dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, July 30, 2015

CCM msitafute mchawi, mwajiloga wenyewe


KATIKA toleo 414 la gazeti hili niliandika kuhusu umuhimu wa CCM kuendeleakunoa kisu na kukata. Leo napenda kuendeleza pale nilipoishia kwa kuwa naamini CCM ikizembea au kudanganyika yenyewe ndio itakatwa huko mbele ya safari. Afya ya CCM ni mbovu! CCM inaumwa! Bila tiba ugonjwa utaongezeka na hatimaye itajiunga na nduguze kina KANU na UNIP kuzimu. Natumai madaktari na ndugu wa CCM watafungua masikio!
Hakika maradhi ya CCM yametoa dalili kubwa na za kutisha. Haijapata kutokea jamii ya kitanzania achilia mbali wanachama wa CCM ikashuhudia usaliti, dharau na kiburi cha hali ya juu kilichojitokeza katika chama kama hiki kilichoshuhudiwa katika mchakato ulioishia na kuteuliwa kwa Dk. John Magufuli na umati kukatwa japo mmoja ndio inaonekana alisikia uchungu zaidi ya wenziwe.
Katika makala hii nitajaribu kufafanua ni nini hasa kilipelekea CCM ikaugua kiasi hiki? Pia nitajaribu kupendekeza tiba ya kila ugonjwa kwa kadri ntakavyojaliwa. Kwa kawaida ili mtu aambukizwe ugonjwa lazima akosee masharti ya afya bora. Lazima afanye kosa. Ni wachache sana wanaambukizwa bila kufanya kosa au kukiuka kanuni za afya bora.Kama nilivyosema katika toleo la 414 kosa la kwanza ni CCM kujaribu kukata halafu ikaacha. CCM ilifanya kama mgonjwa mzembe. Iligundua ni kiungo gani kilichomsababishia maambukizi ikaenda hospitali kwa nia ya kukata kiungo lakini ilipoona kisu cha daktari ikatoka mbio kurudi nyumbani! Hii ni pale CCM ilipotaka kuvua magamba na ikaambiwa gamba litaishia kiunoni! Na CCM ikanywea. Badala yake CCM ikaja na visingizio vya kuhalalisha kitendo chake cha kushindwa kukata. Waliodhamiriwa kukatwa wakachekaa! Vichwa vikafura! Wakaonyesha jeuri! Wakanyakuwa uongozi wa Kamati nyeti za Bunge! (sawa na ugonjwa kuongeza kasi ya kushambulia mwilini)! Likafika zoezi la kuandika katiba mpya mmoja akapewa jukumu la kuongoza kamati ya uandishi! Magamba yakajaa kiburi kupita maelezo. Yaani wale wale waliokusudia kuwavua gamba ndio haohao wanachama wao wakawachagua bungeni kuongoza kamati na mambo nyeti! Hata ingekuwa wewe na mimi ungeamini uko juu, juu tena juu zaidi! Ugonjwa ukakolea mwili mzima! Ndio maana tukashuhudia viungo vibovu vikipewa nafasi kugombea urais kwa tiketi ya CCM! Na kiungo kimoja kwa jeuri kabisa kikasema tena kwa sauti kuuubwa NIKATE UONE! Na kiungo kingine japo kimeona mwenziwe kakatwa nacho wala hakiogopi! Kinasema hadharani daktari alikosea! Kinadai mgonjwa akakiangukie kiungo kilichokatwa la sivyo eti mgonjwa atakufa! Usoshalisti mamboleo! Perestroika ya aina yake!
CCM ikitaka kupona ugonjwa huu ni lazima iondoshe viungo vyote vilivyo na maambukizi. CCM isiangalie kiungo hiki huko nyuma kilimsaidia vipi! CCM isidanganyike kuwa ikikata viungo hivi itakufa! Hakika ikiviacha ndio kaburi litakuwa jirani. Viungo hivi tayari ni vigonjwa! Vinaweza huko mbele ya safari kuamua kufa na mtu! Hivi tujiulize hivi: viungo hivi vigonjwa vikiachwa nwilini na kupakwa vaselini na pafyumu ili visinuke halafu vikapitishwa kugombea ubunge na vikaamua kujikata vyenyewe kabla ya kugombea au baada ya kupata ubunge CCM italia na nani?! Utakuwa msiba wa mnywa gongo! Majirani watakuja kufukia na kushika hamsini zao.
Kosa la pili la CCM ni kuendelea kumtambua mwanachama na kiongozi aliyelazimika kuachia cheo kutokana na kashfa tena kashfa iliyoibuliwa na wabunge wake wenyewe. Mtu huyu CCM inaendelea kumtambua kama mstaafu! Yaani yeye na kina Msuya, Warioba, Salim ngoma droo! Ni matusi ya wazi kwa mawaziri wakuu wastaafu wa kweli! Nani anadanganywa hapa? Hivi CCM haioni hili lilifanya mtu aamini anaogopewa? Hivi kina Nalaila Kiula, Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, Profesa Ana Tibaijuka nao ni waastaafu?! CCM iliogopa nini kumwambia 'bwana ee wewe umeachishwa au umefukuzwa au umestaafishwa kwa manufaa ya umma tupishe'! Leo CCM isingehangaika!
Huko mbele ya safari ikitokea kiongozi wa CCM kafisadi tumwambie dhahiri shahiri ‘wewe fisadi, ishia bila mafao’. Na tusiishie hapo tumpeleke Kisutu fasta! Leo hii msingeambiwa mbona hamjampeleka mahakamani? Kuitisha mkutano wa wazee na kudai mwenzetu kapata ajali ya kisiasa ni kupulizia pafyumu kidonda kilichooza! Sasa sijui tuseme ajali za kisiasa zimekuwa nyingi? Mwalimu aliwahi kusema kwa kizanaki ‘mficha maradhi kilio humuumbua’! CCM huu ni wakati wa kuitupa dampo dhana ya ‘huyu ni mwenzetu’! Awe mwenzenu kwa utumishi uliotukuka si kwa ufisadi.
Kosa la tatu lililosababisha maambukizi ni kuruhusu watu ambao walitaka kuwavua kama gamba kwa shutuma za ufisadi na kuharibu taswira ya chama kuendelea na nafasi zao ndani ya chama! CCM iliruhusu waliomsababishia maambukizi shughuli ya kumtibu! Ndio maana tunasikia na kusoma kuwa kuna mmoja kupitia upenyo huu wa kuruhusiwa kumtibu mgonjwa aliwahi kumuuliza Mwenyekiti wa chama kikaoni eti ni nini alifanya kuhusu kashfa ya umeme ambacho Mwenyekiti kama mkuu wa nchi hakujua!? Huu ni ujasiri unaotokana na mtu kujiamini kuwa hakuna wa kumfanya lolote! Mtu anapata wapi ujasiri wa kumzodoa Amiri Jeshi Mkuu hivi? Iweje chama kitoe fursa ya Mwenyekiti wake kuzodolewa hivi? (labda watuambie ni porojo haikutokea?). Tunaambiwa pia kutokana na CCM kuacha magamba ndani ya nafasi za uongozi za chama Katibu Mwenezi naye aliwahi kuzodolewa hivihivi kikaoni! Eti aliambiwa anaropoka ya kichwani mwake badala ya maamuzi ya vikao! Utadhani Katibu Mwenezi wa chama anatakiwa awe bubu, asitumie ubongo wake hadi vikao vikae!Imamu akilewa au padre akiiba sadaka na muumini au kiongozi mwandamizi akimuona si lazima vikao! Ataelezwa au kuumbuliwa na aliyemwona hapohapo! Vikao vitafuata! Akiumbuliwa itakuwa ajabu akadai kikao kilikaa lini? Kiburi hiki kilitokana na CCM kubakiza maimamu walevi na mapadre wapora sadaka madhabahuni! Nusura misa na sala iharibike kama si wazee wa usharika na maulamaa kuingilia kati! Leo tuna rasimu ya katiba ambayo mwandishi mkuu ni mmoja kati ya viungo vigonjwa vilivyoacha kukatwa. Hilo peke yake linaondolea ile rasimu udhu! Hivi CCM ilinufaika na nini kumwachia kiungo walichotaka kukikata kisimamie mchakato wa kuandika rasimu ile? Hivi ukimwamini mtu na umpe jukumu zito vile ilikuwaje ukataka kumvua kama gamba? Umtuhumu mtu mwizi wa mahindi yako shambani tena kwa sauti kuubwa halafu wiki inayofuata unampa kazi ya kuvuna mahindi shambani? Si jamii itakuona hamnazo? CCM lazima ifanye tathmini na kujua ni nini kilifanya kikawaamini magamba kiasi kile? Ni woga tu au kuna watu waliwakingia kifua? Kama kuna watu walicheza u godfather hawa nao si wa kuonea huruma hata kidogo. Kama ulikuwa uoga tu itafiti ulisababishwa na nini ili irekebishe.
