Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, August 26, 2015

Jiwe walilolikataa CCM limekuwa jiwe kuu Chadema



Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa
Injili inatufundisha kuwa enzi ya Yesu Kristo, baadhi ya watu walimwona ni kama kichaa na mvuruga amani katika jamii.
Wakati viongozi wakuu, wasomi na maadui zake wakimituhumu kwa utovu wa nidhamu, dhambi na mambo mengine, watu wa kawaida walizidi kumiminika na kumfuata.
Watanzania wa leo na hasa wanasiasa hawapendi kutumia maandiko matakatifu yanayopingana na matakwa yao au sera zao.Wanasiasa hupenda kutumia maandiko yale yanayotetea nafsi zao,masilahi yao na madaraka yao.
Mfano wa hili ni yale maandiko yasemayo: ‘’kila kiongozi anatoa mamlaka kwa Mungu kwa hivyo ni lazima kuyatii.” Lakini ukweli ni kwamba maneno ya Mungu ukiyatumia vibaya ni wazi lazima yatakuja kukugeuka muda si mrefu.
Kwa sababu maandiko matakatifu hasa Biblia ina majawabu yote yanayotafutwa na mwanadamu kwa sababu yanahusu historia ya mwanadamu na Mungu jinsi walivyotembea pamoja.
Ukitaka kujua kama unaendelea au la au upo sahihi katika mambo fulani ni lazima ulinganishe na mtu au kitu kingine au tukio fulani. Ukisikiliza hukumu za kesi mbalimbali utasikia hakimu ananukuu hukumu ya kesi iliyofanyika nchi fulani na hivyo kuifanya kama msingi wa hukumu anayoitoa. Wataalamu wanasema ‘hakuna jipya chini ya jua.’
Uchaguzi wa mwaka huu
Sasa tukirudi katika ulingo wa siasa za Tanzania na yanayotokea nyakati hizi hususani uchaguzi wa mwaka huu, tusifikiri ni tukio ambalo halijawahi kutokea popote duniani.
La hasha! itakuwa ni kujidanganya. Siyo siri kwamba tangu waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ahame CCM na kujiunga na Chadema, siasa za Tanzania zimebadilika, hili halina upinzani.
Sijui kama CCM walitabiri madhara ya kulikata jina lake mapema katika vikao vya juu vilivyofanyika kule Dodoma au na wao wanashangaa kama mimi.
Sasa hivi mazungumzo nchini Tanzania karibu kila kona ni Lowassa. Nilikwenda kuona wagonjwa hospitalini, nilikuta baadhi ya wagonjwa na mfanyakazi mmoja wakiwa katika mjadala mzito juu ya Mzee Lowassa. Mfanyakazi mmoja wa hospitalini hapo alitaka kupindisha ukweli, alipewa ukweli wake na wagonjwa waliokuwa karibu.
Walimwambia: “ Hatutaki kudanganywa kwani Lowassa kwa CCM kawa fisadi kwa vile ameondoka?” Hii ni alama wazi kwamba wananchi sasa wameanza kujitambua na kutambua kile kinachoendelea katika siasa zetu ikiwamo propaganda na porojo za kisiasa.
Ukweli ni kwamba kinachoonekana katika siasa za Tanzania kinalinganishwa na kilichotokea katika maisha ya Yesu. Alifanyiwa kila aina ya fitina, chuki, mizengwe hata akasalitiwa na rafiki yake Yuda na hatimaye akauawa kwa kutundikwa msalabani.
Kwa baadhi ya watu Yesu alionekana ni mzushi, alikuwa mchochezi katika jamii, alikuwa mvunja sheria za Wayahudi na mtu aliyekuwa anahatarisha amani ya jamii. Kuna mahali alifika akamponya mtu mwenye pepo kisha nguruwe wakaswagwa baharini.
Mzee Lowassa kajiondoa CCM na sasa amegeuka kuwa lulu na kivutio ndani ya Chadema, Ukawa na kwa Watanzania kwa jumla. Kwa mantiki hii kweli mzee Lowassa anaonekana kuwa kama jiwe lililokataliwa ndani ya CCM, lakini sasa limekuwa jiwe kuu ndani ya Ukawa.
Mzee Lowasa analaumiwa kuwa amekuwa akihonga ili watu wamuunge mkono katika harakati zake. Lakini kwa upande wangu ninashangaa kwani kadiri siku zinavyopita, watu wanaomuunga mkono wanaongezeka. Najiuliza hivi Lowassa ana fedha kiasi gani kuthubutu kuuhonga ule umati uliokusanyika Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na hatimaye mjini Mwanza juzi?
Hakuna mtu au kiongozi aliyelaaniwa hapa duniani na kuchafuliwa, kutukanwa, kudharauliwa na kusiginwa kama Yesu mwana wa Yusufu, lakini hata hivyo watu kila siku alipokuwa anakwenda walikusanyika mamia kwa mamia kinyume cha matakwa ya maadui zake.
Najiuliza wale wote wanaomfuata Lowasa ni wehu, vichaa, wajinga na wapumbavu? Kufikiri hivi itakuwa ni makosa na kujidanganya, itakuwa ni kutafuta majibu mepesi kwa maswali magumu. Kuleta porojo katika jambo nzito kama hili ni kujiaibisha mbele ya umma.
Huku ni kumfanya Mzee Lowassa aonekane kama ‘ jiwe lililokataliwa ndani ya CCM na sasa limeguka kuwa jiwe kuu ndani ya Ukawa.”
Katika hatua hii ya Mzee Lowassa kukihama Chama cha Mapinduzi na kujiunga na chama kikuu cha upinzani nchini, anaonekana kuhama na baadhi ya vigogo wa CCM. Na sasa ukweli unaanza kujitokeza juu ya uhai, uimara, mpasuko, udhaifu na upungufu ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika.
Kwa mantiki hii utabiri wa Mwalimu Julius Nyerere juu ya upinzani wa kweli kutoka ndani ya CCM yenyewe, unaendelea kutimia siku hadi siku.
Kwa upande wangu, nazidi kupata nguvu ya kuandika kwamba ‘CCM imegeuka mnara wa Babel’.
/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment