Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, August 26, 2015

Lowassa aleta kiwewe

NA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM
SHUGHULI za wafanyabiashara kwenye masoko ya Tandale, Tandika na Kariakoo jijini Dar es Salaam, zimesimama kwa muda jana baada ya mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kupita kwenye maeneo hayo.
Tofauti na juzi ambapo Lowassa alifanikiwa kufika kwenye kituo cha Daladala cha Gongo la Mboto bila kujulikana
na wananchi aliopishana nao njiani, jana baada ya kiongozi huyo kufika eneo la Tandale kwa Tumbo saa 3:11 asubuhi wakati akielekea Soko la Tandale, baadhi ya vijana waliokuwa eneo hilo waliweza kumbaini na kuanza kulifuata gari lake kwa nyuma.
Kitendo cha vijana hao kuulizana na kujijibu wenyewe, kilizua hamasa kwa madereva wa bodaboda ambao nao
walianza kuufuata msafara huo. “Kwanini hawatuambii jamani kama unakuja, tungejiandaa angalau kukupokea,” alisikika mmoja wa madereva wa bodaboda akisema wakati akiwa anaufuata msafara huo.
Wakati msafara huo ukielekea sokoni Tandale, tayari madereva wengine wa bodaboda walikuwa wametangulia mbele kuwaeleza wenzao kuwa kiongozi huyo yupo kwenye maeneo ya kwao jambo lililofanya wahamasike na kuanza kushangilia huku wakiwa wamenyoosha vidole viwili ikiwa ni alama inayotumiwa na Chadema.
Dakika tatu zilitosha kujaza watu kwenye barabara hiyo inayoelekea Soko la Tandale. Ilipotimia saa 3:18 asubuhi,
Lowassa bado alikuwa kwenye msafara huo, huku magari yakiwa hayaendi kutokana na msongamano wa watu
waliokuwapo barabarani.
Wakati msafara huo ukienda taratibu, umati huo ulikuwa ukiimba nyimbo mbalimbali, huku wakishangilia na kupiga miluzi zikiwamo; “Rais…Rais… Rais…’, ‘Lowassa asante baba kututembelea’, ‘Wewe ndiye rais wetu, Magufuli atafute pa kutokea’ na nyingine.
Saa 3:21 Lowassa alishuka ndani ya gari lake aina ya Noah lenye namba ya usajili T 607 DDR akiwa na mgombea
mwenza, Juma Duni Haji na kuwasalimia wafanyabiashara wa soko la Tandale ambapo wengine walikuwa wakiimba
‘wewe ndiye tumaini letu’ huku wengine wakiwaambia wenzao wampishe ‘rais’ akanunue maharage ya soya.
Akiwa sokoni hapo, Lowassa alianza kumsalimia mfanyabiashara Said Omari na kumuhoji kuhusu changamoto anazokumbana nazo.
Mahojiano baina ya Lowassa na mfanyabishara huyo ni kama yafuatavyo:
Lowassa: Vipi biashara inaendaje?
Omari: Biashara ni mbaya. Vitu vinapanda bei kila kukicha.
Lowassa: Tufanye nini ili maisha yako yawe bora zaidi?
Omari: Tunaomba tuboreshewe miundombinu, pembejeo, soko likiwa la kisasa na biashara yetu itakwenda vizuri. Lakini mheshimiwa ukiangalia soko letu ni la kizamani sana. Lakini tukiimarishiwa hata hali ya biashara yetu itaimarika.
Lowassa: Unalipa kodi shilingi ngapi?
Omari: Hapa tunalipa ushuru wa manispaa.
Lowassa: Huwa unapata shilingi ngapi kwa siku?
Omari: Wakati mwingine napata shilingi 30,000, 20,000, 10,000. Inategemeana na biashara ilivyokwenda siku hiyo.
Lowassa: Kilo moja ya maharage ni shilingi ngapi?
Omari: Kilo moja nauza shilingi 1,800.
Lowassa: Naomba unipimie kilo kumi za maharage.
Baada ya mahojiano hayo yaliyodumu kwa dakika takribani saba, Lowassa alipimiwa kilo kumi za maharage ambapo alimkabidhi mfanyabiashara huyo shilingi 18,000.
Wakati Lowassa akikabidhiwa maharage hayo, Duni naye aliomba kupimiwa kilo kumi na kulipa shilingi 18,000 kama alivyofanya Lowassa.
Katika hali ya kushangaza, wakati Lowassa akimkabidhi msaidizi wake ambebee mfuko huo wa maharage, ghafla
ukakatika na kusababisha wananchi kugombania maharage hayo wakiyazoa.
AELEZEA FURAHA YAKE Akizungumza na MTANZANIA baada ya kumaliza mahojiano na Lowassa, Omari alieleza furaha yake akisema imekuwa kama neema kwake kutembelewa na kiongozi mkubwa wa aina hiyo na kununua bidhaa yake.
“Kwa kweli furaha niliyonayo siwezi kuielezea. Nimefurahi mno, nahisi neema imenishukia leo.
Lowassa na Duni wamenunua jumla ya kilo 20, nimefarijika sana. Kweli huyu ndiye kiongozi anayetufaa, Mungu amwongoze,” alisema mfanyabiashara huyo.
Alisema hawajawahi kutembelewa na kiongozi mkubwa katika soko hilo, na kwamba Mungu amjalie Lowassa apate urais ili maisha yao yawe mazuri kwani wameichoka Serikali iliyopo madarakani.
Mfanyabiashara mwingine
aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Mohamed, akizungumza na MTANZANIA, alisema wameburuzwa kwa muda mrefu na Serikali iliyopo madarakani, hivyo matumaini waliyoyategemea sasa yamewadia.
“Tuna imani na Lowassa, tumeteseka sana kwa muda mrefu, lakini sasa ni tumaini letu kuwa mwanasiasa huyo mkongwe atatuvusha na kutuletea maisha mazuri,” alisema Mohamed.
MWENYEKITI WA SOKO ANENA
Baada ya Lowassa kumaliza mahojiano na Omari, aliuliza kama diwani yupo maeneo hayo, lakini alijibiwa kuwa
hayupo, ndipo alipotokea mwenyekiti wa soko hilo, John Barua.
Lowassa alianza kumhoji mwenyekiti huyo kama ifuatavyo:
Lowassa: Mfanyiwe nini ili biashara yenu iende vizuri?
Barua: Utaratibu ni mbovu kuanzia miundombinu na pembejeo, tungepewa fursa, kwanza haya majengo tuliyajenga sisi lakini kwa sasa yapo mikononi mwa manispaa.
Lowassa: Je, mkiachiwa mtaweza kuendesha wenyewe?
Barua: Kabisa. Yakiwa mikononi mwetu tutaweza ila tunachoomba ni kwamba mabadiliko yafanyike.
Wakati akiendelea kuwatembeleawafanyabiashara wengine, msongamano wa watu ulizidi kufurika katika eneo hilo
la soko.
Mmoja wa watu waliokusanyika eneo hilo alilalamika akisema: “Jamani nilitaka nimpe mkono, lakini Wapambe wake wamenizuia. Lakini kura yangu nitampatia… Tumekuelewa mzee.”
Mwingine alisikika akisema: “Watake wasitake, mwaka huu huyu ndiye rais wetu… asante baba kwa kuja, Mungu
akusaidie.”
Katika hali iliyoshangaza wengi, Lowassa alimfuata mama mmoja ambaye alikuwa anauza uji na chai ambapo aliomba ampatie uji.
Alipopimiwa uji kwenye kikombe, Lowassa alikunywa na kumkabidhi mama huyo Sh 10,000.
Kitendo cha Lowassa
kuinua kikombe na kunywa uji huo, mama huyo alipiga kelele huku akirukaruka asiamini anachokishuhudia, huku
watu waliokuwapo jirani nao wakishangilia.
Ilipotimu saa 3:43 asubuhi, Lowassa alianza kuondoka katika eneo hilo la soko huku umati wa watu ukisukuma
gari lake na mmoja wao akisema; “CCM wajinyonge… si wanatuita wapumbavu sasa wanatutambua mwaka huu.”
Umati huo wa watu
ulisukuma gari la Lowassa kwa kilomita takribani moja na nusu kabla msafara huo kuingia Barabara ya Morogoro.
BODABODA WAGEUKA TRAFIKI
Katika hali ya kushangaza waendesha bodaboda walikuwa wakiyazuia magari mengine, huku wakisimamisha pikipiki zao, wakisema ‘acheni rais apite’.
Msafara huo ambao ulikuwa umepangwa kuelekea katika soko la Kariakoo, uliacha barabara ya Morogoro na kupita ya vumbi iliyotokea Kigogo Polisi, wakihofia kuzuiwa na polisi kutokana na kufuatwa na idadi kubwa ya bodaboda.
Lowassa na msafara wake walipofika eneo la Mburahati, vijana wa bodaboda waliokuwapo kwenye vituo vyao, walijikuta wakiunga msafara huo.
/Mtanzania.

No comments :

Post a Comment