Kosa la nne na hili lina historia ndefu kidogo ni kuruhusu fedha iwe nishati mbadala katika chaguzi. Ikubali ikatae CCM ilibatiza rushwa kuwa TAKRIMA. Tena mwasisi aliyetangaza jina jipya la ubatizo kutoka rushwa na kuwa takrima safari hii naye alikuwepo kwenye kundi la wasaka madini linaloitwa IKULU MINING & PROSPECTORS CO LTD. Ikulu imegeuka investment opportunity! fursa ya uwekezaji. Kutokana na chama kikongwe kupeleka mwangi chanya (negative signal) kuwa sasa ruksa kutumia fedha kukarimu basi boksi la pandora (pandoras box) ilifunguliwa. Jini la manoti likatanda mashariki na magharibi, kaskazini na kusini! Sasa hapendwi mtu wala sera! Noti tu! Kitaalam mgonjwa anayeugua ugonjwa huu anaitwa MEGALOMANIAC! Anapenda pesa kuliko anavyojipenda!Katika ile kampuni ya IKULU MINING & PROSPECTORS CO LTD walikuwepo MEGALOMANIACS sugu! Unajiuliza hivi waziri wa nchi ya Tanzania anawezeje kuandaa mabasi namna ile?! Nchi nyerere alitawala miaka 24 akatoka bila Coaster! Kuna mgombea alinichekesha! Alitengeneza VIPEPERUSHI alipoenda kuvigawa watia saini wakamuuliza 'vya nini?' Akawaambia 'ili msome maelezo mnijue vizuri kabla ya kunipa sahihi zenu'. Wakamjibu 'hatuna shida ya VIPEPERUSHI tunataka 'VIPEPERUSHWA'! Alichoka! Ukishakuwa na viongozi megalomaniacs dini ya kuabudu fedha inasambaa kwa kasi. Sasa taifa lina watu wasioamini sifa za mgombea! Wanaamini mgombea mwenye fedha! Awe ana uwezo au hana kwao si dili! Wananchi malofa lakini nao wamebatizwa u MEGALOMANIAC! CCM lazima ikiri kosa hili na ilitafutie muarobaini. Kwa bahati mbaya sana popote pale duniani ambapo watu wameaminishwa wana haki ya kuvuna fedha wakati wa uchaguzi imekuwa vigumu sana kurekebisha bila kuchukua hatua madhubuti. YUDA ESKARIOT hakuwahi kuacha kupenda pesa! Jini la manoti halirudi kwenye chupa kirahisi! Huvutia sana! Hata wazee wa ukoo waweza kulewa wakatetea watu waovu. Sasa CCM ina mzee ambae kakamatwa kisawasawa na jini manoti. Si dalili njema kwa ukoo. Hebu tufikiri kidogo hivi: hivi maulamaa na wazee wa kanisa wa CCM wangemuiga mzee mwenzao ingekuwaje siku ile pale Dodoma? Pesa ingeshinda! Megalomaniac mkuu (THE GRAND MEGALOMANIAC) angeweza kutinga ikulu! Nchi ya Mwalimu ingegeuka a Megalomaniac State!
CCM nyie ndio mna serikali na vyombo kama Polisi, TISS na Takukuru! Iweje rushwa ionwe hadi na watoto vyombo hivi vikae kama vilipigwa sindano ya usingizi ya nusu kaputi? Nani huyu aliwapa hawa waheshimiwa nusu kaputi? Ya nini kuwa na Takukuru inayosinzia kwenye zoezi muhimu kama hili?!
Gonjwa hili (megalomanianism) ni gumu kutibika sawa na lile la madawa ya kulevya! Linashambulia mishipa ya fahamu ya taifa, viongozi na watu wake! Linahitaji jitihada za ziada kutibika. Nijaribu kusaidia tiba ya gonjwa hili hivi: kama ambavyo kumtenganisha teja na wauza unga inasaidia kumtibu teja katika gonjwa la hela inasaidia kumtenga mpokea na mtoa hela! Tunaweza kuweka utaratibu wa kampeni ambao unaondoa au kupunguza mwingiliano baina ya mtoa na mpokea hela wakati wa kampeni. Inaweza isitokomeze lakini kwa hakika itapunguza gonjwa. Njia mojawapo ni kutumia teknolojia; kuna nchi ya Afrika iliyofanya uchaguzi mapema mwaka huu na ilipunguza sana gonjwa hili kwa kuwapangia wagombea watano waliojitokeza kugombea urais kipindi cha tv ya taifa (TVT) cha dakika 15 kuhutubia taifa. Ilipunguza sana utiaji na upojeaji hongo. Hakika baadhi ya wananchi waliopiga simu badala ya kuhoji sera zao walilalamikia utaratibu eti unawakosesha kipato! Ilikuwa kiashiria kuwa rushwa imepungua! Tunaweza kuuboresha kwa kuwapa vipindi vingi zaidi na muda mrefu zaidi kitueleza sera zao. Tunaweza kuwapa vipondi vya redio vinavyosikika nchi nzima. Baada ya hapo twende kuwapigia kura. Mtu anaweza kudai watatoa rushwa kabla; lakini tukumbuke wagombea wengi hutoa rushwa wakati wa kampeni na si kabla ya hapo! Rushwa uliyotoa mwaka kabla ya siku ya kupiga kura inaweza isimsaidie mtoa rushwa! Mpokeaji atakuwa kesha ila na bado ana shida zake! Na hapa ndio nitoe tiba ya pili ya gonjwa hili. Wengi wa wagombea wanakuwa na hela nyingi za mkupuo mara tu wanapomaliza ubunge! Bulungutu la mafao ya ubunge ambalo kila kipindi linaongezwa ndilo linachochea rushwa! Tusipodhibiti ipo siku bulungutu hili litakuwa bilioni au zaidi. Kama kweli CCM ina dhamira ya kweli ya kuondosha u megalomaniac basi no vyema bulunguti hili likafutwa. Licha ya kwamba ndio limegeuka HONGO FINANCING BANK halina mantiki. Hivi malipo ya kustaafu si analipwa mtumishi aliyemaliza utumishi? Iweje malipo haya ya kustaafu alipwe mtumishi ambae anaweza kuendelea na utumishi?! Yaani mtu alipwe mafao ya kustaafu utumishi, arudi kutumika alipwe tena mafao makubwa zaidi ya kustaafu? Ukiachilia mbali udhaifu wa dhana hii ya kustaafu kwa wabunge wetu kuna miongoni mwao ni watumishi serikalini na wengine walishastaafu huko walikokuwa kabla ya kuingia bungeni. Hivi ni akili ya aina gani hii? Waziri apokee mafao ya kustaafu ya ubunge na apokee mafao ya kustaafu serikalini? CCM tuondosheeni wizi huu wa staili ya Kiboroloni!
Nipendekeze tiba ya tatu: CCM tusaidieni kuweka ukomo wa ubunge. Kama rais ana vipindi viwili (na si lazima avimalize) kwa nini mbunge iwe sesa?! Hivi mtu atakayestaafu ubunge mara 3 au 4 na kila anapostaafu akapokea milioni 238 ataacha kuhonga?! CCM hili lingekuwepo wala msingesumbuliwa na hawa waliowasumbua safari hii. Wangekuwa vijijini wakicheza na wajukuu au kwenye biashara zao. CCM tusaidieni kuondoa USULTANI kwenye ubunge kwani nyie ni chama tawala na ndio mliouzaa na kuulea usultani huu. Nyie ndio mumesababisha wabunge masultani kufoka eti kuna watu wanajipitisha kwenye falme zao! Mnajiua wenyewe! Vijana wanataka kushiriki siasa lakini wanaona sura zilezile muaka nenda rudi! Kwenye kinyang’anyiro wanazidiwa feza na masultani!
Kosa la tano ambalo limeathiri afya ya CCM kwa kiwango cha kutisha ni kuruhusu na kupalilia siasa za mitandao na makundi. Mitandao au syndicate ni gonjwa sugu! Haliponi kwa urahisi. CCM inayajua makundi na hii mitandao na ukiwasikiliza viongozi wake hata huyu mteule wa sasa inaamini kuwa ni ukuaji wa demokrasia! Eti ni lazima pawe na makundi katika kutafuta uongozi. Utawasikia: ‘mmoja akipatikana makundi yanavunjwa tunarudi kuwa kitu kimoja’! Najiuliza hivi mwaka alichaguliwa Mwinyi au Mkapa kulikuwa na makundi yapi? Maana makundi yanaweza kuundwa chini ya chama kimoja na ndani ya mfumo wa vyama vingi. CCM inapaswa kukaa chini na kujiuliza hivi ni nini kilizuia makundi enzi zile na nini kimechochea makundi sasa?! Ni nini kinafanya mjumbe wa NEC au Mkutano Mkuu ambaye atashiriki kupitisha majina anatoka hadharani kujiunga na kundi?! Ukuaji gani wa demokrasia sampuli hii? Ukisharuhusu siasa za kimakundi hutaweza kuzuia siasa za makundi ya kikabila, kijimbo, kidini kimaslahi binafsi! Iko siku tutakuwa na kundi la magaidi katika siasa kwa kudhani makundi ni lazima na eti yatatoweka kama moshi! Kundi liwe moja tu kundi la CCM toka ALFA na OMEGA! Chama kinacholea makundi kinajitakia kilio cha bure. Makundi hayafi! Ukiona makundi yanakufa basi kila kundi limepata! CCM ijiulize je makundi yote yamepata pale Dodoma? Haiwezekani kundi limerudi tu nyuma kupanga mashambulizi kabla ya oktoba au 2020 au 2025? CCM itafute muarubaini wa kuzuia kuibuka makundi. Je inatokana na utaratibu mbovu wa kupata wagombea? Je ni udhaifu wa kusimamia chama? Je ni uwepo wa waunda makundi ndani ya chama? Je ni kasoro katika Baraza la Mawaziri? Maana iweje watu walio katika Baraza moja la Mawaziri wajae kugombea kiti kimoja? Si watu wazima hawa? Wameshindwa kuelewana ndani ya Baraza? Sasa wamekosa wakikutana tena ndani ya Baraza na ikawa walichezeana rafu? Mchezo huu ni hatari! Ni mauti yetu huko mbele ya safari. Kuwa na Baraza ambalo watu wamewekeana kinyongo si busara hata kidogo. Tumeona baraza lililopita makundi yakihasimiana! Ipo siku kutakuwa na mabaraza mawili rais aamue ajiunge na baraza lipi!
Kosa la sita ni CCM kusimamia dhana ya kudharau elimu! Mwasisi wa CCM alikuwa muumini mkubwa sana wa elimu. Alisomesha vijana wengi mno na yeye mwenyewe akitumia muda mwingi kusoma na kuandika vitabu. Mwasisi huyu kuna kipindi alisomesha hadi wazee tukatambulika vyema ulimwenguni kwa kupunguza ujinga. Sasa inashangaza sana chama chake kinatukuza kiwango cha kujua kusoma na kuandika kama kiwango muafaka cha mtu kupewa uongozi katika karne hii ya 21 na kukiwa na wataalam lukuki waliosomeshwa na taifa hili! Kisingizio kikubwa ni haki za binadamu! Utadhani kuongozwa na mjinga ni haki yetu ya binadamu! Ni kutafsiri vibaya haki za binadamu. Hivi kwa kuwa binadamu ana haki ya burdani na kucheza kwa mujibu wa mkataba wa haki za binadamu wa umoja wa mataifa wa mwaka 1948 (UN HUMAN RIGHTS CHARTER OF 1948) basi mtu mwenye kitambi adai kuchezea TWAFA STARS (inayoitwa Taifa Stars)? Akikataliwa adai haki yake ya binadamu imevunjwa? Nilishangaa sana yule dada eti dokta akitoa hoja hii pale BMK na akapigiwa makofi hasahasa na wabunge wa CCM! Ajabu kabisa! Ni CCM hiyohiyo imeweka kiwango cha elimu ya chuo kikuu kwa rais! Ina maana ilivunja haki za binadamu? Hivi ndio kumuenzi Mwalimu huku kwa kudharau elimu?
Kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia ni upuuzi kuwa na mbunge anayemudu kusoma na kuandika tu! Miswada inayoenda bungeni sasa si ya 1977! Sasa ni ‘geo engineering’, ‘biofuels’, ‘nano technology’, ‘biotechnology’, na mingine kama hii! Kujua kusoma na kuandika haifanyi kazi tena! . Sasa ni mikataba na makampuni ya kigeni si na NMC, NHC,na mashirika ya umma. Unahitaji zaidi ya kusoma na kuandika kama mbunge. Ukitaka kujua kiwango cha elimu ni kidogo bungeni sikiliza udhaifu wa hoja, matusi, viti kuwa tupu, kutokujua kanuni za chombo chao wenyewe, ukimya wakati miswada ya kisayansi inaposomwa, kupiga soga huku mijadala ikiendelea, kusinzia bungeni, n.k. Uwezo wa elimu mdogo! Wataacha kuimba taarabu, kutukanana, kugonga meza na miguu kama mazuzu? Mtu unajiuliza hivi mbunge wa kujua kusoma na kuandika anamudu vipi ujumbe wa Bodi? Hivi akienda nje safari za mafunzo anajifunza nini? Kusoma na kuandika? Mbunge wa kujua kusoma na kuandika akienda London anajifunza nini?! Akiingia House of Commons anaelewa kitu au ndio kina “yes yes mzungu kala fenesi?” Hebu tuacheni huu utani unaokifu!
Hoja nyingine ya kipuuzi iliyotolewa eti ukiweka kiwango cha juu utanyima watu ajira! Watu wazima wanaongea utadhani hawana ubongo? Au ni kwa kuwa ubunge umegeuzwa kuwa ajira? Hivi kuna nafasi ngapi za ubunge ili tuzitumie kupunguza tatizo la ajira nchini?! Hivi nafasi hizo za ajira zitapatikana kwa wengi ilhali karibu sura ni zile zile kila uchaguzi? Hata viti vya upendeleo wanaopendelewa ni walewale kila mwaka!
Hoja nyingine nayo muflisi wanasema hata wasomi wanatuangusha! Ni kweli kuna wasomi hovyo kabisa. Lakini hivi ukimchukua dereva aliyesomea VETA lakini mlevi akiangusha gari utadharau madereva wote waliopitia VETA ukachukue madei waka Manzese Stendi?
Mtu unawaza hivi hawa wanaoshabikia sifa ya kujua kusoma na kuandika kwa nini wanapeleka watoto wao shule tena za bei mbaya? Kwa nini serikali ya CCM inajenga vyuo kama kujua kuandika na kusoma inatosha?! Hivi mbunge akijua kuandika na kusoma dereva wake aweje? Asiwe ameenda shule kabisa ili walau kuwe na tofauti? Tusidanganyane! CCM imekumbatia wenye kiwango kidogo cha elimu na kwa kuwa ndio wako kwenye Bunge kwa wingi wanalinda maslahi yao! Maamuzi ya BMK ni ya hawa wanaolinda maslahi yao! Hayapaswi kuwa ya chama kama CCM.
CCM pia inaogopa ikidai kiwango cha juu inadhani itaonekana si ya wakulima na wafanyakazi! Dhana potofu tu! Sasa wakulima wengine wana digrii! Wafanyakazi ndio usiseme! Vijana wasomi mitaani wamejaa kibao na madiploma na madigrii yao ya nini kukumbatia vihiyo?
Tatizo hili limejikita hadi kwa ngazi za watendaji wa CCM wa ngazi mbalimbali na wajumbe wa mkutano mkuu. Hawa ndio sura ya chama kwa wananchi! Sura kwa wananchi ni ya kujua kusoma na kuandika! Watendaji wengi wa ngazi za mikoa na wilaya ni adui wa wasomi katika maeneo yao. Hawawapendi wasomi kwa kuwa wana inferiority complex! Hawa ndio utawasikia wakidai ‘wasomi wana matatizo, wanajifanya kujua kila kitu’! Waingereza husema ‘if you think education is a problem try iliteracy’! Ni viongozi mazoea! hawana ubunifu!
Vijana wa leo ni tofauti na wa 1977. Hawezi kukubali kuongozwa na kihiyo. Mnajikosesha wanachama vijana wenye elimu kwa kukumbatia wajua kusoma na kuandika.
Tunaingia EAC sasa, hivi wenzetu wanapeleka wa kujua kusoma na kuandika kule? Kwa nini CCM inasuasua au kupata kigugumizi kwa hili? Ni vipi chama kikongwe kama CCM kikumbatie elimu ya kusoma na kuandika? Mbona wapo wanachama wengi tu wenye sifa au wenye watoto wenye sifa hizi? Inawaogopa kina nani? Wabunge na wajumbe wa NEC na Mkutano Mkuu? Mbona kiwango cha elimu cha urais kilipowekwa tuliona hata wazee wakipiga shule?! Rais ambaye ni mwenyekiti wao awe na elimu lakini huku chini asaidiwe na mbumbumbu?! Hivi CCM haijui mbumbumbu wengi ndio hawa ni rahisi kughilibiwa na kuchoma kadi hadharani? Yaani hata ubongo wa kufikiri kuwa nirejeshe kadi kwa wenyewe hawana. Kukitokea wimbi la kutimkia kwingine wengi watakuwa hawa wasio na elimu. Ni rahisi saaana kurubuniwa. CCM itizame wajumbe wake wa NEC na Mkutano Mkuu waliorubunika kwenye mchakato, itaona wengi wao ni jamaa wa kuandika na kusoma! Huko mbele ya safari inaweza kuwa balaa. Imekaaje hii ndugu wa Sekretariati?
Hata msimamo wa kiwango cha elimu kikatiba msione haya kuurejea! Serikali yenu iliwahi kuwapa ultimutum watumishi wa serikali angalau form four! Ikawapa muda na atakayeshindwa aondoke! CCM igeni serikali yenu. CCM ni chama kikongwe kuingia karne ya 21 na wa kusoma na kuandika ni fedheha na hatari!
Kosa la saba la CCM ni kuachia siasa ziendeshwe kwenye nyumba za ibada. Hiki ni kipindi hadi watu wamechinjana na kumwagiana tindikali. Ni kipindi nyumba za ibada zimepigwa kiberiti. Huku haya yakiendelea kiongozi wa CCM alikuwa anachanja mbuga kanisani na misikitini akiendesha harambee, kuzindua helikopta na kutoa misaada! CCM kimyaa! Utadhani kiongozi yuko ziara ya kuzindua matawi ya chama! Ni hatari kuingiza udini kwenye kampeni za kisiasa hasa kampeni za kusaka uongozi. Ipo siku tutapiga kura kidini tukiendelea hivi. Almanusura nyongo itumbuke! Kwanza alitoka ‘nabii’ akatukana wenzie lakini babkubwa ni pale mgombea alipofananishwa na Mtume Mohamed (SAW) na Joshua! CCM msione haya hata kidogo kukemea siasa za aina hii. Nyie ndio wenye serekali inayo sajili taasisi za kidini, ndio mna vyombo vya uchunguzi na dhamana ya kuhifadhi amani nchini. Msiacha watu wacheze karata tatu na amani ya nchi eti kwa kuwa ni mwanachama almaarufu au kwa kivuli cha imani. Hivi tuwaulize CCM udini huu si mumeulea? Hivi viongozi wa CCM waliomiminika Loliondo kunywa kikombe cha babu ni sekretariat iliwaagiza? CCM haikuona upotofu na hatari ya watendaji wake kujihusisha na tiba ya ndoto ya kiimani? CCM haikuona umuhimu wa kuwaonya na kusitisha zile safari?!
Kosa la nane ni CCM kuruhusu bunge kuendeshwa kihuni. Uhuni ulianzia pale uchaguzi wa spika ulipoendeshwa kihuni. Kwa mara ya kwanza nchini na duniani ili mtu awe spika wa bunge la JMT ilibidi aidha azaliwe mwanamke, azaliwe mwanaume ajibadili jinsi hospital (transgender) au azaliwe mwanamme lakini adanganye kuwa ni mwanamke (katika historia za papa kuna papa mwanamke aliyejifanya ni mwanaume kwa hiyo inawezekana kutokea)! Kwa chama kikongwe kama CCM kubariki upuuzi ule ni jambo la fedheha sana! Mwalimu angekuwepo angesema ni uteuzi wa spika kikaburu! Upuuzi huzaa upuuzi!Hakuna ubishi bunge ambalo spika aliteuliwa kikaburu liliendeshwa katika kiwango cha chini mara kadhaa kupita kikao cha walevi watani zangu wa kule Rombo! Wenye kupaswa kulinda kanuni wakawa wavunja kanuni! Wenye kutukana wakachochewa kumwaga radhi! Alimradi hili halikuwa Bunge tukufu! Iweje muanze shughuli kwa dua na muda mfupi baadae mtukanane matusi ya nguoni!? Kusema ukweli japo matusi yaliryshwa toka pande zote ni dhahiri wa CCM walitoka na kombe la ushindi! MATUSI CUP! Kapteni kutoka Jimbo la Mtera! Mbunge mwenye jina la kiongozi wa CCM aliyetumikia taifa kwa uadilifu mkubwa Mzee JOB! CCM haikupaswa kuacha hali iendelee vile! Ilipaswa kuwaita wabwaga matusi wake na kuwaonya! Kwa kukaa kimya imepatikana picha aidha CCM inafurahia matusi au imewatuma! Hii ni CCM ya Nyerere au ya Nyenyere? Ni vyema CCM ikawatupa wote walioshiriki MATUSI CUP na ikatoa semina elekezi kwa wajao kuwa haitavumilia mitambo ya matusi! Ni vyema CCM ikahakikisha uchaguzi wa spika kikaburu haurejewi tena! Muasisi aliwaasa ukitenda dhambi ya ubaguzi ni sawasawa na kula nyama ya mtu, huachi! Ila nadhani hamjanogewa au kulaaniwa kiasi hicho!ACHENI dhambi hii.
Kosa la tisa ni CCM kuendelea kukumbatia nafasi za upendeleo bungeni. Enzi za Mwalimu nafasi za upendeleo zilikuwa na umuhimu. Nia ilikuwa kustawisha uwakilishi wa makundi yaliyo mazingira hatarishi (vulnerabke groups). Kulikuwa na makundi ya wazee, wazazi, vijana, wa mama, wakulima na wafanyakazi. Mazingira yamebadilika sana ukifananisha na wakati ule kiasi ambacho dhana ya upendeleo imepoteza maana. Sasa kwa mfano uwanja wa siasa unaruhusu kila mtanzania mwenye sifa kushiriki kuomba uongozi. Elimu ya makundi haya pia imeboreka kiasi wengi sasa wanajua haki zao. Lakini dhana hii ya upendeleo pia imechuja kutokana na jinsi upendeleo huu unavyoendeshwa. Mathalan tumeshuhudia nafasi hizi za upendeleo zikipewa sura zile zile mwaka nenda mwaka rudi! Upendeleo ndani ya upendeleo! Sasa aliyependelewa miongoni mwa wanawake hawakilishi tena kundi bali anajiwakilisha mwenyewe na kikundi kinachompendelea kila uchaguzi.
Mfano mwingine ni kuwa baadhi ya makundi yameachwa! Pia kuna makundi mapya yamejitokeza. Hali hii imepoteza maana ya kupendelea! Kwa nini makundi mengine yaachwe kama kupendelea ni jambo zuri? Utapendelea makundi mangapi? Wakati umefika wa kuachana na huu utaratibu wa viti vya upendeleo. Umepoteza maana na unatumika vibaya. Si siri wengi wa wabunge wa mipasho, matusi, elimu duni, watoro, n.k. wanatoka kundi hili. Kama hofu ni kukosekana uwakilishi wa wanawake si mmepitisha 50:50? Hata hili lilipitishwa kwa shinikizo tu watu wasionekane ni wapinzani wa usawa wa kijinsia. Kujipendekeza tu na kutafuta misifa! Hivi kulikuwa na mantiki gani ya kuacha vijana, wakulima, wafanyakazi, wazee, walemavu kwenye mgao?! Tuna uhakika gani kwenye 50% watakuwepo? Hivi wakichaguliwa 50% wanawake wazee, wake za matajiri au viongozi, wasio vilema, wasio wakulima itakuwaje? Halafu tunatoka na kujidai tutakuwa taifa la kwanza kuwa na 50:50! Kama nafasi za upendeleo UWT zimehodhiwa na watu walewale asilimia 50 itamsaidia vipi msichana ambae ameamua kugombea?! Atakuwa msindikizaji! Ukitaka kujua ni maslahi binafsi waambie basi kipindi kimoja au viwili upishe wengine usikie watakavyokusonya! Hebu tuweni wakweli hivi hawa wa nafasi za upendeleo kule bungeni wanapitisha miswada kwa kuzingatia maslahi ya kundi wanaloliwakilisha au maslahi ya vyama vyao? Kila mmoja wetu anajua utii wao si kwa makundi yao ya upendeleo bali vyama vyao! Tunamdanganya nani? Huenda CCM inadhani kwa kuwa kwa sasa inanufaika itakuwa hivyo milele. Ikumbuke ipo siku inaweza kuwa mhanga! Kuna watu wakishika madaraka wanaweza kuweka hata 40:60!
CCM tusaidieni watu wote waachwe waende majimboni kugombea katika uwanja ulio sawa. Milango iachwe wazi kwa makundi yote. Tusiwe na bunge ambalo mtu ameenda mle kwa kuwa tu anavaa sketi au boksa, ni zeruzeru, ni kijana anayevaa mayenu, ana mvi au analima matembele! Tanzania ya sasa ilivyo tukiweka uwanja sawa haitakuwa shida kupata makundi yote. Tena tutapata wanawake, walemavu, vijana, wakulima, wazee na wafanyakazi wenye viwango! Tusiendeshe nchi kana kwamba Desemba 9 1961 ilikuwa jana!
Kwa leo niishie hapa nisimkwaze sana mgonjwa! Ni matumaini yangu mgonjwa na nduguze hawatanichukia kwa kusema ugonjwa unaomsumbua ndugu yao.
Waasalam

 - See more at: http://raiamwema.co.tz/ccm-msitafute-mchawi-mwajiloga-wenyewe#sthash.lde77NRH.dpuf

No comments :

Post a Comment