ANGALAU wabunge wanne kutoka katika vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mara baada ya kuvunjwa kwa Bunge hili la 10, Raia Mwema limeambiwa. Wabunge hao wamedaiwa kuanza mipango hii na gazeti hili linafahamu kuwa wabunge hao wanne tayari wamezungumza na CCM wiki hii na wakati wowote baada ya kuvunjwa kwa Bunge wanaweza kutangazwa. Gazeti hili limeambiwa na vyanzo vyake vya kuaminika kwamba mojawapo ya sababu ya wabunge hao kurejea CCM ni kutaka watumie fedha zao za mafao ya kustaafu pasipo kuchangia vyama vyao kama ilivyo utaratibu kwenye baadhi ya vyama vya upinzani nchini. Kwa mujibu wa Kamati ya Huduma za Bunge, wabunge wa Bunge la 10 watalipwa kiinua mgongo chao chenye thamani ya shilingi milioni 230 kila mmoja; na wapo wabunge ambao hawataki ‘ kugawana na vyama vyao’ fedha hizo. “ Kwenye vyama vya upinzani kuna utaratibu wa wabunge kuchangia vyama vyao. Vyama kama CUF kwa mfano, wabunge wanakatwa kwenye mishahara yao kila mwezi kwa ajili ya kusaidia shughuli za chama chao. “Ruzuku peke yake haitoshi na ndiyo maana mojawapo ya vyanzo vya mapato vya vyama vya siasa ni michango kutoka kwa wabunge wao. Sasa kuna hofu kuwa wapo wabunge ambao safari hii hawatapitishwa kwa sababu ya makubaliano ya Ukawa kugawana majimbo. “ Mtu anaona bora ahamie zake CCM na achukue kiinua mgongo chake mapema maana akibaki kwenye chama chake atakatwa na ubunge hatapata. Hawa wanne najua watakuja,” kilisema chanzo chetu cha kuaminika ambacho ni mojawapo ya viongozi wa kitaifa wa CCM. Raia Mwema limeambiwa kwamba vyama ambavyo vitaathirika na hatua hii ni CUF na Chadema ambavyo ndivyo vyenye wabunge wengi kuliko NCCR Mageuzi na NLD ambayo haina mbunge hata mmoja hadi sasa. Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema chama chake hakijatoa agizo lolote la kutaka wabunge wake wachangie fedha kutokana na malipo ya mafao ya kiinua mgongo. “Sisi kama Chadema hatujawahi kumlazimisha mbunge wetu achangie chama kwa nguvu. Suala hili limekuwa la maridhiano na wakati mwingine imekuwa kawaida kwa wabunge kukikopesha chama na baadaye wakalipwa. “ Sidhani kama kuna mbunge wa Chadema anaweza kuhama chama chake kwa sababu hiyo. Kama ni kwa sababu nyingine labda lakini hiyo sidhani. Nakuhakikishia kwamba hakuna mbunge yeyote aliyelazimishwa kuchangia,” alisema Mbowe. Juhudi za kumpata Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa hadi wakati tunakwenda mitamboni. Raia Mwema linazungumza na wabunge hao wanne wa Ukawa wanaodaiwa kutaka kujiunga na CCM na yakikamilika majina yao yatawekwa hadharani.
- See more at:
http://raiamwema.co.tz/wabunge-ukawa-wakimbilia-ccm#sthash.R0Ssxm7N.dpuf

No comments :
Post a Comment