zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, July 31, 2015

Mambo manne ya Lowassa.

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amechukua fomu ya kuomba kuwania urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku akiwarushia madongo wanaomshambulia kutokana na uamuzi wake wa kujiunga na chama hicho kwani ametafakari na kubaini kuwa ndani ya CCM mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana.
 
Alisema hayo jana baada ya kukabidhiwa fomu hiyo na Mwenyekiti wa Taifa Chadema, Freeman Mbowe, katika hafla iliyofanyika makao makuu ya chama hicho Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi na viongozi wandamizi wa chama hicho.
 
“Wapo watu wanaonishambulia kwa nini nimejiunga na Chadema, lakini wanapoteza muda hawatanirudisha, nimeridhika ndani ya CCM mabadiliko hayawezi kupatikana wakati Watanzania wengi wanataka mabadiliko,” alisema.
 
Lowassa alifafanua kuwa uamuzi wake wa kujiunga na Chadema ni katika kutekeleza maelekezo ya muasisi wa CCM, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyesema Watanzania wanataka mabadiliko wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.
 
Alisema tatizo la umaskini limekuwapo toka mwaka 1961 hadi sasa, hivyo Watanzania walio wengi wanataka mabadiliko na kwamba vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimejipanga kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu pasipo kutumia lugha za kuudhi na kejeli.Lowassa alisema kitu cha msingi ni kushikamana kuhakikisha ushindi unapatikana na kwamba wananchi ambao bado hawajajiandikisha wakafanye hivyo na wale waliojiandikisha watunze shahada zao za kupigia kura.
 
“Nafurahi kwa keshima mlionipa, najiandaa kufanya kazi iliyotukuka na kazi itakayotuletea ushindi na Watanzania ushindi,” alisema.
 
ALIVYOWASILI MAKAO MAKUU CHADEMA
Lowassa aliwasili saa 6:40 mchana akiwa na mkewe, Regina, katika gari aina ya Nissan Patrol yenye namba T 841 CYP na T 878 CFU lililokuwa na walinzi wake.
 
Lowassa baada ya kuteremka, alitembea kwa miguu huku akiwapungia wanachama, wapenzi na wananchi waliokuwa eneo hilo.
 
KAULI YA LISSU
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema jina la Edward Lowassa halikupatikana kwa bahati mbaya bali chama kilifanya utafiti kwa zaidi ya miezi mitatu ili kumpata mtu sahihi anayeweza kugombea urais mwaka huu.
 
Lissu alisema kazi kubwa ilifanyika kumpata Lowassa na kwamba siku za nyuma hawakuwahi kutangaza kwa kuwa mipango ilikuwa haijakamilika na kwamba viongozi wote wa juu wa Chadema walishiriki katika mchakato huo.
 
"Tulikaa katika vikao vya kamati kuu mpaka saa sita usiku na haukuwa uamuzi rahisi, lakini pia haukuwa wa kushtukiza," alisema. 
 
Lissu alisema katiba ya nchi ibara ya 39(1)C, inasema kuwa mtu hatagombea urais kama siyo mwanachama wa chama cha siasa na ibara ya 39(1)E inasisitiza sifa za mgombea ni lazima asiwe amepatikana na kosa la kukwepa kodi katika kipindi cha miaka mitano, huku akisisitiza kwamba Lowassa hana 'criminal record' (rekodi ya uhalifu).
 
Alisema Lowassa hana kosa linaloangukia katika ibara hizo na hivyo anayo sifa sitahiki za kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao.
 
Lissu ambaye alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki alisema, kwa sasa kuna majimbo 265 ya uchaguzi na kwamba Ukawa wanahitaji kupata wabunge wasiopungua 133 ili kuwawezesha kuunda serikali ikiwamo kuteua jina la Waziri Mkuu.
 
Aidha, alisema baada ya Lowassa kupitishwa rasmi na chama atakuwa huru kusafiri mikoa yote kujitambulisha na kwamba akifanya hivyo hatakuwa amevunja sheria, bali atakuwa anafanya kama waliolianzisha ila yeye atalifanya vizuri zaidi.
 
MBOWE ATANGAZA RATIBA
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliweka wazi ratiba ya vikao vya chama hicho ambavyo vitapitisha majina ya wagombea ubunge na rais.
 
Alisema kuanzia Agosti 2, mwaka huu, kamati kuu itakutana, Agosti 3, Baraza Kuu la chama hicho, Agosti 4, kikao cha Mkutano Mkuu wa chama hicho na kuanzia Agosti 5 hadi 7, kamati kuu itakutana kwa ajili ya kuchambua na kupitisha wagombea wa ubunge.
 
Katika hafla hiyo, Mbowe alimkumbusha Lowassa kusalimia kwa salaam ya chama hicho ya 'Peoples Power' ambayo mwanasiasa huyo aliyejiunga na Chadema akitokea CCM aliitikia wito huo na kuitoa kwa zaidi ya mara tatu huku wanachama wakiitikia 'Pawaaaa'.
 
MATSON CHIZII ANENA
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM, Matson Chizii, aliibuka na kuahidi kuwapa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mbinu za ushindi.
 
Alisema anaijua CCM kwa kuwa amekuwa kada wa muda mrefu na kwamba anazijua mbinu zote zinazotumiwa na CCM kupata ushindi na kwamba atazitumia mwaka huu.
 
Chizii alisema anatarajia kuhamia Chadema muda wowote na kwamba anachosubiri ni tataribu za kichama aweze kukabidhiwa kadi rasmi.
 
“Mimi sina tena haja na CCM, nimekuwa msaidizi wa Lowassa kwa kipindi kirefu na mimi nitahamia Chadema kama alivyofanya kiongozi wangu,” alisema.  
 
Akizungumza na NIPASHE makao makuu ya Chadema jana alipokuwa amehudhuria hafla fupi ya Lowassa kuchukua fomu, Chizii alisema Chama cha ukombozi ambacho ni CCM kimetikiswa.
 
Alisema mwaka huu Watanzania watashangaa kuona kundi kubwa la makada wa CCM likihamia Chadema huku akisisitiza kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mgumu.
 
“Mwaka huu kuna uwezekano wa kuundwa serikali ya mseto ama Ukawa kuchukua nchi, ushindani utakuwa mkali sana,” alisema.
 
Chizii amewahi pia kuwa Katibu wa CCM mikoa mbalimbali ukiwamo Dar es Salaam.
 
Viongozi wa Chadema waliokuwapo mbali na Lissu na Mbowe, ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema; Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Viti Maalum, Anna Komu.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment