
Katika safari yake hiyo ya mikoa 15 ambapo 12 ni ya Bara na mitatu ya Visiwani, maelfu ya wanachama wa CCM walijitokeza kumdhamini katika wilaya za Nyamagana na Ilemela alizofika kuomba udhamini.
Akiwa katika wilaya ya Nyamagana, Lowassa alipata wadhamini 1671, Ilemela wadhamini 1,456,
Alipowasili jijini hapa, Lowassa alipokelewa na umati kuanzia misafara ya pikipiki, magari na watembea kwa miguu.
Akitangaza wadhamini waliojitokeza kuungana naye kwenye safari ya matumaini, Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Elias Mpanda, alisema wadhamini hao wamepatikana wilayani hapo, kutokana na kuamua kuchukua maamuzi ya kumkubali na kuamini kiongozi huyo ni mtendaji mzuri wa kazi.“Hawa wote ni wana CCM ambao wameamua kujitokeza kwa hiyari yao kumdhamini mgombea wa urais kupitia chama chetu…hawa wote wamejitokeza kwa Lowassa na ni wanachama 1,671,” alisema Mpanda.
Katika wilaya ya Ilemela, katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Ole Meliuti, alisema wanachama hao wamejitokeza kumdhamini Lowassa kutokana na matumaini waliyonayo endapo atapata nafasi ya urais atakuwa muarobaini wa matatizo yao.
Naye mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema Lowassa amekuwa wa kwanza kuingia mkoa wa Mwanza kutokana na kuwa kitovu cha mikoa ya kanda ya ziwa.
Mgeja alisema ngome kubwa ya Lowassa ipo mikoa ya kanda ya ziwa, hivyo ni kiongozi ambaye ataweza kutatua changamoto iwapo atashinda nafasi hiyo.
Naye mwakilishi wa wazee mkoa wa Mwanza, Emanuel Lutalaka, alisema kiongozi lazima aandaliwe na awe mchapakazi.
“Lowassa amefanya kazi makao makuu ya chama kwa muda mrefu, hivyo chama anakifahamu vyema kutokana na kuandaliwa kwake na mchapakazi mzuri,” alisema Lutalaka.
Akitoa neno la shukrani kwa wanachama hao, Lowassa alisema uchaguzi wa mwaka huu ni uchaguzi ambao haujawahi kutokea na ni wa kipekee.
“Wakati mgumu katika nchi yetu umepata kitu cha maana na kitu cha laana…chama chetu kinapimwa sasa, kinaweza kushinda uchaguzi lakini tutashinda kwa kuchagua watu ambao wataweza kulinda maslahi ya nchi,” alisema Lowassa.
Alisema anapochaguliwa Rais pia anachaguliwa mwenyekiti wa chama, hivyo wachague mtu ambaye anakijua chama na ana uchungu na chama hicho.
“Unamchagua Rais awe mwenyekiti ambaye anakijua chama na amekitumikia na si kuchagua mtu ambaye atakipoteza chama maana leo alikuwa chama kingine leo yupo CCM hataweza kujenga chama,” alisema.
Alibainisha uchaguzi huo ni mkubwa sana kwa wana CCM na wataweza kuushinda iwapo watakuwa na umoja na mshikamano, wachague watu watakaowaongoza katika kipindi hicho kigumu.
“Ningetamani kuongea mengi lakini kanuni zinanibana, Mwanza na kanda ya ziwa ninaifahamu pamoja na changamoto zake, kama mambo yakiwa mazuri, nitakuja kuzungumza tuone tutafanyaje ili Mwanza iwe nzuri,” alisema.
Aidha, Lowassa alisema mtaji wa mwanasiasa yeyote ni watu, hivyo kutokana na mapokezi makubwa aliyoyapata Mwanza, ana imani uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mzuri zaidi.
“Lazima Watanzania watafakari nchi yetu kwa sasa imepata gesi, hivyo gesi hiyo inaweza kututajirisha ama kutufukarisha…mataifa makubwa yanaweza kuvuna na kutunyonya maana inaweza kuwa ni laana ama baraka kwetu,” alisema.
CHANZO: NIPASHE


No comments :
Post a Comment