
Mgombea huyo atatoka miongoni mwa makada 38 waliojitokeza na kukamilisha mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za uteuzi wa kumpata atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani.
Uamuzi wa kuamua suala hilo ambalo limekuwa likitawala mijadala mbalimbali kwa muda mrefu utafanyika kupitia vikao vya juu vya maamuzi vya CCM ambavyo ni Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), Kamati Kuu (CC) na Mkutano Mkuu.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao hivyo iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Rajab Luhwavi, mfululizo wa vikao vya juu vya maamuzi vya CCM utaanza kwa kikao cha Sekretarieti ya Kamati Kuu ambacho kitafanyika kesho, kikifuatiwa na Kamati ya Usalama na Maadili Jumatano ijayo.
Vikao vingine ni CC ambayo itakutana Julai 9 na kufuatiwa na kikao cha Nec Julai 10 na baadaye kuhitimishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho utakaofanyika Julai 11 na 12, mwaka huu.
Wakati vikao hivyo vinaanza, macho na masikio ya Watanzania yameelekezwa katika mji wa Dodoma ambako kutafanyika vikao hivyo.Mji huo kwa sasa umefurika maelfu ya watu, huku makundi ya wapambe wa wagombea wa kiti cha urais yakipigana vikumbo kutaka kuona wagombea wao wanateuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho.
Jumla ya makada 38 waliofanikiwa kurejesha fomu kabla ya kuchorwa mstari mwekundu wa kufungwa rasmi kwa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo Julai 2, mwaka huu, saa 10:00 jioni wakiomba kuteuliwa, hivi sasa wanasubiri vikao vya juu vya maamuzi kuamua nani kati yao atateuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kimojawapo kikongwe barani Afrika kwa ajili ya kuchuana na wagombea wa vyama vingine hususani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Vita hiyo ya kuwania kuwa mgombea wa CCM inawahusisha mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Federick Sumaye; Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda; Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal; Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan; Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa (TIS), Dk. Hassy Kitine na Balozi wa zamani wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Dk. Augustino Mahiga.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof.Mark Mwandosya; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha Rose Migiro; Waziri, wa Uchukuzi Samuel Sitta; Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Wamo pia Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe; Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani; Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Waziri wa Nishati na Madini aliyejiuzulu, Prof. Sospeter Muhongo; Balozi Ali Karume, Amos Siyantemi, Mussa Mwapango na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Makongoro Nyerere.
Wengine ni Balozi Patrick Chokala, Balozi Amina Salum Alli, Naibu Waziri wa zamani wa Fedha na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega; Ritha Ngowi, Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala; Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina; Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Malaria, Dk. Mwele Malecela; Idelphonce Bilohe, Boniface Ndengo, Leonce Mulenda,Banda Sonoko, Joseph Chaggama na Maliki Marupu.
WALIOKWAMA
Hata hivyo, baadhi ya waliojitokeza kugombea walipoteza sifa na kutupwa nje ya ulingo kabla ya kuanza kwa mchujo wa awali kutokana na kushindwa kurejesha fomu kwa wakati uliopangwa.
Wagombea hao ni Dk. Muzamil Kalokola, Hellena Dinah Elinewinga, Mwalimu Athony Chalamila na Peter Nyalali.
HALI ILIVYO DODOMA
Wakati wagombea wa kiti cha urais, ‘presha ikipanda na kushuka’ kutokana na hofu ya kukatwa majina na hivyo kukosa nafasi ya kuteuliwa; NIPASHE imeshuhudia mji wa Dodoma ukiwa umetapika watu kutoka kila kona ya nchi; huku pia barabara zikiwa hazipitiki kirahisi, na bei ya vyakula na vyumba vya kulala wageni vikiwa zimepanda bei maradufu.
Mathalan, bei ya vyakula kwenye migahawa iliyopo katikati ya mji wa Dodoma, ambayo hutumiwa zaidi na wananchi wa kawaida imepaa kutoka Sh. 2,500 hadi kufikia Sh. 4,000 kwa sahani moja; jambo ambalo limeufanya mji huo kuonekana ghali kimaisha.
Aidha, baa na kumbi za starehe zimefurika kutokana na kuendesha biashara kwa saa 24 kutokana na ujio wa watu wanaowaunga mkono wagombea wa kiti hicho wanaosubiri maamuzi ya vikao vya juu CCM kuamua nani atakayesimamishwa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
SHEIN APENDEKEZWA KWA KISHINDO
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amevuka hatua ya kwanza Zanzibar baada ya Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kumpendekeza kwa kauli ya moja kwa Kamati Kuu kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao kilichofanyika jana Makao Makuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar na kuongozwa na Mwenyekiti wa muda Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya kupokea jina la Dk. Shein baada ya kujitokeza kuomba achaguliwe kugombea nafasi hiyo mwaka huu.
“Baada ya kupokea jina na kujadili kikao cha Kamati Maalum ya Halmashaurin Kuu ya CCM Zanzibar kwa kauli moja tumependekeza kwa Kamati Kuu ateuliwe kugombea tena kiti cha urais wa Zanzibar.” alisema Vuai.
Alisema baada ya kazi hiyo kufanyika, hatua inayofuatia ni kuwasilishwa jina lake katika Kamati Kuu ya CCM kabla ya kujadiliwa na Halmashauri Kuu na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya uteuzi wa mwisho.
Kabla ya kufanyika kikao hicho, wajumbe wa Kamati Malum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar walimteua kwa kauli moja Dk. Bilal kuwa Mwenyekiti wa Kikao hicho na Dk. Shein kulazimika kupisha kikao kimjadili kabla ya kupendekezwa kugombea wadhifa huo.
Shangwe katika jengo hilo zilianza kujitokeza ikiwamo nyimbo za ‘CCM, CCM, CCM’ muda mfupi baada ya mwenyekiti wa kikao hicho kutangaza kuwa kwa kauli moja, wajumbe wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM wamependekeza kwa Kamati Kuu Dk. shein agombee tena nafasi ya Urais wa Zanzibar.
Akitoa shukurani baada ya kupendekezwa na kikao hicho, Dk Shein aliwashukuru wajumbe hao kwa uamuzi wao na kuahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi na serikali kwa uadilifu na uwazi kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
Aidha, Rais Dk. Shein aliwapongeza wajumbe wa NEC Zanzibar kwa kufanikisha kazi hiyo muhimu na nzito kwa mafanikio makubwa na kuahidi kuwa ataendelea kuwa mwadilifu katika kutumikia chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wagombea wa vyama vingine ambao tayari wametangaza nia ya kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar ni Katibu Mkuu wa Chama cha Tadea, Juma Ali Khatib, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid Mohamed (ADC), Mwenyekiti wa AFP, Soud Said Soud na Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ambar Khamis Haji.
CHANZO: NIPASHE

No comments :
Post a Comment