi
Tano; Prof. Moshi alisema ni kasoro kwenye mikataba inayoingiwa na kampuni kubwa mbalimbali za wawekezaji nchini, zikiwamo kuruhusu wawekezaji wakubwa katika baadhi ya kampuni kumiliki hisa nyingi bila kuhusisha serikali au Watanzania wenyewe kwa uwiano unaowapa nguvu katika maamuzi.
Alisema kwa sababu hiyo, wawekezaji hupata nafasi ya kuamua kununua baadhi ya vitu nchini mwao na kwingineko, hivyo kuongeza mahitaji ya dola na kushusha thamani ya shilingi.
ATHARI
Prof. Moshi alisema miongoni mwa athari zinazoonekana wazi kutokana na kasi kubwa ya kuporomoka shilingi ni pamoja na kuongezeka kwa mfumuko wa bei.
"Wafanyabiashara wanapotumia fedha nyingi kuagiza vitu kutoka nje maana yake ni kwamba watalazimika pia kuuza kwa bei ya juu ili kufidia gharama na kupata faida. Shilingi inapozidi kuporomoka ndivyo pia bei zinavyobadilika na matokeo yake kuongeza mfumuko wa bei... wanaoumia zaidi ni wananchi wa kawaida kwani vipato vyao viko palepale lakini gharama za maisha zinaongezeka kila siku," alisema Moshi.
Alitaja athari nyingine kuwa ni kudharauliwa kwa sarafu ya nchi na kwamba hilo linathibitishwa na baadhi ya viongozi ambao huitambulisha shilingi kama "fedha ya madafu".
WAFANYABIASHARA WALIA
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti walisema kushuka kwa thamani ya shilingi kila uchao kunawaathiri kwa kiasi kikubwa na kutishia ustawi wa biashara zao.
Meneja wa Mauzo wa kampuni ya kuuza magari ya Tezz Commission Agent ya Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam, Hafidh Amir, alisema miongoni mwa athari za kuporomoka kwa shilingi ni kuongezeka kwa gharama za kuagiza magari na pia biashara kuwa ngumu kwani hulazimika kuongeza bei ili kufidia gharama hizo.
Amir alisema gari linapoagizwa kutoka katika nchi kama Japan hufika nchini baada ya kipindi cha wastani wa miezi miwili na hivyo kuporomoka kwa shilingi huwapa wakati mgumu katika kuyauza.
"Kwa mfano, miezi miwili iliyopita tuliagiza gari aina ya Toyota Noah wakati dola moja ya Marekani ikiwa sawa na Sh. 1,800.
Leo hii (jana) dola moja ni Sh. 2,300 na ushuru bandarini kwa Noah za kuanzia mwaka 1999 ni dola za Marekani 2,500 hapo achilia mbali gharama nyingine kama za usajili," alisema na kuongeza:
"Kwa ujumla gharama za kuagiza Noah hivi sasa ni kama Sh. milioni 12.5. Kwa hiyo bei ya kuuza ni lazima iwe juu ya hiyo kufidia gharama na kupata faida kidogo. Lakini wateja wengi wamezoea bei ya Noah ya miezi michache iliyopita ya kati ya milioni 11 na 12.5, sasa hapo ndipo ugumu wa biashara unapoanzia," alisema Amir na kuongeza:
"Tunaomba serikali iangalie namna ya kuiokoa shilingi yetu kwa sababu hali inazidi kuwa mbaya... inaongeza ugumu katika biashara zetu," alisema Amir.
SULUHISHO
Prof. Moshi alisema ili kukabiliana na tatizo la kuporomoka kwa shilingi kila uchao taifa linapaswa kufanya maamuzi magumu katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa sera za kilimo zinatekelezwa kivitendo ili kuzalisha chakula cha kutosha na kuepuka uagizwaji wa vyakula kama mchele na ngano.
"Tuhakikishe vilevile kuwa hatuagizi bidhaa tunazoweza kuzizalisha katika viwanda vyetu nchini... kwa mfano, hakuna sababu ya kuagiza kutoka nje bidhaa kama bia na toothpick (vijiti vya kuchokonolea meno) zinazoweza kuzalishwa hapa hapa nchini," alisema na kuongeza:
"Mikataba tunayoingia na wawekezaji wakubwa iandaliwe vizuri kwa kuhakikisha kuwa serikali inakuwa na hisa nyingi kwa uwiano walau wa asilimia 49 kwa 50, au kuhakikisha kuwa Watanzania wanakuwa sehemu ya wamiliki," alisema.
WABUNGE WANENA
Juzi, wakati akichangia katika mjadala wa bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, aliingia bungeni na mfuko wenye rundo la bidhaa kutoka nje ya nchi zinazoingizwa nchini na kusema kuwa zinasababisha shilingi kuporomoka na hivyo Wizara ya Viwanda na Biashara inapaswa kuchukua hatua za haraka kukomesha hali hiyo.
Baadhi ya bidhaa zilioonyeshwa na Lugola bungeni ni dodoki la kuogea, soksi, vitambaa vya kufutia jasho, chaki, pipi, nyembe, pamba za kutolea uchafu masikioni, kiberiti, rula, penseli, vichongeo vya penseli na ‘note book’ kutoka nchi za Kenya, Marekani na China, ambavyo alidai vingeweza kuzalishwa nchini na kulinda thamani ya shilingi.
“Tuna mambo ambayo tusipoyatafutia ufumbuzi Taifa hili litaendelea kuangamia, la kwanza ni kuporomoka kwa thamani ya sarafu, leo tunatumia Sh. 2,075 kununua dola moja ya Marekani, maisha yanazidi kuwa magumu, serikali iache porojo,” alisema Lugola.
WAZIRI WA FEDHA
Wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema miongoni mwa sababu za kuporomoka kwa shilingi ni kuimarika kwa dola ya Marekani dhidi ya fedha nyingine nyingi duniani kote; mapato kutokana na mauzo nje ya nchi kuwa madogo kulinganisha na mahitaji ya kununua bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi; kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia; na kuongezeka kwa mahitaji ya dola kwa ajili ya malipo ya gawio nje ya nchi kwa baadhi ya kampuni binafsi.
Waziri Mkuya aliahidi kuwa serikali itachukua hatua kadhaa za kulinda thamani ya shilingi na baadhi ya hatua hizo ni kuimarisha maeneo maalum ya kuzalisha bidhaa za kuuza nje (Export Processing Zones) na maeneo maalum ya uwekezaji kiuchumi (Special Economic Zones).
"Hivyo ni rai yetu kwa Watanzania kuzitumia fursa hizi ili kuongeza mauzo yetu nje sambamba na kupunguza uagizaji wa bidhaa na huduma zisizo za lazima kutoka nje ili thamani ya shilingi yetu iendelee kuimarika," alisema Waziri Mkuya,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment