.jpg)
Wadadisi wa mambo wanaeleza kuwa hali iliyozikumba baadhi ya nchi za Afrika inaweza kutokea Tanzania mwaka huu.
ZAMBIA
Nchini Zambia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1991 wananchi walikiamini chama cha upinzani cha Movement for Multparty Democracy (MMD) na kumpa nafasi ya Urais mgombea wake, Frederick Jacob Titus Chiluba kuwa rais wa pili baada ya kumshinda Baba wa taifa la Zambia, Kenneth Kaunda wa United National Independence Party (UNIP).
Chama Cha MMD kiliendelea kushinda chaguzi zilizofuata chini ya Levy Patrick Mwanawasa (2001, 2006), ambaye alifariki mwaka 2008. Mwaka 2008 Rupia Banda alishinda uchaguzi kupitia chama hicho hicho cha MMD. Hata hivyo, baada ya Miaka 20 ya kuongozwa na MMD wananchi waliamua kuiondoa madarakani serikali hiyo na kukipa kura chama kingine cha upinzani cha Patriotic Front cha Michael Sata katika uchaguzi wa mwaka 2011.
Mabadiliko hayo ya Wazambia yalitokana na kuchoshwa na uongozi wa chama tawala UNIP.
MALAWI
Mwenendo wa kisiasa kwa Malawi hauna tofauti na Zambia baada ya wananchi kukichoka chama cha Ukombozi cha Malawi Congress Party (MCP), kilichoongozwa na Hastings Kamuzu Banda.Banda alishiriki kwenye uchaguzi uliohusisha vyama vingi mwaka 1993 na kuangushwa na Elson Bakili Muluzi na chama chake cha United Democratic Front (UDF).
KENYA
Siasa za Kenya pamoja na kutawaliwa na hisia za ukabila, lakini wananchi walikiangusha chama chao kwa kuchagua upinzani.
Miaka ya 90 baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi wananchi wa Kenya walionyesha kukerwa na chama kilichowaletea Uhuru cha Kenya African National Union (Kanu).
Kanu iliangushwa na Mwai Kibaki ambaye alikuwa Mtendaji Mkuu wa Kanu baada ya kujiengua kwenye chama hicho mwaka 1991 kutokana na kuhitilafiana na viongozi wenzake na kuunda chama cha Democratic Party.
Hata hivyo, katika uchaguzi wa Urais wa mwaka 1991, Kibaki alikuwa wa tatu na mwaka 1997 alikuwa wa pili na hatimaye baada ya wananchi kuwekeza nguvu zao kwa upinzani, mwaka 2002 Mwai Kibaki alishinda uchaguzi kupitia muungano wa upinzani wa The National Rainbow Coalition (National Alliance of Rainbow Coalition (NARC), ambayo iliiangusha rasmi Kanu na katika uchaguzi mwingine wa 2013 yalifanyika mageuzi baada ya Uhuru Kenyata na Muungano wake wa Jubilee kuibuka kidedea.
Kuangushwa kwa vyama hivyo vya ukombozi pamoja na mambo mengine, kunasababishwa na mambo makubwa mawili, kuhitilafiana kwa baadhi ya makada wenye nguvu ndani ya vyama husika, pili wananchi kukichoka chama kilichowaletea uhuru.
Kuchokwa kwa chama tawala aghalabu ni matokeo ya kujisahau kwa watawala, kukithiri kwa ufisadi, unenvu na kutokujali hisia wala matarajio ya wananchi. Hiki ni kile Mwalimu Nyerere alismema “ulevi wa madaraka.’
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment